Makamu wa Rais atilia shaka ujenzi jengo la halmashauri Sikonge

Muktasari:

Jengo la halmashauri ya wilaya ya Sikonge lawekewa jiwe la msingi na Makamu wa Rais,Samia Suluhu Hassan leo mjini Sikonge ingawa asema hajaridhishwa na ujenzi huo.

Tabora. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameonyesha kutofurahishwa na ujenzi wa jengo la ghorofa la halmashauri ya wilaya ya Sikonge kutokana na kutoendana na gharama halisi na kuwepo eneo ambalo halikupaswa kujengwa.

Akizungumza leo Jumamosi Februari 23, 2019 kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye jengo hilo amesema kiasi cha pesa kinachotumika ni kikubwa ukilinganisha na mahitaji na eneo lilipojengwa.

Amesema jengo hilo halikupaswa kujengwa kwa gharama kubwa na badala yake lilipaswa kujengwa jengo lenye gharama hata ya Sh2 bilioni ambalo lingeweza kuwa na ofisi zote muhimu.

Makamu wa Rais,alimuuliza mhandisi wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura),wilaya ya Sikonge, Filbert Mpalasinge, kama mhandisi mshauri anatoka wapi na kujibiwa Dar es salaam ambapo alisema ndio maana zinatumika pesa nyingi.

Awali akitoa maelezo ya jengo hilo,mhandisi wa Tarura,wilaya ya Sikonge, Filbert Mpalasinge, alisema jengo hilo litakalokuwa na ghorofa nne litakapokamilika, linatarajia kutumia zaidi ya Sh5 bilioni na hadi sasa zimetumika Sh2.4 bilioni hadi lilipofikia kwa kuwa na ghorofa mbili.

Makamu wa Rais yupo mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi ya ambapo anatembelea wilaya zote saba za mkoa huo