Mama mbaroni akituhumiwa kuwachoma moto watoto wawili

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issah

Muktasari:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamshikilia mkazi wa Nyombo Tarafa ya Lupembe wilayani Njombe, Adelina Ngollo (36) kwa tuhuma za kuwachoma moto watoto wake wawili na kuwasababishia madhara makubwa.

Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamshikilia mkazi wa Nyombo Tarafa ya Lupembe wilayani Njombe, Adelina Ngollo (36) kwa tuhuma za kuwachoma moto watoto wake wawili na kuwasababishia madhara makubwa.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi mkoa huo, Hamis Issah  wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Njombe.

Amesema mwanamke huyo anadaiwa kuwachoma watoto hao ambao mmoja ana umri wa miaka (4) na mwingine (7) kutokana na tabia yao ya kwenda kwa majirani na kuombaomba chakula.

"Kitendo alichokifanya mama huyu akikubaliki kabisa akidai sababu ya kuwachoma moto hawa watoto hakuwa makini kuwaangalia kwani watoto walikuwa wanatembea tembea kwa majirani na kuomba chochote kitu ili wajikimu na siku iende," amesema Issah.

Amesema baada watoto hao kuwa na tabia hiyo majirani walimuita mwanamke huyo na kumueleza kuwa malezi ya watoto hao siyo mazuri, maneno hayo yalimuumiza na kuyaweka moyoni.

Kamanda Issah ameeleza kuwa mwanamke huyo alipofika nyumbani kwake aliwaamsha watoto wake wawili na kuwachoma moto kwa kutumia jiko la mafiga matatu linalotumia kuni na kuungua mikononi na sehemu zingine za mwili.

Amesema mwanamke huyo alidai kuwa amefanya ukatili huo kwakuwa watoto wake hao wameshindwa kumlea mdogo wao mwenye umri wa mwaka mmoja.

"Najaribu kufikiri kweli watoto wa miaka saba na minne wanaweza kumlea mtoto wa mwaka mmoja huku mama mwenye watoto watatu akiwa ameshindwa kuwalea na kuwaacha wanakuwa ombaomba?" amesema Issah.

Amesema baada ya kuwachoma moto watoto hao aliwafungia katika chumba mpaka mwanakijiji mmoja ambaye alisikia uchungu na kutoa taarifa ambapo watoto walikutwa wakiwa na hali mbaya.

Kamanda huyo amesema kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo kimepelekea wanakijiji kuwa tayari kuwachukua watoto hao na kuwalea huku wakiomba sheria kufuata mkondo wake.

Amewataka wananchi mkoani Njombe kuwalea watoto katika misingi mizuri na kuacha tabia ya kuwapa majukumu watoto ya kuwalea watoto wenzao.