Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majeruhi wafunguka  ajali iliyoua tisa Singida

Majeruhi wa ajali iliyotokea usiku wa kuamkia jana Mkoani Singida   Frank Masanja akiendelea kupatiwa matibabu. Picha na Jamaldin Abuu


 

Muktasari:

 Katika ajali hiyo, watu tisa walipoteza maisha huku 19 wakijeruhiwa na kuwahishwa  katika Hospitali za Iramba, na ya rufaa ya mkoa wa Singida kwa matibabu zaidi.

Singida. Baadhi ya majeruhi walionusurika kwenye ajali ya basi la Kampuni ya Lujiga Express mkoani Singida, wameeleza kuwa gari walilokuwa wakisafiria lilikuwa bovu, jambo lililosababisha safari yao kuchelewa.

Katika ajali hiyo iliyotokea Aprili 10, 2024, watu tisa walipoteza maisha huku 19 wakijeruhiwa na kupelekwa  katika hospitali za Iramba na hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida kwa ajili ya matibabu zaidi.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 11, 2024 wakiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, majeruhi hao wamesema walianza safari kutoka Dar es salaam saa 3 asubuhi badala ya saa 12 asubuhi, kutokana na ubovu wa gari hilo.

Frank Masanja (35), mkazi wa Dar es salaam aliyekuwa akielekea Kahama, amesema waliambiwa gari linaondoka saa 12 asubuhi lakini hadi kufikia saa 2 asubuhi bado walikuwa hawajatoka, jambo lililosababisha baadhi yao kutaka kuahirisha safari, hata hivyo walianza safari saa 3 asubuhi na walitumia muda mrefu Morogoro kwa ajili ya matengenezo.

“Ilikuwa saa 11 alfajiri, sasa tulipofika sijui sehemu gani ile, yule dereva sijui alikuwa anasinzia, lile basi lilimsumbua sana, kwenye tiketi walikuwa wameandika saa 12 kamili lakini hadi kuja kutoka ilikuwa saa 3 kasoro asubuhi, hadi abiria wengine tukashuka chini,” amesema.

Amesema walipofika Dumila, gali lilijaa moshi ndani, hali iliyowatisha na kudhani linataka kuungua, baadhi ya watu wakatokea dirishani.

Kwa upande wake, mkazi wa Dar es Salaam, Dorothea Kazimili (35) amesema kabla ya kuanza safari, roho yake ilikuwa inasita kusafiri na gari hilo kutokana na moshi mwingi uliotoka, jambo lililowafanya watake gari likaguliwe na askari, hatimaye askari alikuja akafanya hivyo na kuendelea na safari.

“Lile gari lilikuwa ni bovu, tuseme mara ya kwanza lilitaka kuwaka wakaweka  maji, likatengemaa, tukasema sisi hatuendelei na safari kwa kweli, labda muite mtu wa kulihakiki hili gari, wakaita askari akalihakiki, wakasema tunaweza kuendelea na safari lakini mimi roho yangu ilikuwa inasitasita,” amesimulia.

Mkuu wa Idara ya Upasuaji kutoka Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Singida Dk Wilson Masuke. Picha na Jamaldin Abuu

Kwa upande wake, mkuu wa idara ya upasuaji katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida, Dk Wilson Masuke amesema katika majeruhi 11 waliowapokea, mmoja aliyetambulika kwa jina la Steve Mgeni (45) amepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa mkoani Dodoma kutokana na hali yake kuwa mbaya, huku wakitarajia kumpa ruhusa mmoja na wengine hali zao zikiendelea kuimarika.

Amesema miili miwili waliyoipokea imetambulika kama Lutobola Charles ambaye tayari ndugu zake wamejitokeza pamoja na Peter Mahona ambaye bado yupo chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo, kutokana na ndugu zake kutojitokeza hadi sasa.

Akiizungumzia ajali hiyo hapo jana Mkuu wa wilaya ya Singida, Godwin Gondwe alisema basi hilo lilikuwa likitokea Dar es salaam kuelekea mkoani Mwanza lilikuwa na jumla ya abiria 56.