Makonda kuwachongea watendaji wazembe kwa Rais Samia

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda (aliyekaa kwenye kiti) akiwa na viongozi chama hicho na Serikali Mkoa wa Shinyanga baada ya kupokewa jana katika mwendelezo wa ziara yake ya mikoa 20. Picha na CCM

Muktasari:

  • Makonda amesema atawasilisha kwa Rais Samia Suhuku Hassan orodha ya watendaji wazembe kwa ajili ya hatua kuchukuliwa, huku wale wanaotekeleza majukumu yao kwa ufanisi watatambuliwa.

Shinyanga. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema atawasilisha orodha ya watendaji wazembe na wasiootekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema akihitimisha ziara ya awamu ya kwanza sehemu ya pili ya mikoa 20, Makonda amesema vilevile atawasilisha ripoti kwa Rais Samia ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, ya watendaji wanaotekeleza wajibu wao vizuri ili nao wapongezwe.

Makonda ametoa ahadi hiyo leo Januari 28 alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Sabasaba mkoani Shinyanga.


Amefafanua kuwa orodha ya watendaji wazembe ataiwasilisha kwa ajili ya hatua kuchukuliwa, huku wale wanaotekeleza majukumu yao kwa ufanisi watatambuliwa.


Mwanasiasa hiyo amesema yeye si mtu wa kuwavumilia watumishi wasiotimiza wajibu wao.


Amesema Shinyanga ikiwa ni mkoa wa nane katika ziara yake baada ya Tabora, Pwani, Singida, Manyara, Arusha, Tanga na Kilimanjaro, ambako kote huko watendaji wazuri wamebainika na kupongezwa na wale wanaoharibu wamejulikana.


"Baada ya ziara hii nitakabidhi ripoti na hatua mtaziona, nimekula kiapo nitawapigania wanyonge wa Taifa hili, niwaambie watumishi wote wa Serikali ngazi zote, ukiboronga au kuharibu Makonda hatakutetea, utabeba mzigo wako mwenyewe,” amesema.


Makonda amesema, "kama mtumishi ameboronga au hawathamini wananchi kama waajiri wake, CCM ya Samia ambayo msemaji wake ni Makonda, haogopi uchawi au ushirikiana wala kujipendekeza kupata cheo, bali atafanya kwa mujibu wa sheria."


Katika hatua nyingine, uongozi wa CCM Wilaya ya Shinyanga umemkabidhi Makonda Sh2 milioni kama mchango wao wa fomu kwa ajili ya Rais Samia kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa tena kuwania urais kupitia chama hicho tawala katika uchaguzi mkuu wa mwakani.


Mbunge wa Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi amekabidhi fedha hizo kwa Makonda, akisema chama hicho mkoani humo kipo bega kwa bega na Rais Samia katika harakati hizo.
Uongozi wa CCM Kilimanjaro na Arusha ni miongoni mwa mikoa iliyochanga fedha za fomu ya Rais Samia.


Awali, Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), amesema ndani ya miaka mitatu jimbo la Shinyanga Mjini limetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya uboreshaji wa sekta za afya, elimu na miundombinu ya barabara.


"Tumeboresha sekta ya maji na umeme, miradi inaendelea katika maeneo mbalimbali ya jimbo hili, ingawa kuna sehemu bado maji hayafika, lakini mchakato unaendelea," amesema Katambi.


Akiwa wilayani Kahama, Makonda amesema watumishi wa sekta ya afya, wakiwamo wauguzi na madaktari watakaobainika kusababisha vifo kwa wagonjwa kwa sababu ya uzembe wa kuchelewa kutoa huduma, watachukuliwa hatua zaidi badala ya kuhamishwa vituo vya kazi.


Makonda ameeleza hayo baada ya kupokea kero kutoka kwa kinamama waliodai kunyanyaswa na watumishi wa sekta ya afya wilayani humo, wakimwomba Makonda kuwasaidia kutatua changamoto hiyo.


Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita amesema Serikali wilayani humo imewasimamisha kazi baadhi ya wauguzi na madaktari katika hospitali ya wilaya kwa uzembe na kumuondoa mganga mkuu wa wilaya.