Makosa manane ya bodaboda yanayogharimu maisha ya watu

Muktasari:

  • Watu 8,200 wamepoteza maisha ndani ya miaka 10 nchi nzima

Moshi. Ujio wa pikipiki maarufu kama bodaboda unatajwa kuleta neema ya ajira kwa vijana na kurahisisha usafiri, lakini unadaiwa kuleta janga la ajali na kusababisha vifo na vilema vya kudumu.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini wengi wa waendesha pikipiki hizo wamekubuhu katika kufanya makosa manane wawapo barabarani na kusababisha ajali zinazowapukutisha wao na abiria wanaowapakia.

Ni kutokana na wingi wa ajali zinazohusisha bodaboda, Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro na hospitali zinazoizunguka zimekuwa zikipokea majeruhi wa ajali wanaofikia zaidi ya 30 kila wiki.

Ofisa uhusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo anasema ajali za pikipiki ni janga na wao katika wodi ya upasuaji wa mifupa wamekuwa wakipokea majeruhi wa ajali za bodaboda kati ya 14 na 15 kwa wiki.

“Lakini ukienda kule wodi ya general surgery (upasuaji wa jumla) unakuta tunapokea majeruhi wa pikipiki kati ya 15 na 30 kwa wiki. Wengine majeraha ni mabaya wanapata ulemavu wa kudumu,” anasema.

Ofisa uhusiano huo anasema majeraha mabaya zaidi hutokea katika uti wa mgongo ambapo majeruhi wanaopata majeraha hayo hupata ulemavu wa kudumu na wengine inakuwa ndio mwanzo wa kuwa wategemezi.

Makosa 8 ya bodaboda nchini

Katika uchunguzi huo uliohusisha mahojiano na madereva wa bodaboda wenyewe na wa magari, imebainika kuwa madereva wa bodaboda huwasha indicator (taa ya kiashiria cha kukata kona), lakini wao huashiria eneo ambalo silo wanaloenda.

“Unakuta dereva wa bodaboda anaonyesha indicator kuwa anakata kulia barabara inayofuata mbele yake lakini hakati anaendelea tu na safari yake,” anasema Haji Sadick wa Majengo mjini Moshi.

Dereva huyo wa magari ya kusafirisha watalii, anasema inapotokea dereva wa gari akiamini kuwa bodaboda inakata kulia au kushoto, inatokea ajali lakini iliyosababishwa na uzembe wa bodaboda.

“Hili la indicator ni ugonjwa sugu kwa madereva wa bodaboda. Unakuta anawasha taa umbali hata wa kilomita tano wala haingii huko anakoonyesha. Hawa watu wanahitaji viboko.”

Kosa la pili linalotajwa kuchangia ajali nyingi kati ya magari na pikipiki hizo ni mwendokoasi wa baadhi ya madereva wa pikipiki ambao hawajali kama eneo husika linahitaji mwendo wa spidi 30 au 50.

Mfanyabiashara Bosco Simba, anasema licha ya uwepo wa vibao katikati ya mji wa Moshi vinavyowataka kwenda spidi 30, madereva hao huenda hadi spidi 100.

“Mpaka tunajiuliza hivi vibao vya alama hizi za barabarani vimewekwa kwa ajili ya magari tu au vyombo vyote vya moto? Wapewe elimu hawa watu maana wanafikiri wana haki muda wote,” anasema Simba.

Wakili Peter Mshikilwa wa jijini Dar es Salaam anataja makosa mawili wanayofanya madereva wa bodaboda kuwa ni pamoja na kujichukulia sheria mkononi inapotokea ajali hata kama wao ndio chanzo.

“Jeshi la Polisi linapaswa liendelee kutoa elimu kwa hawa waendesha pikipiki. Miongoni mwao kuna wahuni wengi kwa sababu ajali ikitokea tu wao ndio wanageuka trafiki na kutoa adhabu,”anasema.

Wakili huyo anasema chombo pekee chenye wajibu wa kushughulikia ajali ni Idara ya Usalama Barabarani, lakini badala yake kila ajali ikitokea bodaboda hupigiana simu na kujiona ni trafiki.

Mbali na kosa hilo, lakini wakili huyo anataja kosa lingine kubwa la bodaboda ni baadhi yao kutosimama kwenye alama za waenda kwa miguu (zebra crossing), jambo ambalo ni hatari.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) tawi la Kilimanjaro, David Shillatu anasema Serikali inapaswa kushughulika na madereva wa bodaboda watukutu kabla hali haijawa mbaya zaidi. “Hawajui kuwa ukimgonga mtu kwenye zebra crossing hiyo inachukuliwa kama dangerous driving (uendeshaji wa hatari) na hilo kosa ni kubwa na halina faini. Ni lazima wapewe elimu,” anasema Shillatu.

