Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mama na baba lishe soko la Kisutu wakabidhiwa vibanda

Kaimu Mkurugenzi wa Fao, Abebe Gabriel akihutubia katika uzinduzi wa kampeni ya ulaji unaofaa kwa kutumia vyakula vya asili, Kisutu jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Wafanyabiashara wa chakula maarufu mama na baba lishe katika soko la Kisutu jijini hapa, wamekabidhiwa vibanda ikiwa ni hatua ya kuwaongezea ufanisi katika kazi zao.

Dar es Salaam. Wizara ya Kilimo ikishirikiana na Shirika la Chakula duniani (FAO) na taasisi ya kiraia ya Agrithamani imekabidhi vibanda 35 kwa wafanyabiashara wa chakula maarufu baba na mama ntilie katika soko la Kisutu jijini hapa ikiwa ikiwa ni hatua ya kuongeza ufanisi katika kazi zao.

Vibanda hivyo ambavyo vimetolewa na Fao vimekabidhiwa kwa wafanyabiashara hao katika kuhamasisha mapishi ya vyakula vya asili ili kuwawezesha walaji kula chakula chenye lishe bora.

Akizungumza katika halfa hiyo ya uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha ulaji unaofaa kwa kutumia vyakula vya asili hapa nchini, leo katika soko hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Fao, Abebe Gabriel amesema watu wengi barani Afrika hula chakula ambacho hakina lishe bora.

"Twakimu zinaonyesha takribani watu bilioni moja barani Afrika hawawezi kumudu gharama za kula chakula bora," amesema Abebe.

Aidha amesema ili kuondoa changamoto hiyo ni wakati wafanyabiashara hao wa vyakula kupika vyakula vya asili ambavyo vina virutubisho muhimu kwa ajili ya lishe bora.

"Suluhisho tunalo wenyewe, ni kwa kupitia vyakula vyetu vya asili na sio kutoka mahali pengine," ameongeza Abebe.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mobhare Matinyi, ambaye alikuwa amemuawakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesema licha ya nchi kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 100, lakini bado liko tatizo la utapiamlo kwa watoto ambalo ni matokeo ya lishe duni.

"Hali hii ya lishe duni imesababisha vifo kwa watoto na wanawake hasa wajawazito wakati wa kujifungua kutokana na upungufu wa damu," amesema Matinyi.

Amesema madhara mengine ni pamoja na watoto kuathirika kiakili na baadae kuwa na kizazi ambacho kina mchango mdogo kwa taifa.

"Mifumo ya chakula inahitaji kuimarishwa kuanzia ngazi ya uzalishaji hadi chakula kinapomfikia mlaji. Mama na baba ntilie ni watu muhimu katika hili kwani wakazi wengi mijini hupata chakula kutoka kwao hivyo ni muhimu waangaliwe ile kuhakikisha wanatoa lishe bora kwa jamii," amesema Matinyi.

Naye Meneja wa Agrithamani Theobald Sylvester amesema programu hiyo imeanzia jijini hapa na baadae itaenda katika mikoa mingine ikiwemo Dodoma na Mbeya.

"Tunatarajia kuendelea kutoa vibanda hivi katika mikoa mingine, lakini tuna utaratibu wa kuwafuatilia ili kuona namna gani vinawasaidia," amesema.

Pia amesema upishi wa vyakula vya asili kwenye maeneo ya mijini utachagiza kukuza vipato kwa wafanyabiashara hao kwani wapo watu wengi wanatamani kupata vyakula hivyo lakini inawalazimu kusubiri nyakati za likizo wanaporudi katika maeneo yao ya asili.

Mamalishe katika soko hilo, Pili Dennis amezishukuru taasisi hizo kwa kuwapatia vibanda hivyo na kusema hiyo itawaongezea ari ya kufanya kazi kwa bidii.

"Tunashukuru sana, naamini hata kipato changu kitaongezeka kwa sababu sasa nitakuwa na maeneo mawili ya kuuzia chakula," amesema Pili.