Mama, mtoto waliwa na fisi, wa miaka mitatu anusurika

Mama, Mtoto waliwa na fisi, wa miaka mitatu anusurika

Muktasari:

  • Ukuu wa Mungu umejidhihirisha kwa Agnes Joel, mtoto mwenye umri wa miaka mitatu aliyenusurika kifo katika matukio mawili yaliyopoteza maisha ya wengine.

Tabora. Ukuu wa Mungu umejidhihirisha kwa Agnes Joel, mtoto mwenye umri wa miaka mitatu aliyenusurika kifo katika matukio mawili yaliyopoteza maisha ya wengine.

Katika tukio la kwanza, mtoto huyo hakugongwa na nyoka aina ya koboko aliyewaua mama yake mzaziEster Saimon na nduguye mkubwa, Mrisho Amir (11). Wakati nyoka anamgonga mama yake, mtoto huyo alikuwa amebebwa mgongoni.

Kana kwamba hiyo haitoshi, mtoto huyo aliendelea kuwa hai hata fisi walipofika eneo la tukio na kuila maiti ya ndugu yake hadi kubakiza fuvu la kichwa pekee.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Safia Jongo amesema mtoto huyo aliokolewa siku tano baadaye akiwa amedhoofu na kulala pembeni mwa maiti ya mama yake iliyoharibika.

“Hakuna neno lingine zaidi ya kusema ni muujiza na maajabu ya Mungu mtoto mdogo wa miaka mitatu kunusurika kifo cha kugongwa na nyoka hata kuliwa na fisi licha ya kulala porini kwa zaidi ya siku nne,” alisema kamanda Jongo.

Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Peres Magiri alisema mama wa mtoto huyo na mwanaye mkubwa hayajajulikana alikuwa akitembea kwa miguu kwenda Kijiji cha Kanyamsenga.

“Tukio hilo limetokea Kijiji cha Kikungu. Mwili wa mama umekutwa umeharibika vibaya huku ule wa mtoto wake mkubwa ukiwa umeliwa na fisi na kusalia fuvu la kichwa pekee,” alisema Magiri

Maelezo yote alisema yalitolewa na mtoto huyo mdogo aliyekutwa pembeni ya maiti ya mama yake akiwa hoi kwa njaa na uchovu.

“Baada ya kuokolewa na kunyweshwa uji, mtoto huyo alipata nguvu na kueleza tukio nzima ambapo alisema mama na ndugu yake walianguka chini na kunyamaza kimya baada ya kung’atwa na likitu lirefu,” alisema Magiri.

Kutokana na maelezo hayo, mkuu huyo wa wilaya alisema walibaini kuwa vifo vya wawili hao vilitokana na kugongwa na nyoka aina ya koboko wanaopatikana eneo hilo.

“Mtoto huyo alisimulia pia jinsi alivyowaona fisi wakimla ndugu yake. Ni tukio siyo tu la kutisha bali la kushangaza mtoto huyu kutodhurika katika matukio yote mawili. Hakika ni Mungu ndiye amemwokoa na kifo,” alisema Magiri.

Mkuu huyo wa wilaya alisema juhudi za kufuatilia utambuzi wa marehemu zinaendelea na taarifa zaidi zitatolewa.

Diwani wa Chabutwa, Edward Almasi, aliwatambua mama, mtoto aliyefariki na aliyenusurika.