Makonda afafanua agizo la chama kwa Waziri Mkuu

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari, akizungumza katika Uzinduzi wa Kitabu cha Kuanzisha na Kuratibu Klabu za Kidijiti, katika ukumbi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Novemba 2, 2023.

Muktasari:

  • Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda akutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jijini Dodoma na kufanya naye mazungumzo, asema maagizo waliompa jana ameyapokea na kuanza kuyafanyia kazi.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda kutoa maagizo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo ametinga ofisini kwa mtendaji mkuu wa Serikali, akisema chama hicho kina imani naye.

Jana Jumatano Novemba Mosi, 2023 akiwa jijini Dodoma, Makonda alimpa miezi sita Majaliwa kushughulikia changamoto ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara.

“Chama (CCM) kinamtaka Waziri Mkuu (Majaliwa) anayesimamia na kuratibu kuondoa na kufuta migogoro ya ardhi inayosababisha wavuvi, wakulima na wafugaji na wananchi kuteseka kutokana na ardhi yao,” amesema Makonda jana.

Hata hivyo leo Alhamisi Novemba 2, 2023 Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa taarifa kwa umma, ikieleza kuwa CCM imesema haina mashaka na utendaji kazi wa Majaliwa, ikisisitiza ni kiongozi mtiifu na mchapakazi.

“Chama tuna matumaini makubwa na uwajibikaji na uaminifu wa Waziri Mkuu (Majaliwa), tumemuona katika maeneo mengi akisimamia shughuli mbalimbali za Serikali.

“Nilipotoa agizo la chama kwa Waziri Mkuu nilitaka lifike kwa mtu anayeweza kuleta matokeo chanya kwa chama,” amesema Makonda katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Makonda amesema lengo la CCM chini ya Mwenyekiti Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Serikali inatimiza kile ambacho imepewa kukifanya kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi, akisema wana matumaini makubwa na utendaji kazi Majaliwa.

Makonda ambaye kabla ya kuonana na Majaliwa alianzia bungeni kwa mwaliko maalumu na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, amesema CCM ni kuhakikisha ndoto ya Rais Samia ya kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi inafikiwa.

“Waziri Mkuu ni mtendaji mtiifu, mwaminifu maelezo yaliyotolewa kwake na CCM kuhusu migogoro ya ardhi tayari ameyapokea na ameanza kuyatekeleza.

“Nina imani hata miezi sita tuliyompa inawezekana akatumia hata miezi mitatu tukapata ripoti. Pia tumemwagiza Waziri Mkuu, kuwachukulia hatua wote watakaonekana kukwamisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya Serikali,” amesema Makonda.

Majaliwa amesema Serikali imepokea maelekezo ya CCM na itaendelea kuyafanyia kazi ili kuhakikisha migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini inaendelea kushughulikiwa.

Kuhusu udhibiti wa fedha za umma, Majaliwa amesema Serikali itaendelea kulisimamia jukumu hilo ili fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi maendeleo zitumike ipasavyo na katika viwango vya ubora vinavyotarajiwa.