Mama, mtoto wasumbuliwa na ugonjwa wa ajabu, waomba msaada

Mkazi wa Kijiji cha Imbilili Juu Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara, Safari Gidale ambaye ni mtoto wa Helena Hungoli akizungumzia maumivu anayopata kutokana na ugonjwa wa kuota nyama upande wake wa kishoto wa mwili. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

Helena Hungoli (60) na mwanaye Safari Gidale ambao ni wakazi wa Kijiji cha Imbilili Juu, Babati Mkoani Manyara, wameiomba Serikali na wasamaria wema kuwapa msaada kwani wanaugua ugonjwa wa kuota nyama mwilini zinazowasababishia maumivu makali.

Babati. Mwananchi wa Kijiji cha Imbilili Juu, Halmashauri ya mji wa Babati Mkoani Manyara, Helena Hungoli (60) ameiomba Serikali na wasamaria wema kumpa msaada, kwani anaugua ugonjwa wa ajabu hivyo anahitaji matibabu.

 Hungoli amesema ugonjwa huo ambao ngozi yake imeota na kuning'inia hivyo kufunika upande mmoja wa uso pamoja na mdomo na kumsababishia maumivu makali.

Akizungumza nyumbani kwake kwa taabu mama huyo amesema kwa sasa hawezi kufanya kazi yoyote ya kumuingizia kipato kutokana na kuwa na hali hiyo tangu akiwa mtoto mdogo.

“Kila sehemu ya mwili wangu inauma na kwa hali niliyokuwa nayo inabidi nishinde nyumbani muda wote na sasa nahitaji msaada mkubwa, serikali na wasamaria wema nisaidieni,” anasema.

Mbali na mama huyo, mtoto wake anayejulikana kwa jina la Safari Gidale naye amekumbwa na ugonjwa huo kwa kuota nyama upande wake wa kushoto wa mwili wake.

Ugonjwa huo unamsababishia Gidale maumivu na uzito upande mmoja hali inayomfanya atembee akiwa amepinda hana wa kumsaidia yeye na mama yake na kuomba msaada wapate matibabu.

 “Tunaiomba serikali na wasamaria wema wenye uwezo watusaidie tupate matibabu kwani hivi sasa mimi na mama yangu hatuna msaada wowote ule tunateseka hapa nyumbani,” amesema.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Imbilili juu Hassani Suleiman amesema kwa hali ya mama huyo iliwaogopesha majirani mpaka kumkimbia hali iliyomfanya awe katika mazingira magumu zaidi.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho Suleiman amesema baada ya kuonekana mara kwa mara wananchi wa eneo hilo walizoea hali hiyo na wakawa wanawatembelea na kuwapa chakula.

“Wanaishi kwenye mazingira magumu mno kwani hata kupata mlo wa chakula mara tatu kwa siku kama watu wengine inakuwa changamoto kutokana na hali duni ya uchumi,” amesema.

Mdogo wa mama huyo Josephina Hungoli ameelezea matumaini yake na kusema sasa anaona mwanga utaonekana baada ya waandishi wa habari kufika nyumbani kwao kijiji cha Imbilili Juu.

“Kupitia ninyi waandishi wa habari tuna matumaini makubwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu watatupa msaada wa matibabu ili ndugu zangu wasaidiwe,” amesema.

Namba ya msaada 0682995922 -Jina Hemedi Samweli Maganga.