Makalla: Hali ya maji tumwachie Mungu

Friday November 26 2021
hali majipic

Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira ( DAWASA), Cyprian Luhemeja (mbele) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla aliyekuwa ameambatana na viongozi kadhaa wa mkoa huo walipofanya ziara kukagua vyanzo vya maji vya Ruvu chini na Ruvu juu na kukagua hali ya uzalishaji na usambazaji wa maji jana. Picha na Nasra Abdallah

By Nasra Abdallah

Kibaha. Huenda uhaba wa maji jijini Dar es Salaam ukaendelea kwa muda kutokana na mtiririko wa Mto Ruvu kutorudi katika viwango vinavyotakiwa.

Mwezi uliopita, siku chache baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutangaza upungufu wa mvua nchini, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) ilitangaza kupungua kwa maji katika Mto Ruvu Chini kutoka lita milioni 520 zilizokuwa zinapatikana awali hadi lita milioni 460 kila siku.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla jana alitembelea mto huo na kukiri kwamba hali bado si shwari na kilichopo ni kuomba kudra za Mwenyezi Mungu, kwani mkoa wake unategemea maji kutoka Mto Ruvu Chini uliopo Bagamoyo na Mto Ruvu Juu uliopo Kibaha.

“Yale ya kibinadamu tumeshafanya kwa uwezo wetu, ikiwamo kuwasaka wachepushaji maji, kilichobaki ni kudra za Mungu. Tumekuja hapa kuona hali halisi ili mkoa uwe mabalozi wazuri wa kuwaeleza wananchi nini kinachoendelea, kwani ukiona kitu kwa macho ni rahisi kuwaeleza watu kuliko kuelezewa,” alisema Makalla.

Katika ziara hiyo, Makalla aliongozana na wakuu wa wilaya zote tano za Dar es Salaam, akisema licha ya juhudi zilizochukuliwa, bado hali si nzuri kutokana na kukosekana kwa mvua.

Kwa uzoefu wake, akiwa Naibu Waziri wa Maji kwa miaka miwili, alisema mahitaji ya maji kwa Dar es Salaam yalikuwa ni zaidi ya lita milioni 540, lakini uzalishaji ulikuwa ni lita milioni 520.

Advertisement

Katika lita hizo, alisema vyanzo vikubwa ni Mto Ruvu Juu ambao kwa siku huzalisha lita milioni 196 na Ruvu Chini lita milioni 270. Hata hivyo, alisema Ruvu Chini wanapata lita milioni 20 tu kwa siku.

“Kabla ya tamko la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutaka ufanyike msako, uzalishaji ulifika lita milioni 68 sawa na asilimia 25.

“Kwa sasa tunazalisha lita milioni 200 sawa na asilimia 74, hivyo kuwa na upungufu wa asilimia 26,” alieleza Makalla.

Chanzo kikuu cha maji katika mto huo alisema ni mvua ambazo zilikuwa zinategemewa kunyesha Oktoba na Novemba, lakini hazijaonekana hivyo kutoa funzo kwa wananchi kuwa wanapaswa kutunza vyanzo vya maji na kuyatumia yaliyopo kwa uangalifu.

“Leo tumeona, kuna upungufu wa maji hadi mashine zinatumika kuyavuta, hivyo itabadilika tu pale mvua zitakapoanza kunyesha. Sala ni muhimu, viongozi wetu wa dini waendelee kuomba kwani tulipofika mambo yapo nje ya uwezo wa kibinadamu.

“Tuombe hali ibadilike kuanzia Novemba hii, Desemba mpaka Januari. Viongozi wa Dar es Salaam tunaotumia maji haya tumejionea ukweli twendeni tukawaelimisha watu,” alisema Makalla mbele ya wakuu wa wilaya alioongozana nao pamoja na waandishi wa habari.

Makalla alisema wameamua kutembelea vyanzo hivyo kujionea hali halisi kwa kile alichoeleza “kuona ni kuamini.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja alisema wamefurahi kupata ugeni huo kwani wanaona Serikali ipo na wao katika kipindi hiki kigumu kukidhi mahitaji ya wananchi.

Luhemeja alitumia nafasi hiyo kuahidi kwamba watajitahidi kadri wawezavyo kupambana na upungufu uliopo ili kupeleka huduma hiyo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyonge alisema kutokana na upungufu huo wa maji ni muda sasa wa kufufua visima vilivyokuwa vikitumika kabla ya kutandazwa kwa mabomba ya maji na Meya wa Ubungo, Jafari Juma alisema Serikali ina kila sababu ya kupongezwa kwa kufanya msako wa waliokuwa wanachepusha maji kwa kuwa hali hii ingeachwa, mambo yangezidi kuwa mabaya.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng`wilabuzu Ludigija alisema watu wawe wepesi kutoa taarifa pale wanapoona kuna mahali mabomba yanavuja kuepuka upotevu wa maji katika kipindi hiki ambacho mgawo wa maji bado unaendelea ili yaliyopo yatumike badala ya kupotea.

Advertisement