Makalla atangaza mgawo wa maji Dar

Muktasari:

  • Hatimaye Serikali imetangaza mgao wa maji katika jiji la Dar es Salaam kutokana na upungufu wa maji katika vyanzo vya maji vya Ruvu Chini na Ruvu Juu kulikosababishwa na ukame.

Pwani. Wakati Serikali ikitangaza kuanza kwa mgawo wa maji jijini Dar es Salaam, sababu ya kutokea shida ya maji kila unapofika mwisho wa mwaka imeelezwa.

Akizungumza leo Jumanne Oktoba 25 baada ya kutembelea vyanzo vya vya kuzalisha maji vya Ruvu Chini na Ruvu Juu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema sababu ni kupunguza kwa uzalishaji wa maji unaotokana na ukame.

Makalla aliyewawakilisha pia wakuu wa mikoa ya Pwani na Morogoro amesema hali sio nzuri kwani kina cha maji cha vyanzo hivyo vyote kimepungua huku uzalishaji ukipungua kutoka lita za ujazo milioni 466 kwa siku hadi kufika lita milioni 300 sawa na asilimia 64 ya uzalishaji wote wa maji.

"Naomba niwaambie wananchi kuwa mgao haupekuki kutokana na ukame ambao tayari TMA ilishatangaza kuwepo kwa hali hii muda mrefu kulikosabbisha na kunyesha kwa mvua chache msimu wa mvua uliopita na kuchelewa kunyesha kwa mvua katika msimu huu wa vuli.

"Pia watu waelewe hali hii haisababishwi na Serikali wala sera za CCM bali ni mipango ya Mungu, hivyo asitokee mtu huko akaanza kupotosha huko, kikubwa tuendelee kumuomba Mungu atuletee mvua za vuli na vyanzo vyetu vya maji viweze kujaa,” alisema Makalla.

Aidha jitihada nyingine ambazo serikali imezifanya Makalla alisema kuanzi Mkoa wa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, kamati zote za ulinzi na usalama zimewadhibiti watu wote ambao walikuwa wakichepusha maji na sasa kisingizo cha kuwa ni wao wanaosababisha uhaba wa maji hakipo.

Pia kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani amewaomba kutumia vizuri maji yanayopatikana ili yaweze kuwafaa kwa nyakati hii.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Dawasa, Cyprian Luhemeia alisema watatoa ratiba za mgao huo siku sio nyingi.

Kwa mujibu wa Dawasa kupitia maofisa Mtendaji wake, Luhemeja, Maji yanayohitajika kwa jiji la Dar es Salaam kwa siku ni lita za ujazo milioni 500 hivyo kufanya kuwa na uhaba wa lita 200 kwa sasa.


Katika ziara hiyo, Makalla aliongozana na bodi ya Dawasa pamoja na Wakuu Wilaya ne Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Lubigija, Mkuu wa Wilaya Kigamboni, Fatma Almas, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Heri James na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe.

Alipotafutwa Naibu Waziri wa Maji Maryprisca Mahundi kuzungumzia mikakati ya Serikali kukabiliana na adha hiyo ambayo inaonekana kuanza kuwa sugu katika miezi ya mwisho wa mwaka alijibu kwa kifupi,

“Kama ulimsikiliza vizuri aliyetangaza hiyo, majibu yako wazi hiyo ni natural calamities (majanga ya asili), hata hivyo nipo kikaoni,” alisema na kukata simu.