Makamba aitilia ngumu kampuni kusambaza umeme vijijini

Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufundi katika Kampuni ya ETDCo, Mohamed Abdallah akifuatilia jambo wakati wa hafla hiyo ya utiaji saini.

Muktasari:

  • ETDCo ilitakiwa kuwa miongoni mwa kampuni tano za kusaini mikataba hiyo na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), lakini imedaiwa kushindwa kutekeleza moja ya miradi iliyopewa mkoani Mbeya.

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati, January Makamba amezuia Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCo) kusaini mkataba wa usambazaji umeme akitoa madai ya kuwepo kwa uzembe.

Makamba amezuia mkataba huo leo Desemba 19, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme katika maeneo yaliyopo pembezoni mwa miji (Awamu ya tatu).

ETDCo ilitakiwa kuwa miongoni mwa kampuni tano za kusaini mikataba hiyo na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ikitakiwa kusaini mkataba wa kusafirisha umeme wa msongo wa 33KV katika mtandao wa kilometa 102. 5 za msongo mdogo wa matumizi ya umeme wa kawaida kwa Mikoa ya Kigoma na Geita.

“Mfano ETDCo wa Mbeya, kazi ya Mbeya umefikia asilimia 28 na ulitakiwa kuwa asilimia 88, halafu leo unataka kusaini mkataba upeleke mikoa miwili, hautasaini, na iwe fundisho kwa wengine,” amesema Makamba wakati akikemea wakandarasi wanaotaka kazi mpya huku wakiwa na kasi ndogo.

Makamba amesema haiwezekani mkandarasi huyo kupokea mradi mwingine wa Sh18 bilioni unalenga kuwafikia wananchi 6,725 katika mikoa hiyo ya Kigoma na Geita wakati kashindwa mkoa mmoja.

Makamba ametengua mkataba huo mbele ya wakandarasi na watendaji wengine wa REA huku akitoa angalizo la kutotoa kazi kwa mkandarasi yeyote kwa kigezo cha uzawa endapo hatazingatia muda wa mkataba.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufundi wa ETDCo, Mohamed Abdallah ameiomba Serikali itazame upya uamuzi huo kutokana na changamoto alizokutana nazo.

“Kweli mradi wa Mbeya ulikuwa wa miezi 18, tulitakiwa kumaliza mwezi huu, changamoto ilikuwa upatikanaji wa vifaa. Viwanda vya China vilifungwa kutokana na ugonjwa wa Uviko-19.

 “Baada ya kufungua, tayari tumeonyesha kasi ya kufunga transfoma 33 kati ya 114 zinazohitajika, tunaomba Serikali iendelee kutuamini.”