Malori ya Tanzania zaidi ya 250 yashikiliwa DR Congo

Dar es Salaam.  Malori 250 ya mizigo kutoka Tanzania yanayobeba madini ya shaba kutoka Congo, yanashikiliwa nchini humo kwa kile kinachodaiwa baadhi ya kampuni za migodi zinadaiwa kodi.

Hilo limethibitishwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Congo, Said Mshana alipozungumza kwa simu na Mwananchi kuhusina na sakata hilo.

Hata hivyo, Balozi Mshana alisema tayari ofisi yake imeshaanza kulishughulikia tatizo hilo huku akiwataka madereva na wamiliki wa malori hayo kutoa ushirikiano.

“Hili suala limekaa kidiplomasia zaidi, lazima lishughulikiwe kwa kufuata utaratibu wote.

Tukikurupuka na baadaye ikabainika ni kweli kuna tatizo la kikodi tutaonekana kama tunawatetea wakwepa kodi, jambo ambalo hata nchi yetu huwa ikipambana na watu wa aina hii,” alisema Balozi Mshana.

Hivyo, alisema itoshe tu kusema ofisi ya ubalozi inalishughulikia suala hili kwa karibu na tayari mazungumzo yameshaanza.

Alisema ataendelea kutoa taarifa kalingana na hatua watakazokuwa wamefikia, “Sio malengo yetu kuona Watanzania wanaishi huku kwa shida.”


Walichosema Tamstoa

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha wamiliki malori wa kati na wadogo Tanzania (Tamstoa), Chuki Shabani akizungumza na Mwananchi kuhusiana na hilo, alisema mpaka jana malori hayo yanashikiliwa kwa siku 44, katika eneo  linaloitwa Wiski Kasumbaresa upande wa Congo.

 Shabani alisema inasemekana migodi inayochimba madini hayo  ambayo malori huenda kubeba mzigo huo wa shaba kuleta nchini kwa ajili ya kusafirishwa kwa njia ya bandari kwenda nchi zingine, inadaiwa kodi na Serikali ya Congo.

Mwenyekiti huyo alisema hata kama kosa ni hilo, isiwe sababu ya serikali hiyo kushikilia magari, bali wangeruhusu mizigo hiyo ishushwe na madereva na wafanyabiashara wa shaba hiyo waendelee na mambo mengine.

“Tumeambiwa hata yale magari ambayo yameingia ndani ya migodi yatashikiliwa pia mpaka Serikali ya Congo itakapomalizana na wamiliki wa migodi hiyo, hii si sawa,” alisema mwenyekiti huyo.

Alisema kushikilia gari la biashara kwa siku 44 ni nyingi na kunakwamisha kazi zingine na kuwaongezea gharama madereva zisizo za lazima.


Shabani alisema mpaka sasa madereva na utingo wao wanaishi kwa tabu nchini humo kwa sababu tayari wameishiwa vyakula na fedha na eneo waqlipo halina huduma muhimu za kujikimu halina hata vyoo hali inayohatarisha pia afya zao.

“Wakati wanachama tukiwa na kikao chetu kulijadili hilo, tukaona tuzungumze na chombo cha habari ili serikali na umma ujue nini tunachopitia kwa sasa ili kuweza kutoa msaada katika mgogoro huo kwa sababu hali imekuwa mbaya sio kwetu tu bali hata kwenye uchumi wa nchi.

“Nasema hali ni mbaya hadi kwa nchi kwa kuwa magari yaliyoko kule yalipaswa kununua mafuta na kuiingizia nchi kodi ,lakini hayawezi kufanya hivyo kwa sasa, kuna wakati madereva wanapita kula kwa mama Ntilie, lakini hawapiti tena, kwa hiyo  imekuwa shida kubwa ambayo inaenda kuathiri na uchumi wa nchi.

Venance Msaki mmoja wa wanachama wa Tamstoa alisema  wamekuwa wakipata gharama kutokana na sakata hilo, kwani kwa Tasac pekee huchaji dola 60,000 kila siku  kwa gari kukaa nchini humo na kontena ,lakini bado gharama za kuwahudumia madereva na utingo wao.

“Tumekaa kimya kwa siku zote hizo 40, tukijua labda serikali ya Congo ingeachia magari yetu lakini haijawa hivyo, hivyo tunaiomba serikali yetu kwa kuwa tunaijua ni sikivu itusaidie hata wakituambia tushushe mizigo turudi tupu, tupo tayari ili tuje tufanye kazi zingine Tanzania, “alisema Msaki.

Akilizungumzia hilo, Balozi Mshana alisema wao wanasikiliza muafaka utakaofikiwa na wamiliki, madereva na mwenye mzigo.

“Nasema hivyo pia kwa sababu siku mwenye mzigo akija kulalamika ametupiwa mzigo wake njiani au umeibiwa, hatutakuwa na majibu,” alisema.

Hata hivyo alisema katika hilo wanataka wakubaliane wenyewe kwanza, kisha watoe taarifa ni kipi wamekiamua waweke kwenye maandishi.

“Kinyume na hapo hatuwezi tu tukawaruhusu watu kutelekeza mizigo ya watu kwa kuwa hata wakati wanapewa kazi hiyo walipeana kwa makubaliano,”alisema Balozi huyo.

Naye Amani Urasa ambaye ni mwananchama pia, aliliambia gazeti hili kuwa anapitia wakati mgumu, kwa sababu gari lake lililozuiwa Congo alilinunua kwa mkopo.

“Sasa kulizuia Congo lisiendelee kufanya kazi nyingine wti sababu tu mwekezaji huyo anamgogoro wa kikodi na serikali yake, kuna nipa wakati mgumu sana wa kulipa mkopo wangu, nategemea gari lifanye kazi ndipo nilipe deni,” alisema.

Aliongeza; “Katika hili tunaomba serikali kusogea karibu nasi kwa kuwa ndiyo kipindi tunahitaji zaidi joto lake kuliko kipindi kingine chochote.”


Dereva azungumzia hali ilivyo

Mmoja wa madereva aliyepo nchini humo, aliyetambulika kwa jina moja la Dula, aliiambia Mwananchi kwa simu kuwa kuna magari yanayoendelea kushikiliwa katika mpaka wa Kasumbaresa kati ya mpaka wa Congo na Zambia na mengine yako eneo la Whisk kilometa kumi kabla ya kufika Kasumbaresa.

Alisema hapo pana maegesho ya magari na hukaguliwa kabla ya kuanza safari.

“Kwa hiyo sisi wametuweka uwanjani tu mahali ambako hakuna huduma yoyote, tukitaka kujisaidia tunaenda popote tu kwa sababu hakuna vyoo,” alisema Dula.


Kumbe sio mara ya kwanza

Hata hivyo, inaelezwa kuwa huu hii si mara ya kwanza kwa malori yanayobeba shaba kuzuiwa Congo.

Balozi Mshana alisema hivi karibuni malori 54 yanayosafirisha mizigo kwa kampuni zaidi ya 54 zilishawahi kushikiliwyalishikiliwa nchini humo.

Alisema mpaka sasa malori zaidi ya 500 kutoka Tanzania huingia nchini humo kwa ajili ya kubeba shaba.