Majeruhi wa bodaboda bado janga MOI

Muktasari:

  • Takriban majeruhi 20 hadi 25 hupokelewa kwa siku, katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).

Dar es Salaam. Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) imesema majeruhi wengi wa bodaboda wanaofikishwa katika taasisi hiyo wana mivunjiko mikubwa na ndiyo inayosababisha gharama kubwa za matibabu.

Kulingana na MOI, uchunguzi wa hivi karibuni umebaini kwa siku taasisi hiyo inapokea majeruhi 20 hadi 25.

Hayo yameelezwa hivi karibuni na Daktari Bingwa Mbobezi wa Mifupa MOI, Dk Joseph Mwanga wakati akielezea matukio yanayohusisha majeruhi wa bodaboda wanaopokelewa kwenye taasisi hiyo.

“Majeruhi huvunjika vibaya sana, mtu huyu atatumia muda mwingi na gharama kubwa kujitibia, wakati nwingine kama sio kifo basi anaweza asirejee katika hali yake ya kawaida…kundi hili la bodaboda na bajaji ndilo linaloongoza kwa ajali,” amesema.

Amesema asilimia 60 ya majeruhi hao wanatokana na bodaboda na wanaopokelewa katika kitengo cha dharura MOI.

Kwa mujibu wa takwimu za taasisi hiyo, asilimia 30 ya majeruhi hao wanatokana na ajali za gari na asilimia 10 ni ajali nyingine.

“Ajali hizi za pikipiki zinaongoza kusababisha majeruhi na wanaume ndilo kundi linaloathirika zaidi kwa asilimia 70, majeruhi wengi wa bodaboda hupata mivunjiko mikubwa ya mifupa hali inayochangia ukubwa wa gharama za matibabu,” amesema.

Dk Mwaga amesema kwa miaka 18 iliyopita kitengo cha dharura cha MOI kilikuwa kinapokea majeruhi watatu hadi watano kwa siku, ukilinganisha na sasa ambapo majeruhi 20 hadi 25 hupokelewa kwa siku.

Septemba 29, 2023 katika maadhimisho ya siku ya moyo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema changamoto inayowakabili wanaofanya mazoezi barabarani ni kupoteza maisha kwa ajali za bodaboda.

Ili kutatua changamoto hiyo amesema atawasilisha ombi kwa Waziri Mkuu Kassim Majliwa ili barabara zinazojengwa ziwe rafiki kwa wananchi wanaofanya mazoezi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria watu milioni 1.9 hupoteza maisha kutokana na ajali za barabarani na ndizo zinazoongoza kwa vifo vya watoto na vijana kuanzia miaka mitano hadi 29.

Kulingana na shirika hilo, asilimia 92 ya vifo vinavyotokea barabarani ni katika mataifa yanayoendelea na zaidi ya nusu ya waathirika wa ajali hizo ni watumiaji wa barabara.

WHO inasema ajali za barabarani hutumia asilimia tatu ya pato la taifa kwa mwaka.