Makada 30 wanaotaka kumrithi Ndugai hawa hapa….

Katibu Msaidizi Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni CCM Taifa, Solom Itunda akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Muktasari:

Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kukiwakilisha chama hicho kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania wamefika 30.

Dodoma. Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kukiwakilisha chama hicho kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania wamefika 30.

Idadi hiyo imetimia leo Januari 12, 2022 baada ya wengine 13 kujitokeza kuchukua fomu hizo ambapo kwenye Ofisi za makao Makuu ya CCM Dodoma wamejitokeza saba, ofisi ndogo ya Dar es Salaam watano na ofisi ya Zanzibar akichukua mmoja.

Akitoa taarifa hiyo leo Januari 12, Katibu msaidizi mkuu Idara ya Oganaizesheni CCM Taifa, Solomon Itunda amewataka wanachama hao kuendelea kujitokeza katika siku zilizobaki.

Wanachama waliojitokeza mpaka sasa kuomba kuteuliwa  kuwania nafasi hiyo katika ofisi za Dar es Salaam ni Mbunge wa Geita Vijijini Joseph Musukuma, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa umoja wa wanawake Tanzania (UWT) Sophia Simba, Patrick Nkandi, aliwahi kuwa mbunge wa Shinyanga Mjini Stephen Masele na Hamidu Chamani.

Wengine ni Godluck Medee, Juma Chum, Baraka Byabato, Festo John, George Nangale, Wakili na Mwanadiplomasia Barua Mwakilanga, Zahoro Hanuna, aliyewahi kuwa Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge, Thomas Kirumbuyo na Angelina John.

Kwa upande wa Ofisi za makao makuu ya chama hicho jijini Dodoma waliojitokeza ni Dk Simon Ngatunga, aliyewahi kuwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Sikonge, ofisa vijana mwandamizi mkoa wa Dodoma Tumsifu Mwasamale, aliyewahi kuwa ofisa tawala mwandamizi wa Wizara ya Fedha idara ya Mhasibu mkuu wa Serikali, Merkion Ndofi na Mbunge wa Mlimba Morogoro Godwin Kunambi.

Wengine ni Naibu Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson, Abwene Kajula, Mbunge wa Ilala Mussa Zungu, Mbunge wa Tabora Mjini Emmanuel Mwakasaka, Profesa Handley Mpoki, Dk Mussa Ngonyani, Hamisi Saidi ambaye ni mjumbe wa Halmashauri kuu CCM Tanga, Asia Abdallah na aliyewahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo Dk Titus Kamani.

Katika ofisi za Zanzibar, Mhandisi Abdulaziz Jaad Hussein ndiye ambaye amechukua fomu.