Makandarasi watoa maazimio saba kukabili athari za kupanda bei ya mafuta
Mwenyekiti wa Chama cha Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania (Tucasa), Samuel Marwa akizungumza katika mkutano wa dharura wa makandarasi na watoa huduma shirikishi Tanzania kujadili athari za kupanda kwa bei za mafuta katika sekta ya ujenzi.
Muktasari:
- Vyama vya makandarasi nchini vimeiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na athari za ongezeko la bei ya mafuta, ikiwamo kuruhusu madai maalumu kwa mikataba ya bei zisizobadilika, kuharakisha malipo na kufanya maboresho ya mikataba ya umma.
Dar es Salaam. Vyama vya Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania (Tucasa) vimetoa maazimio saba ya dharura vikiiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na athari za ongezeko la bei ya mafuta duniani.
Tucasa imesema kupanda kwa bei ya mafuta kumeendelea kuongeza gharama za utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini na kuwaweka wakandarasi wengi katika hatari ya kupata hasara, hali inayotishia kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uwekezaji.
Maazimio hayo yametolewa Juni 12, 2026 katika mkutano wa dharura wa makandarasi na wadau wa sekta ya ujenzi uliofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo washiriki walijadili athari za kupanda kwa bei ya mafuta kunakochochewa na mivutano ya kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati.
Akiwasilisha maazimio hayo, Mwenyekiti wa Tucasa, Samuel Marwa amesema hatua ya kwanza ni Serikali kutambua ongezeko la sasa la bei ya mafuta kama mshituko wa kipekee wa kiuchumi unaoathiri utekelezaji wa mikataba ya umma na miradi ya maendeleo nchini.
Marwa amesema chama hicho kinapendekeza kutolewa kwa mwongozo wa sera utakaoziwezesha taasisi zote za umma kushughulikia athari za ongezeko hilo, kwa mtazamo unaofanana na unaolinda masilahi ya taifa pamoja na wadau wa sekta ya ujenzi.
“Tunaomba Serikali iruhusu kwa muda wakandarasi walioingia mikataba ya bei zisizobadilika kuwasilisha madai maalumu yanayoweza kuthibitishwa kuwa yamesababishwa na ongezeko hili la kipekee la gharama za mafuta,” amesema Marwa.
Kwa mujibu wa maazimio hayo, Tucasa pia imependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa majadiliano utakaowakutanisha Serikali, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), wakandarasi, washauri elekezi, taasisi za fedha na wadau wengine muhimu ili kupata suluhisho la pamoja la changamoto hiyo.
Makandarasi hao pia wameiomba Serikali kuchukua hatua za kifedha na kiutawala zitakazolinda utekelezaji wa miradi ya kimkakati pamoja na kuzielekeza taasisi za umma kuharakisha uhakiki na malipo ya madai halali ya wakandarasi ili kuboresha mtiririko wa fedha katika utekelezaji wa miradi.
Katika mapendekezo ya muda wa kati na muda mrefu, Tucasa imeitaka PPRA kufanya mapitio ya mikataba sanifu ya umma, ili kujumuisha vifungu vinavyoweza kushughulikia mishtuko mikubwa ya kiuchumi inayojitokeza duniani.
Aidha, chama hicho kimependekeza kuandaliwa kwa mwongozo wa kisheria na kiutawala utakaobainisha namna ya kushughulikia athari za mishtuko ya kiuchumi katika mikataba ya umma, pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa kurekebisha bei pale gharama za bidhaa muhimu zitakapopanda kwa kiwango kikubwa kilichokubaliwa.
“Tunahitaji mfumo wa manunuzi ya umma wenye uwezo wa kustahimili mishtuko ya kiuchumi inayojitokeza mara kwa mara duniani ili kulinda miradi ya maendeleo na maslahi ya taifa kwa ujumla,” amesema Marwa.
Awali, Marwa ameeleza kuwa changamoto kubwa zaidi inawakumba wakandarasi wenye mikataba ya bei ya kudumu, kwani mikataba hiyo haiwaruhusu kurekebisha gharama hata pale kunapotokea mabadiliko makubwa ya bei za bidhaa muhimu kama mafuta.
Akichanagia Mwenyekiti Mstaafu wa Tucasa, Richard Mlay amesema kupanda kwa bei ya mafuta kumeongeza mzigo mkubwa kwa wakandarasi wengi, huku baadhi yao wakishindwa kuendelea kutekeleza miradi kwa gharama walizokubaliana wakati wa kusaini mikataba.
Amesema ongezeko hilo limeathiri moja kwa moja gharama za usafirishaji wa vifaa, uendeshaji wa mitambo na shughuli nyingine za ujenzi, hali iliyovuruga mipango ya kifedha ya wakandarasi wengi.
“Tunapaswa kutafuta suluhisho la muda mfupi na la muda mrefu kwa sababu wakandarasi wengi wanaendelea kutekeleza miradi katika mazingira ambayo gharama zimebadilika kwa kiwango kikubwa tofauti na walivyotarajia waliposaini mikataba,” amesema Mlay.
Meneja Masoko wa Kiwanda cha Haz, Hafifa Bahfif amesema athari za kupanda kwa bei ya mafuta zimeonekana pia katika sekta ya uzalishaji wa vifaa vya ujenzi.
Amesema kabla ya kupanda kwa bei ya mafuta, kilo moja ya malighafi ya kutengeneza mabomba ya plastiki ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh3,200 na Sh3,400, lakini kwa sasa imefikia takribani Sh5,600 kwa kilo kwa ubora uleule wa malighafi.
Kwa mujibu wa Bahfif, hali hiyo imeongeza gharama za uzalishaji na kusababisha bei za mabomba kupanda, jambo ambalo limewaathiri zaidi wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maji na miundombinu mingine waliokuwa tayari wameandaa bajeti zao kwa kuzingatia bei za awali.
“Mkandarasi aliyekuwa amepanga kutumia Sh120 milioni kununua mabomba kwa ajili ya mradi wake sasa analazimika kutumia hadi Sh150 milioni au zaidi kupata mabomba yale yale. Hii inaonyesha namna ambavyo ongezeko la bei ya mafuta na malighafi linavyoathiri mnyororo mzima wa biashara,” amesema.
Naye Mhandisi wa Kampuni ya MERITECH, Ester Christopher, amesema lengo la wakandarasi na wataalamu wa sekta hiyo si kulalamika, bali kuwasilisha mapendekezo yatakayosaidia kupata suluhisho endelevu la changamoto zinazoathiri utekelezaji wa miradi nchini.
Amesema wadau hao wamekuwa wakiwasilisha maoni yao kwa mamlaka husika na wanatarajia kupata mrejesho kuhusu hatua zinazochukuliwa ili kuboresha mazingira ya utekelezaji wa miradi na kupunguza athari za mabadiliko ya kiuchumi.
“Tunahitaji kufahamu hatua zinazofikiwa ili nasi tuweze kwenda sambamba na hali halisi ya utekelezaji wa miradi na kuendelea kutoa mchango wetu katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini,” amesema Ester.