Makali ya tozo za miamala kilio, kicheko

Muktasari:

  • Maumivu yaliyokuwa yanalalamikiwa na wananchi juu tozo kwenye miamala ya kieletroniki kitapungua siku tisa zijazo baada ya Serikali kutangaza kufuta na kupunguza viwango vyake.

  



Dodoma/mikoani. Maumivu yaliyokuwa yanalalamikiwa na wananchi juu tozo kwenye miamala ya kieletroniki kitapungua siku tisa zijazo baada ya Serikali kutangaza kufuta na kupunguza viwango vyake.

Badala yake, nakisi ya Sh500 bilioni kwenye bajeti iliyokuwa itokane na tozo hizo, itafidiwa kutokana na kubana matumizi mengineyo ndani ya Serikali kama kukata kwenye chai, vitafunwa, misafara ya ndani na nje kwa maofisa wa wizara, semina, matamasha na warsha.

Uamuzi huo uliosubiriwa kwa takribani mwezi mmoja, ulitangazwa jana bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na kupokelewa kwa hisia tofauti na wananchi, wanasiasa, wachumi, viongozi wa dini na asasi za kiraia.

Wadau hao walisema hatua hiyo ni funzo kwa Serikali inapopanga jambo linalowahusu wananchi, iwashirikishe kuanzia mwanzo hadi mwisho ili kuepuka hili lililotokea na kuzua mijadala mpana.

Tozo hizo za miamala ya kieletroniki zilianza kutumika Julai mosi, mwaka huu zikiibua hoja ya kuwepo makato mara mbili, jambo ambalo lilipingwa na wananchi kwamba ni kinyume cha sheria.

Akitangaza uamuzi huo, Dk Mwigulu alisema Serikali imepunguza wigo wa tozo, kuchochea matumizi ya miamala ya kielektroniki ili kupunguza fedha taslimu, kurahisisha utozaji na kuzuia kutoza tozo mara mbili.

“Marekebisho yaliyofanyika ni kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu (pande zote) na kufuta tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja (pande zote),” alisema.

Alitaja marekebisho mengine ni kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda benki nyingine (pande zote).

Alisema wamesamehe tozo ya miamala kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia wakala wa benki na ATM kwa miamala yenye thamani isiyozidi Sh30,000.

Vilevile alisema wamepunguza gharama ya miamala kwa asilimia 10 hadi asilimia 50 kufuatana na kundi la miamala.

Serikali imelazimika kuchukua uamuzi huo, licha ya kwamba ilitarajia kukusanya takriban Sh500 bilioni kutokana na tozo ya miamala ya simu na benki.

Fidia maumivu

Ili kufidia nakisi hiyo kwenye bajeti, Serikali itabidi ijibane katika matumizi ambayo Mwigulu alisema hayataathiri utekelezaji wa majukumu ya msingi ya mafungu husika.

Alimtaka mlipaji mkuu wa Serikali kukaa na maofisa masuuli wote kuyaangalia upya mafungu ya matumizi mengineyo ili miradi ya maendeleo yote isiathirike kwa hatua hiyo.

“Tukate kwenye chai, vitafunwa, misafara kwenye safari za ndani na nje kwa maofisa wa wizara zetu kama Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) alivyoelekeza, tukate mafunzo, semina, matamasha na warsha,” alisema.

Alisema fedha hizo pia zitakatwa kwenye makundi yanayokwenda kukagua mradi uleule kwa nyakati tofauti au makundi yanayokwenda eneo lilelile kila mtu na gari lake (mfano, wilaya ileile kila ofisa na gari peke yake, mkoa uleule kila kiongozi) na gari lake pekee yake.


Matumizi ya tozo

Waziri Mwigulu alisema fedha za tozo zilipangwa kuelekezwa katika ujenzi wa madarasa 8,000 nchi nzima ambako mahitaji yanakadiriwa kuwa 17,000.

Alisema mipango mingine ni kujenga vyuo 72 vya Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (Veta) kwenye wilaya ambazo hazina na kutekeleza mpango wa elimu bila ada kwa kidato cha tano na sita.

