Makinda awashukia  wanasiasa kutoa ahadi bila ya utafiti

Muktasari:

Spika mstaafu na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda amewataka wanasiasa kufanya utafiti kabla ya kutoa ahadi kwa wananchi.

Mbeya. Spika wa Bunge mstaafu na Kamisaa wa Sensa ya watu na Makazi 2020, Anne Makinda amesema kitendo wanasiasa kutoa ahadi kwa wananchi bila kufanya utafiti wa eneo husika hususan miradi ya maji, ni kujinyonga wenyewe.

Makinda ameyasema hayo leo Jumatatu Januari 29, 2024 kwenye mafunzo ya waandishi wa habari mikoa ya Mbeya, Songwe na Iringa yaliyofanyikia jijini hapa yakilenga kuwajengea uwezo wa usambazaji wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).Makinda amesema kuwa nchi zinapotaka kutekeleza mipango ya maendeleo, ni lazima zifanye utafiti ikiwemo takwimu za sensa ya watu na makazi ili kuweza kuandaa mpango utakaoleta matokeo.

“Huwezi kutoa ahadi ya tatizo la maji bila kufanya utafiti, sasa hao wanaotoa ahadi wanajinyonga wenyewe wanapaswa kwanza kufanya utafiti ili kufanikisha kutekeleza malengo ya mipango mikakati,” amesema.

Amesema awali Tanzania ilikuwa nyuma katika matumizi ya takwimu, lakini sasa matumizi hayo yameleta tija kubwa katika kuboresha kiuchumi.

“Ndio maana Rais Samia Suhuhu Hassan anasisitiza suala la takwimu lengo ni kuona zinaleta tija kubwa mustakabali wa Taifa katika kuboresha huduma za kijamii,” amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Benno Malisa ameitaka NBS kushirikisha na viongozi wa dini na mila katika elimu ya sensa ili kuisaidia Serikali kutekeleza mipango ya maendeleo.

“NBS angalieni namna bora ya kuwafikia viongozi wa mila na dini kuwapatia elimu ya manufaa ya sensa ya watu na makazi ili kuweza kulifikia kundi kubwa ambalo linawazunguka sambamba na kujua uwekezaji uliofanywa na Serikali,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja Takwimu Mkoa wa Mbeya, John Lyakurwa amesema lengo la kuwakutanisha wanahabari, ni kuwajengea uwezo  wa matumizi ya takwimu za sensa ya watu na makazi na kwamba waandishi zaidi ya 420 kutoka vyama vya waandishi wa habari wamenufaika.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya (MBPC), Nerbalt Msokwa amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo na uwazi wa kuandika habari za tafiti za takwimu katika kutekeleza uwajibikaji kwa kuhabarisha umma wa Watanzania.