Makonda ataka wadau wa utalii kuchangamkia fursa ya maonyesho

Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilifair Promotion, Dominic Shoo akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 5, 2024 jijini Arusha. Picha na Janeth Mushi
Muktasari:
- Maonyesho hayo ya Kimataifa ya utalii ya Karibu Kilifair yatafanyika katika viwanja vya Magereza, jijini Arusha kuanzia Juni 7 hadi 9, mwaka huu, yanategemea kuvutia washiriki kutoka nchi mbalimbali na wanunuzi kutoka masoko ya kimataifa
Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amewataka wadau wa utalii mkoani humo kutumia maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu Kilifair, kujifunza mbinu za uwekezaji kutoka kwa watoa huduma na wanunuzi wa utalii ili kuongeza idadi ya watalii kupitia vivitio vilivyomo nchini.
Makonda ametoa rai hiyo leo Jumatano Juni 5, 2024, baada ya kutembelea na kukagua maandalizi ya maonesho hayo katika viwanja vya Magereza (Kisongo), yanayotarajiwa kuanza Juni 7 hadi 9, mwaka huu.
Amesema kuwa maonesho hayo ni fursa ya pekee kwa wadau mbalimbali wa utalii kujifunza mbinu mbalimbali kutoka kwa wanunuzi na waonyeshaji ambao watashiriki siku hizo tatu.
“Tukio kama hili linakutanisha wote wanaofanya biashara ya utalii katika mkoa wetu watumie maonesho haya kikamilifu. Ni fursa adimu waje kukutana na wenzao wanaofanya biashara ya utalii duniani ambao wanaletwa na maonesho haya,’’ amesema.
“Ili waone namna gani wanaweza wakaboresha na kuongeza utoaji wa huduma tuendelee kupata wageni wengi zaidi ambao watatuongezea kipato kama mkoa na Taifa, nawapongeza wote kwa kazi nzuri wanayofanya katika kukuza sekta hii muhimu ya utalii,” ameongeza Makonda.
Akizungumzia maandalizi ya maonesho hayo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilifair Promotion, Dominic Shoo amesema hadi leo maandalizi hayo yamefikia asilimia 90.
Amesema maonesho hayo yanayokutanisha wanunuzi wa utalii zaidi ya 600 kutoka nchi 40 duniani na waonyeshaji 468 kutoka nchi 37 duniani, yanachangia kuongeza idadi ya watalii nchini.
“Haya maonesho ya Karibu Kilifair tunaweza tusiweze kuyapima lakini kwa kiwango kikubwa tuna imani kwamba kama tulikuwa na watalii milioni moja na sasa hivi tuna watalii zaidi ya milioni mbili sisi ni wachangiaji wakubwa wa ongezeko hilo,” ameongeza.
Amesema maonesho hayo ambayo yatafanyika kwa mara ya tatu baada ya kusitishwa kwa miaka miwili kutokana na janga la Uviko- 19, yamevutia washiriki kutoka Afrika Mashariki na wanunuzi kutoka masoko ya kimataifa.
Amesema maonesho hayo yamelenga kujenga na kukuza biashara ya utalii kimataifa na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.