Makampuni yajiondoa Youtube kwa kuachia video ya udhalilishaji watoto

Muktasari:
Makampuni mengi Ulaya yameondoa matangazo yake kwa kuwa wameshindwa kuiondoa video ya udhalilishaji
Mtandao wa Youtube umeingia katika misukosuko baada ya kuruhusu video ya udhalilishaji watoto na maoni yaliyoamsha hasira kwa watazamaji na watangazaji.
Makampuni makubwa ambayo hutangaza katika mtandao huo ya Lidl, Mars, HP, Deutsche Bank, Sky na BT yameondoa matangazo yake, Jarida la Financial Times linaeleza.
Uongozi wa Lidl ambayo ni Kampuni inayomiliki Supermarkets kubwa nchini Ujerumani umesema umelazimika kuondoa matangazo yake kwa kuwa kitendo hicho hakivumiliki.
Kampuni inayotengeneza viburudisho ya Mars imesema imejitoa kwa kuwa kuwa matangazo yake yalionekana katika video hiyo ya kufadhaisha.
Benki ya Deutsche imesitisha kampeni yake ya kuweka matangazo yake katika mtandao huo pamoja na Google huku Kampuni ya mawasiliano ya BT na Talktalk zikiondoa matangazo yake katika video zilizokuwa chini ya udhamini wao.
Msusuru wa video za udhalilishaji watoto pamoja na maoni uliibuliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na gazeti la The Newyork Times.