Mipango mingine ni kuendelea na ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na vifaa tiba katika maeneo ambayo bado hakuna huduma hizo.

Imetusaidia

Kutokana na uamuzi huo, Tumaini Nyamhokya, rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), alisema wao kama wafanyakazi wanashukuru kwa sababu kilio chao kimesikika na kufanyiwa kazi.

“Kelele yetu kubwa ilikuwa benki, sehemu ambayo mishahara yetu inapitia. Wametugusa na imetusaidia, tutatoa tamko rasmi juu ya uamuzi huu wa Serikali,” alisema Nyamkohya.

maoni mengine yametolewa na Profesa Haji Semboja, mchumi mbobevu na mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa katika uanzishwaji wa vitu mbalimbali ikiwemo tozo ni vyema mfumo ufuatwe ili kuonyesha kile kinachoanzishwa kimefuata sera na sheria.

Profesa Semboja alisema hilo litaondoa kubadilibadili maamuzi kila mara.

Tofauti na maoni ya Profesa Semboja, Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, yeye alishauri Serikali iachane kabisa na tozo akisema zinaingilia uhuru wa watu kutumia fedha zao.

“Wananchi wanapofanya biashara wanalipa kodi, bado wanapofanya matumizi ya kawaida wanakutana na tozo hii si sawa. Serikali iendelee na kodi na iachane na suala la tozo,” alisema.

Askofu huyo alishauri Serikali kabla ya kufanya mabadiliko katika mambo mbalimbali yanayokwenda kumgusa mwananchi moja kwa moja, iwashirikishe wanaoguswa ili waweze kutoa maoni yao kuepusha malalamiko yanayoweza kujitokeza baadaye.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheik Khamis Mataka aliipongeza hatua hiyo ya Serikali akisema inaonyesha ni kwa namna gani Serikali ni sikivu kwa wananchi wake.

“Kipimo cha Serikali sikivu ni kusikiliza wananchi wake, hivyo uamuzi huo unaonyesha kuwa ni sikivu na hilo ni jambo jema,” alisema.

Hata hivyo, Mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa alipotaakiwa kutoa maoni yake alisema, “hilo liwe funzo kwa viongozi wetu kuwa jambo lolote linalohusu maisha ya Watanzania ni vyema kabla ya kufikia maamuzi washirikishe wadau, asasi za kiraia pamoja na wananchi wenyewe ili pale linapotolewa maamuzi kusitokee manung’uniko na malalamiko.”

Wachumi watofautiana

Katika mtazamo wa kiuchumi, wataalamu wa uchumi wametofautiana katika maoni yao juu ya kile kilichofanyika.

Mhadhiri Mwandamizi Chuo kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Lawi Yohana alisema pamoja na kuwa hatua hiyo ya Serikali ni mwanzo mzuri, bado kuna mambo yanapaswa kufanyiwa kazi.

“Kuna makato wakati wa kutoa fedha taslimu hayakutajwa, eneo lililoguswa ni tozo wakati wa kufanya miamala, lakini tozo wakati wa kumtumia mtu fedha ipo palepale.

“Walichokifanya ni kuondoa tozo wakati wa kufanya muamala kati ya benki na benki na kati ya benki na simu, hatua zichukuliwe zaidi,” alisema.

Dk Lawi alisema hatua zaidi ya kupunguza tozo zichukuliwe kwani athari zaidi zinakwenda kwa wananchi wa kawaida ambao tayari wanapitia ugumu wa maisha uliochangiwa na sababu mbalimbali.

Mchumi mwingine, Dk Abel Kinyondo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema kilichofanyika kinakwenda kuwa na faida katika benki lakini hakijamgusa moja kwa moja mwananchi wa kawaida aliyekuwa akilalamika hadi hatua kuchukuliwa.

Kutokana na hilo, aliwataka wananchi na wadau wa maendeleo kujenga utaratibu wa kupinga vitu kabla ya kusomwa bungeni kwa kuwa vikishapitishwa inakuwa ni ngumu kuviondoa.

“Ukiondoa kitu kama tozo kwa sasa unaharibu bajeti ya mwaka mzima, tukitoa tozo kitu fulani na fulani kimeshaanza tutakifanikisha vipi,” alisema.

