Makungwi, wazee wanavyopigia debe jando, unyago Mtwara
Muktasari:
- Wadai havichochei ngono kwa wanafunzi
Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa inayoaminika kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaokatisha masomo katika shule za msingi na sekondari kutokana na sababu mbalimbali kila mwaka.
Takwimu kutoka idara ya elimu mkoani Mtwara zinaonyesha kuwa kati ya wanafunzi 43, 913, walioandikishwa kuanza darasa la kwanza mwaka 2010 ni wanafunzi 24, 586 pekee ndio walihitimu darasa la saba mwaka 2016.
Hii inamaanisha kuwa waliohitimu ni asilimia 71 ya wasichana 17, 647 na wavulana 17, 266 walioandikishwa ndio walifanya mitihani ya kuhitimu darasa la saba huku wenzao 19, 327 wakishindwa kuhitimu.
Takwimu hizo zilizowasilishwa kwenye kikao cha wadau wa elimu mkoani Mtwara zinaonyesha kuwa ni wanafunzi 6, 465 ndio waliofanya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne mwaka 2016 kulinganisha na idadi wanafunzi 12, 375 waliosajiliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2013.
INAENDELEA UK 28
Inatoka UK 27
Jumla ya wanafunzi 5, 910 hawakufanya mitihani kutokana na sababu mbalimbali.
Utoro, mimba na ndoa za utotoni, vifo na mwamko mdogo wa elimu kwa jamii ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kusababisha kuacha shule.
Kwa mfano, kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2015 hadi 2017, jumla ya wanafunzi 393 wa shue za sekondari waliacha shule kwa kupata ujauzito mkoani Mtwara.
Wadogo zao 68 wa shule za msingi pia walipata ujauzito na kuacha shule kwa kipindi hicho cha miaka miwili.
Idadi hiyo inafanya jumla ya utoro wa wanafunzi kwa shule za msingi na sekondari kwa sababu ya mimbo kuwa wanafunzi 461.
Mafunzo na kambi za jando na unyago yanayonyooshewa vidole kuwa miongoni mwa sababu za mimba za utotoni na kusababisha wanafunzi wa kike kukatisha masomo kila mwaka.
Wazee wa mila na makungwi wanaotoa mafunzo hayo ndio wanatupiwa lawama wakidaiwa kuwafundisha watoto masuala kiutu uzima kulinganisha na umri wao.
Hata hivyo, kundi hilo kutoka jamii ya Wayao, Wamakonde, Wamakua na Wamwera wanakanusha madai hayo wakisema mafunzo na kambi za jando na unyago ni misingi ya maadili mema kwa watoto wa jamii zao kutokana na kufundwa kuhusu masuala mbalimbali kimaisha.
Kauli ya wazee wa jadi na makungwi
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wazee wa mila na makungwi wenye dhamana ya mafunzo wanasema kambi za jando na unyago zinawaandaa vijana kuwa watu wema na wanaowajibika kwa jamii.
Fatuma Hassan, mmoja wa makungwi katika mafunzo na kambi iliyohudhuriwa na vijana 305 waliohitimua mafunzo ya jando na unyago wilayani Tandahima Desemba mwaka jana anasema pamoja na stadi za maisha, vijana hao pia hufundishwa maadili mema na kuonywa dhidi ya ngono katika umri mdogo.
“Watoto wa kike wanafundishwa usafi wa mwili, maadili mema na namna ya kuwa mama bora anayelea na kuhudumia vyema familia; tunawaonya dhidi ya ngono katika umri mdogo,” anasema Fatuma.
Kuhusu madai ya mafunzo na kambi hizo kuwakatisha masomo wanafunzi, kungwi mwingine, Sarah Emmanuel anasema madai hayo hayana ukweli kwa sababu mafunzo hayo ya mwezi mmoja kila mwaka hufanyika nyakati za likizo.
“Mwaka 2017 Wilaya ya Tandahimba tumeendesha mafunzo na kambi wakati wa likizo ya Desemba. Mgeni rasmi katika sherehe za kufunga alikuwa Mkuu wa Wilaya Sebastian Waryuba; tungekatisha wanafunzi masomo ni dhahiri kiongozi huyu asingeshiriki,” anasema Sarah.
Mzee wa mila anayetoa mafunzo kwa vijana wa kiume, Abdallah Namuna anataja stadi za maisha, usafi wa mwili na tohara, utunzaji wa mazingira, ukakamavu, ulinzi kwa jamii na kusaidia wazazi kuwa miongoni mwa mambo muhimu yanayofundishwa.
“Tunawafundisha masuala ya kilimo, afya na kuepuka ngono katika umri mdogo,” anasema Namuna
Sherehe za kuhitimisha mafunzo na kambi ya mwaka jana wilayani Tandahimba zilifanyika kijiji cha Namahonga ambapo Mkuu wa wilaya hiyo, Sebastian Waryuba alitumia hotuba yake kuagiza suala la umuhimu wa elimu kuwa miongoni mwa ajenda kuu wakati wa kambi za jando na unyago wilayani humo.
