Makamba aomba Shinyanga kuwa kanda maalumu kwa unyanyasaji wa watoto

Mbunge wa Viti Maalumu Salome Makamba leo Jumatano April 12,2023 wakati akichangia kwenye Hotuba ya Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka 2023/24. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba ameomba Serikali kuufanya mkoa wa Shinyanga kuwa Kanda maalumu ya kushughulikia masuala ya unyanyasaji kwani hali ni mbaya.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba ameomba Serikali kuufanya mkoa wa Shinyanga kuwa Kanda maalumu ya kushughulikia masuala ya unyanyasaji wa watoto kwani hali ni mbaya.

Makamba ameliambia bunge leo Jumatano April 12,2023 wakati akichangia kwenye Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka 2023/24.

Mbunge huyo amesema kuwa matatizo yaliyoko Shinyanga hayatajwi kwa uzito uliopo lakini hali ni mbaya kwa pande zote ikiwemo watoto, wanawake na wanaume.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, taarifa mbalimbali zinataja kuwa Shinyanga ndiyo inaongoza kwa idadi kubwa ya mimba za utotoni lakini vipigo na manyanyaso yameripotiwa kwa wingi katika mkoa huo.

Amesema taarifa pekee ya mwaka jana (2022) iliripoti zaidi ya matukio 42,000 na kati ya hayo, matukio 5000 yalikuwa ni ya wanaume kunyanyaswa na wake zao au familia zao.

“Naomba Serikali iutazame kwa jicho pevu Mkoa wa Shinyanga, lazima tuanzishe kanda maalumu ya kushughulikia masuala haya wala tusibebee mambo kama utani utani tu mbele tutapata wakati mgumu,” amesema Makamba.

Mbunge huyo amesema maadili yameporomoka nchini Tanzania kwa kiasi kikubwa hata inahitaji kushikamana kwa pamoja kila mtu kutumia nafasi yake ili kusaidia kizazi cha sasa na kijacho.

Hata hivyo amesema inashangaza mara nyingi ukimya wa Serikali inaposhindwa kuutaja mkoa huo kwenye matatizo makubwa kama hayo kwani hayako kwa kificho.

Makamba amesema kinachotakiwa zaidi ni elimu kwa wananchi kwani elimu ikifika kwa watu wengine itasaidia kupunguza matatizo hayo kwa kiasi kikubwa ndani ya mkoa na Taifa.

Wakati huo huo, Mbunge huyo amegusia suala la uuzaji wa kiwanda cha saruji cha Tanga ambacho kinataka kununuliwa na kiwanda cha saruji kwa Twiga kwamba jambo hilo litakuwa ni hatari.