Hata hivyo, Dk Donath Olomi, mtaalamu wa uchumi na biashara alisema marekebisho hayo yatasaidia kurudisha watu katika mfumo rasmi wa huduma za kifedha kwa kiasi.

“Ni jambo zuri, ilifanya watu wakwepe kutumia mifumo rasmi ya fedha ambayo ingepelekea kuharibu uchumi, hili lililofanyika linaweza kuongeza mapato kwa kuwa watu watatumia zaidi,” alisema.

“Wanaweza kupunguza kiwango cha tozo lakini wakapata mapato zaidi kwani watu wengi watatumia huduma hiyo na hii itaondoa athari ambazo zingeweza kupatikana katika uchumi ikiwemo watu kutumia muda kupeleka fedha sehemu nyingine au kuweka fedha ndani,” alisema Dk Olomi.

Furaha na huzuni

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema wameupokea uamuzi huo kwa furaha kwa kiasi fulani na pia kwa huzuni.

Alisema marekebisho hayo hayawasaidii Watanzania walio wengi kwani yamejikita zaidi kwenye miamala ya kibenki ambako si wananchi wengi wanaotumia huduma hizo, badala ya kwenye simu ambako ndiko kuna watumiaji wengi na wa hali ya chini.

Hivyo, alisema wataendelea na kesi waliyofungua kupinga tozo hizo kama kawaida wakihoji uhalali wa tozo hizo na si kiwango chake.

Henga alisema hata hivyo wamefurahishwa na uamuzi wa Serikali kuelekeza kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa viongozi na kushauri kwamba huko ndiko Serikali ingelekeza nguvu kwani kuna pesa nyingine zinatumika vibaya, ambazo zingeweza kutumika badala ya tozo.

LHRC ilifungua shauri Septemba mosi mwaka huu, dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ikiomba ridhaa ya kufungua shauri ili mahakama ipitie na kisha kutengua kanuni za Sheria ya Malipo ya Taifa zinazoweka tozo.

LHRC inadai kanuni hizo zimetungwa bila kufuata taratibu zilizoainishwa katika Katiba ya nchi

Shauri hilo linalosikilizwa na Jaji Sekela Moshi limepangwa kuanza usikilizwaji Oktoba 4, mwaka huu.


Walichokisema wabunge

Nje ya viwanja vya Bunge, wabunge walikuwa na maoni tofauti kuhusu utekelezaji, japokuwa wote waliunga mkono suala hilo.

Wabunge walishauri Serikali iwe na inafanya utafiti kwanza kabla ya kufanya uamuzi ili kuepusha kurejea mezani kuanza upya.

Kauli za wananchi

Wakala wa mtandao ya simu wa Moshi mkoani Kilimanjaro, Hellen Mosha alisema tatizo lililopo ni kufanya mambo bila kujiridhisha kwa kufanya tafiti kwanza.

Hellen anaungwa mkono na Mkazi wa Manispaa ya Morogoro, Consolatha Costatine (22) aliyesema tozo hizo ni mzigo zaidi kwa wananchi kutokana na kuelemewa na maisha.

Mkazi wa Malimbe jijini Mwanza, Jamson Mnagwa alisema ni jambo jema kuondolewa kwa tozo za miamala ya benki, kwa kuwa zitatupunguzia ukali wa maisha wananchi.

Mkazi wa Geita, Ikorongo Oto alisema tozo iliyopunguzwa ni kwa watu wenye uwezo wa wanaotunza fedha benki lakini si kwa wananchi wa kawaida.

Imeandikwa na Sharon Sauwa (Dodoma) Saada Amir na Daniel Makaka (Mwanza), Robert Kakwesi (Tabora), Beldina Nyakeke (Musoma), Ernest Magashi (Bukombe) na Rehema Matowo (Geita), Hawa Mathias (Mbeya), Juma Mtanda (Morogoro), Fina Lyimo (Moshi), Mussa Juma (Arusha), Emmanuel Msabaha, Mariam Mbwana, Tuzo Mapunda na Aurea Simtoe, James Magai (Dar).