Madhara ya kutoshiriki jando
Hawa Mpaka, mmoja wa mangariba kutoka Kijiji cha Mchichira wilayani Tandahimba anasema: “Wasioenda jando na unyago hutengwa, kusemwa vibaya na kuchekwa mitaani wakidaiwa kuwa bado ni watoto hata kama wamefikia umri wa utu uzima.”
Anasema kundi la wasioshiriki mafunzo hayo huesabiwa kuwa watu wasio na nidhamu, wasiofundwa na wasio na stadi za maisha ikiwemo ujasiri, ukakamavu kwa vijana wa kiume na nidhamu na heshima ya kujisitiri maungo kwa wale wa kike.
“Ili kuwaondolea adha hiyo inayoweza kusababisha madhara ya kisaikolojia, vijana wanaokosa kushiriki makambi ya mwezi mmoja ya jando na unyago hufundwa angalau kwa siku kadhaa ili kuwawezesha kukubalika katika jamii,” anasema Hawa.
Lawama dhidi ya Serikali
Akizungumzia kumomonyoka kwa maadili miongoni mwa jamii wakiwemo watoto, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mchichira wilayani Tandahimba, Said Likwati anataja utitiri wa vibanda vya kuonyesha video mitaani na udhibiti mdogo wa aina ya picha zinazoonyeshwa kuwa miongoni mwa sababu zinazomomonyoa maadili nchini.
“Baadhi ya video zinazoonyeshwa kwenye vibanda umiza haziendani na maadili na umri wa watoto wanaojazana huko; Serikali lazima idhibiti jambo hili,” anasema Likwati
Sherehe za akina mama ya ‘Mpeano’ inayonogeshwa na ngoma maarufu ya kigodoro pia miongoni mwa mambo yanayotakiwa kudhibitiwa na Serikali kulinda maadili ya watoto, kwa mujibu wa Likwati.
“Sherehe za ‘Mpeano’ hushirikisha watoto ambao huangalia mambo yanayoibua fikra na hisia za mambo ya kikubwa yasiyolingana na umri wao; kuwe na amri ya kitaifa kuelekeza muda na eneo maalumu ya sherehe za aina hiyo tofauti na sasa zinapochezwa hadharani mitaani,” anashauri Likwati.
Serikali yatoa mwongozi
Akihitimsha mafunzo ya jando na unyago wilayani Tandahimba, Mkuu wa Wilaya hiyo, Sebastian Waryuba anaagiza yaongezewe ubora kwa kuhusisha suala la elimu na yafanyike mara moja kwa mwaka nyakati za likizo baada ya kuomba na kupata vibali kutoka ofisi ya utamaduni ya halmashauri.
“Tuyaboreshe mafuzo na kambi za jando na unyago kwa kuongeza uhamasishaji wa elimu kuwa sehemu ya mafunzo ili kuwapa fursa watoto wa Tandahimba kumudu ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi inayokabiliwa na mabadiliko ya Sayansi na Teknolijia,” akaagiza Waryuba.
Pia, amewaagiza wazee wa mila na makungwi kuwaelimisha vijana hao madhara ya ngono na mimba katika umri mdogo kama njia ya kukabiliana na janga la wanafunzi wa kike wilayani humo kukatisha masomo kwa kupata ujauzito wilayani humo.
Wilaya hiyo imeshuhudia wanafunzi 107 wa shule za msingi na Sekondari wakikatisha masomo kwa kupata ujauzito kati ya mwaka 2015 hadi 2017 na hivyo kufanya wilaya hiyo kuwa kinara kwa mimba za wanafunzi mkoani Mtwara.
Mbunge wa Tandahimba, Katani Katani anataja mwamko mdogo wa elimu miongoni mwa wazazi wilayani humo kuwa miongoni mwa sababu za mdondoko wa wanafunzi shuleni.
“Pamoja na kuunda timu maalumu kufanya utafiti wa namna bora na sahihi ya kushirikisha jamii katika juhudi za kuinua mwamko wa elimu wilayani Tandahimba, tumeelekeza nguvu kwenye elimu ya kujitambua kwa watoto wetu,” anasema Katani.
Mbunge huyo anashauri mkazo wa elimu ulenge watoto wa jinsia zote za kike na kiume kutokana na takwimu kuonyesha makundi yote kukatisha masomo.
Akizungumzia suala la mimba katika kikao cha wadau wa elimu Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Mkoa, Gelasius Byakanwa anatoa agizo kwa walimu na waratibu wa elimu kwa kushirikiana na maafisa elimu kuwapima mimba wanafunzi wa kike mara kwa mara.