Shillatu anawataka madereva wa bodaboda wasitambe kwamba kwa vile ni rahisi kutoroka eneo la tukio kwa pikipiki bila kukamatwa, ndio ‘leseni’ ya kufanya makosa ya barabarani kwa makusudi.

Kwa mujibu wa wakili huyo, kosa la sita ambalo wengi wa waendesha bodaboda hao hulifanya ni kuendesha vyombo vya moto pasipo kuwa na leseni wakitegemea kuwapiga chenga trafiki wawapo barabarani.

Makosa mengine mawili ambayo yametajwa ni pamoja na kuyapita magari vibaya na upande usioruhusiwa hususan kwenye mzunguko wa barabara na kuingia barabara kuu bila kuchukua tahadhari.

“Unakuta upo kwenye round about (mzunguko wa magari) unashangaa bodaboda ana-overtake (kupita) ili awahi tu kupita unajiuliza hivi wana wendawazimu au wanavuta bangi?” anahoji Abdul Issa.

Issa anadai wengi wa bodaboda huyachomekea magari wanapoingia barabara kuu bila kujali kuwa pikipiki zao hazina ‘mabodi’ hivyo wakigongwa madhara yanakuwa makubwa kwao na abiria wao.

Wanachosema bodaboda

Madereva wa bodaboda waliohojiwa na gazeti hili walikiri kuwa wengi wao hufanya makosa makubwa wawapo barabarani, lakini wakadai ni kutokana na kutopata mafunzo sahihi ya udereva.

Samwel Peter anayefanya shughuli zake Soko la Samaki la Manyema mjini Moshi, anasema wengi wao hukiuka sheria za barabarani hasa mwendokasi na huyapita vibaya magari wawapo barabarani.

“Kwa kweli ku-overtake (kupita) kushoto badala ya kulia au hata ku- overtake wakati alama za barabarani zinakataza hili lipo sana au kujisahau kwenye indicator ni makosa yapo,” anasema.

Hata hivyo, anasema tatizo madereva wengi wa bodaboda wamejifunzia mitaani tena wengine kwa dakika 30 kisha huingia barabarani wala hawajui maana ya alama za barabarani wala sheria zake.

Dereva mwingine, Gadson Mdee, anasema madereva wengi wa bodaboda hufanya makosa ya wazi barabarani, lakini akasema tatizo hawana elimu ya barabarani kwa vile walijifunza ‘kienyeji’.

“Hili ni tatizo kubwa na wengi wetu tumewapoteza (wamefariki) kwa ajali hizi hizi za kizembe. Anakimbia mahali wala hapastahili. Lakini kuna madereva wa magari nao wanatuonea.”

Mdee anasema wapo bodaboda ambao huyapita magari yaliyo mbele yao na mbele wanapoona pikipiki inakuja, wala hawajali na wakati mwingine wanalazimika kuingia mtaroni ili kuepuka kugongwa.

Polisi waonya, wajipanga

Akizungumzia suala la bodaboda kuanzisha fujo kwa madereva wa magari baada ya kusababisha ajali, kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah anasema ni kinyume cha sheria.

Issah anasema jeshi hilo limejipanga vizuri kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa na halitasita kuwachukulia hatua madereva wa bodaboda ambao watabainika kuzikiuka.

“Bodaboda kuitana na kulizingira gari baada ya ajali ni kosa kisheria kwani unakuta dereva bodaboda ndiye amesababisha ajali, lakini anasababisha fujo. Hili ni tatizo na hatuwezi kulivumilia,” anasema.

“Tulianza operesheni ya kuhakikisha madereva wote wa bodaboda na abiria wao wanavaa kofia ngumu (helmet) wamelitekeleza, ingawa wengine wanavaa za ujenzi siyo zile zenyewe zinazokubalika.”

Kamanda Issah anawataka madereva wa bodaboda kuheshimu sheria za usalama barabarani vinginevyo wanahatarisha maisha yao na abiria wao na kuwataka watambue uhai haununuliwi dukani.

Pikipiki zaua watu 8,237

Novemba 2018, Serikali ililiambia Bunge kuwa katika kipindi cha miaka 10 kati ya 2008 hadi 2018, watu 8,237 wamepoteza maisha kwa ajali za pikipiki huku 38,237 wakipoteza viungo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni alitoa takwimu hizo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalumu (CCM), Fakharia Shomari.

Awali, mbunge huyo alihoji vijana wangapi wamepoteza maisha na wangapi wamepoteza viungo vyao kutokana na ajali ya pikipiki.

Akijibu, Masauni alisema ajali zilizoripotiwa zilizosababisha vifo na kupoteza viungo ziko 38,234.