Makonda amtaka mkandarasi kujisalimisha polisi

Muktasari:

Leo mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekagua miradi ya maendeleo wilayani Kinondoni na ameagiza mkandarasi ajisalimishe Polisi

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemtaka mkandarasi wa kampuni ya ujenzi iliyotengeneza barabara ya Biafra kujsalimisha polisi kabla ya Ijumaa Aprili 19,2019.

Mkandarasi huyo wa kampuni ya Skol Construction Ltd anadaiwa kutengeza barabara hiyo chini ya kiwango.

Makonda ametoa agizo hilo leo Jumatatu Aprili 15, 2019 wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani Kinondoni.

Amri hiyo imekuja baada ya  kampuni hiyo kukiuka agizo la kurudia ujenzi wa barabara hiyo kwa gharama zake kutokana na kujenga chini ya kiwango, jambo linaloleta usumbufu kwa watumiaji.

Katika hatua nyingine, Makonda amemtaka Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo kutowachekea watu wanaoonekana kuwa na ubabaishaji kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akiwa katika miradi ya Barabara ya Kituo cha Mabasi cha Simu 2000 Makonda ameshangazwa na gharama kubwa inayotumika kujenga barabara za Mradi wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (DMDP) tofauti na zile za Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa barabara za mijini na vijijini (Tarura) ambazo zinajengwa kwa kiwango sawa lakini kiasi cha fedha ni kidogo.

Amesema makandarasi wa DMDP wamekuwa wakijiamulia kupandisha gharama za ujenzi kutoka Sh8 bilioni hadi Sh13 bilioni jambo ambalo ametaka kuangaliwa kwa jicho la tatu.

Akijibu kuhusu hilo, Chongolo amesema uongozi wa halmashauri utalifanyia kazi kwa kukaa na makandarasi hao wa DMDP kujua undani wa gharama hizo.