Mama amuunguza mwanaye wa miaka minne kwa kula chukula bila ruhusa

Kaimu Kamanda Polisi Mkoa wa Simiyu, Shadrack Masija akizungumza na waandishi wa habari

Muktasari:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linamshikilia mkazi wa Mtaa wa Kidinda Wilaya ya Bariadi, Mwamba Thomas (36) kwa tuhuma za kumuunguza kwa maji ya moto mtoto wake mwenye umri wa miaka minne akimtuhumu kuiba na kula chakula wakati alipokuwa matembezini.

Bariadi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linamshikilia mkazi wa Mtaa wa Kidinda Wilaya ya Bariadi, Mwamba Thomas (36) kwa tuhuma za kumuunguza kwa maji ya moto mtoto wake mwenye umri wa miaka minne akimtuhumu kuiba na kula chakula wakati alipokuwa matembezini.

Akizungumzia tukio hilo leo Aprili 27, 2022 Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa huo, Shadrack Masija amesema tukio hilo limetokea Aprili 22, 2022 ambapo amesema mtoto huyo alichomwa na maji ya moto kwenye mikono yake miwili na mama yake na amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Bariadi kwa ajili ya matibabu.

"Chanzo cha tukio hilo ni mtoto huyo kuiba tambi ambazo ziliandaliwa kwa ajili ya chakula cha mchana, ndipo mama wa mtoto huyo alichukua hatua ya kumchoma kwa maji ya moto ambayo yalisababisha majeraha kwa mtoto," amesema Masija.

Aidha mganga mfawidhi katika Hospitali ya Mji wa Bariadi Somanda, Yohana Costantine amesema wamempokea mtoto huyu akiwa na majeraha ya kuunguzwa na moto na amelazwa hospilini hapo kwa ajili ya matibabu.

"Tumempokea akiwa na majeraha makubwa mikono yote miwili, amelazwa hapa kwa ajili ya uangalizi na anaendelea vizuri ikilinganishwa na siku ya Kwanza alivyoletwa hapa," amesema Dk Costantine.

 Akiwa katika kitanda cha hospitali akiugulia maumivu mtoto huyo maarufu kwa jina na Hindia amesema alikula tambi akiwa na mdogo wake wakati ambao mama yao alipoondoka nyumbani na alivyorudi ndipo alimpiga pamoja na kumchoma maji ya moto mikononi.

"Alinipiga kisha akawasha moto na kuweka sufuria ya maji yalipochemka akaniweka mikono yote kwenye maji sufuria ikiwa jikoni," amesema Hindia.

Siku ya tukio ilivyokuwa

Hindia akiwa na mdogo wake walichukua tambi zilizokuwa zimetunzwa kwa ajili ya chakula cha mchana na kuzila kabla ya wakati.

Wakisimulia ilivyokuwa watoto waliokuwepo eneo la tukio wamesema waliweka chakula nje ya mlango na kuanza kula baada ya kumuona mama yao warudisha chakula walichokuwa wanakula ndani ya nyumba.

"Alipofika alianza kuwapiga wote na kuwapa kile chakula wakile hadi wamalize akiwaambia kuwa wasipo maliza atawachoma na maji ya Moto" amesema mtoto mmoja.

Wanasema Hindia alishindwa kula chakula hicho kutokana na kipigo na baadaye mama yake aliwasha moto kisha akabandika maji kwenye sufuria yalipo chemka akaweka mikono ya mwanae.

"Asubuhi ya siku inayofuata pombe zilipomuisha akaanza kulia kwa sauti baada ya kuona vidonda vya Hindia akisema atajiua" amesema mtoto mwingine.

Mwamba Thomas anashikiliwa katika kituo Cha Polisi Bariadi na watoto wake wawili wakiwa chini ya uangalizi wa dawati la jinsia huku Hindia akiwa hospitali chini ya uangalizi wa maafisa wa ustawi wa jamii.