Makada Chadema wadaiwa kukamatwa Mwanza, Polisi yasema....

Katibu wa Chadema wilaya ya Nyamagana, David Nyakimwe

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linadaiwa kumkamata Katibu wa Chadema wilaya ya Nyamagana, David Nyakimwe na mwanachama wa chama hicho, Oswald Mang'ombe wakati wakiendelea na maandalizi ya mkutano wa hadhara uliotarajiwa kufanyika uwanja wa shule ya msingi Mabatini jijini Mwanza.

Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linadaiwa kumkamata Katibu wa Chadema wilaya ya Nyamagana, David Nyakimwe na mwanachama mwingine wa chama hicho, Oswald Mang'ombe wakati wakiendelea na maandalizi ya mkutano wa hadhara uliotarajiwa kufanyika uwanja wa shule ya msingi Mabatini jijini Mwanza.

Akizungumza leo Jumapili, Septemba 4, 2022 na Mwananchi Digital kwa simu, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amesema wanachama hao wamekamatwa asubuhi ya leo wakiendelea na maandalizi ya eneo ulipotakiwa kufanyika mkutano huo.

Obadi amesema pamoja na kutoa taarifa Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Nyamagana kwamba mkutano huo utafanyika leo katika viwanja vya shule hiyo lakini anashangaa kuona jeshi hilo linawakamata wanachama wake.

"Tulifuata taratibu zote, tukatoa taarifa kwa OCD wa Nyamagana hawakutupa mrejesho kwamba haturuhusiwi kufanya hivyo. Matokeo yake wanawakamata wanachama wetu, kwa nini iwe Chadema peke yake wakati viongozi wa vyama vingine wanafanya mikutano hii," amesema Obadi

 "Pamoja na kuendelea na mikutano ya maridhiano kati ya vyama vya siasa vya upinzani na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuponya makovu tuliyonayo, nashangaa kuona mambo ambayo tulidhani yatakomeshwa yanaendelea kutokea."

Mwanchi Digital imezungumza kwa simu na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya kuhusu tukio hilo ambapo amesema hana taarifa za kukamatwa kwa wanachama hao wa Chadema kutokana na kuwa nje ya ofisi.

Msuya ameahidi kufuatilia suala hilo na kutoa mrejesho wa hatua za kuchukua atakapokuwa amejiridhisha iwapo wanachama hao wamekamatwa.

Kuhusu Chadema kutoa taarifa ya kuwepo mkutano huo, Msuya amekanusha chama hicho kutoa taarifa ya kuwepo mkutano huo huku akisisitiza kufanya mkutano wa hadhara bila kibali ni kinyume na sheria.

"Muulize vizuri aliyekwambia kwamba ametoa taarifa ya kufanya mkutano huo, sisi hatujapokea taarifa hiyo kama tungeipokea tungewajibu," amesema Msuya

Mkutano huo uliotakiwa kuanza leo alasiri na kuhutubiwa na viongozi mbalimbali wa Chadema akiwemo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chademaz John Heche, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Pambalu na viongozi wengine wa Kanda ya Victoria.