Makarani sense wadaiwa kuwa na kasi ndogo

Muktasari:

Ikiwa leo ni siku ya pili ya sensa ya watu na makazi, malalamiko dhidi ya kasi ya makarani yaanza kujitokeza Temeke.

Dar es Salaam. Wakati sensa ya watu na makazi ikiingia katika siku ya pili leo, malalamiko yameendelea kutolewa dhidi ya makarani kwa kile kinachodaiwa wanatumia muda mrefu katika kaya moja.

Leo Agosti 24 Mwananchi limepita katika baadhi ya mitaa wilayani Temeke na kukutana na malalamiko ya wananchi kutohesabiwa licha ya kuwepo taarifa za makarani kuwepo kwenye mitaa yao.

Akizungumzia hilo Rehema Ndazi mkazi wa Chang’ombe amesema huenda kazi hiyo ya kuhesabu watu ikachukua muda mrefu zaidi kutokana na kasi waliyonayo makarani.

“Jana kutwa nzima tumekaa nyumbani hatujaona karani, leo asubuhi wakati naenda sokoni nimewaona kule stendi hadi sasa hivi hawajafika inaonekana uhesabuji unafanyika taratibu mno.

 “Sasa kwa kasi hii sidhani kama hata hizo siku saba zitatosha, sielewi shida nini maana tunasikia inatumika teknolojia kama ni hivyo inakuwaje mambo yanafanyika taratibu hivi,” amesema Subira.

Hilo limeelezwa pia na Ernest Masanja mkazi wa Temeke mwisho aliyeeleza kuwa haridhishwi na kasi ya kazi hiyo ambayo inasubiriwa na watu wengi.

“Mimi sijahesabiwa hadi sasa, kuna muda nilienda kwenye duka kutuma pesa nikawakuta pale wameingia kwenye hiyo nyumba kwa nusu saa na walivyotoka wakaingia mgahawani.

“Nikabaki najiuliza hivi hawa wanajua kwamba wanasubiriwa, wao wamekaa mgahawani wakati watu wanashauku ya kuhesabiwa, nahisi kuna kitu hakiko sawa, wengi nasikia hawajafikiwa,” amesema Masanja.