Malaria bado pasua kichwa nchini

Dar es Salaam. Hakuna mwongozo rasmi wa kuteketeza vyandarua kwa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara kutokana na ugumu wa kuvikusanya. Hata hivyo, kuna njia zilizopendekezwa za matumizi mbadala.

Mkuu wa kitengo cha kudhibiti wadudu wanaodhuru kutoka Wizara ya Afya, Charles Dismas anasema hakuna mwongozo wa uteketezaji vyandarua kwenye nchi hizo.

Anasema kikwazo ni gharama za kuvikusanya kwa kuwa havipaswi kuchomwa.

Kwa maelezo ya mtaalamu huyo, vyandarua havichomwi kwa kuwa vimewekwa dawa, hivyo kuvichoma kunaharibu mazingira na moshi wake unaleta madhara kwa binadamu.

Shirika la Afya Duniani (WHO), limetoa njia mbadala tatu za matumizi ya vyandarua vilivyochakaa.

Dagaa zikiwa zimeanikwa juu ya chandarua

Inaelekezwa na kutolewa kipaumbele kwa watoto kuvitumia kutengeneza mipira ya kuchezea kupitia vyandarua kuukuu.

Njia nyingine ni kipande cha chandarua kisichoharibika kutumika kama wavu wa dirisha kwa maeneo ya vijijini.

Nyingine isiyopewa kipaumbele kwa sababu inaweza kuwavutia watu kutokuwa na matumizi sahihi ya vyandarua ni kuvitumia kama wigo kwenye bustani.

Dismas anasema WHO imetoa kipaumbele kwa utengenezaji mipira ya kuchezea watoto, sababu ikiwa matumizi mengine yanayotajwa yanaweza kuwa kichocheo cha kuviharibu vyandarua ili vitumike kwa mambo mbadala wa kujikinga na mbu.

Anaitaja njia nyingine isiyopewa kipaumbele ni kukiweka chini ya godoro au mkeka unaotumika kulalia.

Wizara ya Afya inaendelea kutekeleza mpango mkakati wa malaria 2021 -2025, lengo likiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo  kutoka asilimia 7.5 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025.

Lengo hilo linaendana na jitihada mbalimbali za Serikali, ikiwemo uwekezaji katika tafiti za malaria, mfano kwa mujibu wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 wizara kupitia taasisi ya tafiti, kati ya tafiti 213, asilimia 10 zilikuwa za ugonjwa huo  ukilinganisha na asilimia nane ya mwaka uliopita.

Pia katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi, 2022 Wizara ya Afya kupitia Bohari ya Dawa (MSD), ilipokea kutoka kwa wadau wa maendeleo dawa mseto ya kutibu malaria (ALu) dozi 14,977,710, vipimo 33 vya haraka vya malaria (MRDT),  jumla ya vitepe 20,991,875 na dawa ya sindano ya kutibu malaria kali vichupa 2,356,930, na kusisitiza huduma za vipimo na dawa zitatolewa bure.

Kwa mujibu wa wizara, pia vifo vya malaria kwa rika zote vimepungua kwa asilimia 67 kutoka vifo 6,311 mwaka 2015 hadi 2,079 mwaka 2019.

Kati ya vifo 2,079 vya malaria vilivyotokea mwaka 2019, vifo vya watoto wa umri chini ya miaka mitano, vilikuwa 957, sawa na asilimia 46 ya vifo vyote vilivyosababishwa na ugonjwa huo.

Watu waliopimwa na kuonekana kuwa na malaria waliongezeka katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2019 kutokana na kuwepo kwa vifaa vya utambuzi, hususan kifaa cha MRDT.


Ukubwa wa tatizo

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, mwaka 2021/2022, malaria ulikuwa ugonjwa ulioongoza miongoni mwa magonjwa 10 yaliyoongoza kwa wagonjwa wa kulazwa kwa watu wenye umri wa miaka mitano au zaidi na wa pili kwa kulaza watoto chini ya miaka mitano.

Vilevile ni ugonjwa wa pili kwa wagonjwa wasiolazwa baada ya magonjwa ya mfumo wa hewa kwa watoto na wa tatu kwa wakubwa.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2020, vifo vya malaria Tanzania vilifikia 21,758 au asilimia 7.38 ya vifo.

Hii ni sawa na wastani wa vifo 48.99 kwa kila vifo 100,000  na kulifanya shirika hilo kuiweka Tanzania katika nafasi ya 10 duniani kwa viwango vya malaria.

Makundi yaliyo hatari zaidi kushambuliwa na ugonjwa huo ni wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, kwa sababu wanaoshambuliwa wanaongezeka.

Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto pamoja na Viashiria vya Malaria nchini ya mwaka 2022 (TDHS- MIS), ilionyesha kwa mwaka 2022 maambukizi ya malaria kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi miaka mitano yalikuwa asilimia 7.9.

Mikoa saba ilikuwa na viwango vya juu zaidi ya wastani, ikiongozwa na Tabora asilimia 23.4, Mtwara 19.7, Kagera 17.5, Shinyanga 15.6, Mara 15.1, Geita 13.4, Kigoma 12.7, Lindi 11.2, Simiyu 11.2 na  Katavi 8.1.

Mikoa mingine tisa ilikuwa na wastani wa chini ya asilimia moja, ukiwamo Arusha, Kilimanjaro, Singida, Songwe na mikoa yote ya visiwani Zanzibar.


Changamoto

Zipo sababu nyingi za tatizo hili ila TDHS- MIS imeainisha mbili za kitakwimu ambazo ni matumizi ya chandarua na dawa za kukinga malaria kwa wajawazito.

Mfano ni robo ya wajawazito pekee waliopata dozi ya kuzuia malaria angalau mara tatu.

Mikoa inayoongoza kwa malaria pia inaongoza kwa wajawazito kutotimiza dozi zote nne.

Kwenye matumizi ya chandarua, Mkoa wa Tabora ulikuwa wa mwisho kwa watu wake kutumia chandarua. Ni watu asilimia 66 pekee waliotumia chandarua usiku uliopita kabla ya utafiti huo. Mikoa mingine ni Simiyu na Kigoma.


Imeandaliwa kwa msaada wa Bill & Melinda Gates