Makonda: Sio lazima niteuliwe, ninaweza kuwa kiongozi wa familia

Muktasari:

  • Aliyekuwa mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kwa sasa sio lazima ateuliwe au apigiwe kura kuwa kiongozi,  anaweza kuongoza hata familia yake.

Dar es Salaam. Aliyekuwa mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kwa sasa sio lazima ateuliwe au apigiwe kura kuwa kiongozi,  anaweza kuongoza hata familia yake.

Ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 20, 2021 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mahafali ya kuhitimu stashahada ya uzamili ya uongozi katika Chuo Kikuu cha Aalto cha Finland kikishirikiana na Taasisi ya Uongozi Tanzania.

“Mimi ni mkulima, ni mfanyabiashara pia kwa hiyo ninaweza kuwa na mchango mkubwa sana hata kwenye kampuni ninazoweza kufanya kazi. Siyo lazima uwe kiongozi wa kuteuliwa au wa kupigiwa kura, unaweza kuwa kiongozi hata wa familia,” amesema.

Makonda aliyeteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mwaka 2016,  mwaka 2020 alijitosa kwenye kura za maoni CCM kuwania kuteuliwa kugombea ubunge wa Kigamboni kwa tiketi ya chama hicho tawala bila mafanikio baada ya kushika nafasi ya pili nyuma ya mbunge wa jimbo hilo, Dk Faustine Ndugulile.

Huku akitaja masomo ya intelijensia ya hisia  na intelijensia ya kiroho, Makonda amesema katika kozi hiyo amejifunza uongozi ikiwa pamoja na kujali maisha ya watu.

Makonda: Sio lazima niteuliwe, ninaweza kuwa kiongozi wa familia

“Haya masomo mawili yanaonekana yanafanana lakini namna ya kuya connect (kuunganisha) ni lazima pia ujue pia maisha ya watu unaowaongoza na hali wanazotoka, unaweza kumfokea mtu kumbe nyumbani kwake hajala, unaweza kumtukana mtu.”

“Ukitaka kuwa kiongozi mzuri, lazima uwe tayari kujifunza. Mazingira yanabadilika kila wakati, siasa inabadilika, uchumi unabadilika, hivyo ili uwe kiongozi mzuri unapaswa kujifunza kila nyakati,” amesema Makonda.