Mama Tunu Pinda awataka wanawake Songwe kupinga ukatili

Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani katika Mkoa wa Songwe, mama Tunu Pinda ambeye ni Mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda akizungumza na mama mwenye ulemavu wakati wa maadhimisho hayo.

Mbozi. Wanawake wametakiwa kupaza sauti ili kupinga vitendo vya ukatili vinavyofanywa katika jamii zao.

Pia, wametakiwa kuungana katika vikundi ili kunufaika na fursa zinazojitokeza katika maeneo yao.

Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Machi 8, 2023 na Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mkoa wa Songwe, mama Tunu Pinda ambeye ni Mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.

Mgeni huyo rasmi amesema vipo vikwazo ambavyo vimekuwa vikikwamisha wanawake kujikwamua kiuchumi ikiwamo mila, kutokuthubutu na kukata tamaa.

Amewataka wanawake kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na Serikali ili kuwawezesha kuinuka kiuchumi.

"Kina mama kopeni msiogope maadamu mnarudisha, kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo yetu ili kuanzisha viwanda" amesema

Amesema Serikali ipo tayari kuwapa wanawake mikopo nchini kupitia asilimia 10 za mapato ya halmashauri hivyo wanawake watumie fursa hiyo.

"Tuungane pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kufikiria nje ya boksi, kila fursa inayotokea mwanamke awe mbele   ili afanikiwe" ameshauri mgeni huyo rasmi

Amesema kutokana na kutokuwepo usawa wa kijinsia, bado wanawake wanashindwa kujikwamua kutokana na kukandamizwa hivyo amewataka kuungana kupinga mila na tamaduni katika jamii.

Amesema ni wakati wa wanawake kuungana na kupambana kupinga ukatili wa kijinsia.

"Tupambane kupinga ukatili wa kijinsia. Tuhakikishe vitendo vya udhalilishaji kutokomea nchini" amesema

Pia, amewataka wanawake kuzingatia lishe ili kutokomeza udumavu kwa watoto.

"Suala la lishe ni muhimu kwa watoto wetu, elimu itolewe kuanzia kwa mama anayetarajia kupata ujauzito na aliye na ujauzito kwa kila kaya ili kupata watoto wenye afya bora" amesema


DC Mbozi awapa wanawake siri ya mafanikio

Katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi (DC), Esther Mahawe amewataka wanawake wa mkoa wa Songwe kutokata tamaa wakati  wanapoanguka katika safari ya kujikwamua kiuchumi bali wapambane huku akiwashauri wanawake walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika nafasi mbalimbali kufanya kazi kwa bidii.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi (DC), Esther Mahawe ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe (RC), Dk Francis Michael akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mkoa wa Songwe.

DC Mahawe ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael katika kilele cha maadhimisho hayo ambayo kimkoa yanafanyika katika viwanja vya CCM Vwawa wilayani Mbozi  amesema kuwa katika zama hizi mwanamke anatakiwa apambane na pale anapojaribu na kufeli asikate tamaa.

"Tukikaa tukisubiri kuwezeshwa tutachelewa, hizi ni kauli ambazo zimetucheleweshwa kwamba katika mafanikio ya mwanaume mwanamke yuko nyuma" amesema DC huyo na kuongeza;

Tumezubaishwa, sasa hivi ni pembeni ya kila baba aliyeendelea yuko mama na pembeni ya kila mama aliyeendelea kuna baba" amesema

Amesema sababu inayowachelewesha wanawake wengi ni kutokujiamini hivyo kutoa wito kwa wanawake wajiamini.

"Kutokujiamini na kutothubutu, mwanamke unaweza sana, ukianguka nyanyuka anza tena... kufeli ni sehemu ya kukupeleka kwenye mafanikio, feli sana na jaribu sana utafanikiwa" amesisitiza

Ametoa wito kwa wanawake ambao wamepata nafasi hasa za kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika ngazi mbalimbali kufanya kazi kwa bidii ili kudhihirisha kuwa wana uwezo.

"Niwaombe wanawake tulioaminiwa na Rais Samia tusijaribu kumuangusha, tunaweza sana tuamini kuwa tunaweza" ameshauri

"Ni neema Mungu kumchagua Rais Samia ili kuonyesha mfano kuwa wanawake tunaweza" amesisitiza

Aidha Mkuu huyo wa wilaya amewashauri wanawake waliopata nafasi kutowadharau waume zao.

"Nafasi ya mwanaume itabaki palepale, sio kuwa mwanamke umepata fursa ndio uwadharau wanaume hapana, hata kama una fedha kuliko yeye, Mungu akupe hekima
Sio una fedha zako nyumbani unataka uwe kiongozi" ameshauri DC huyo huku washiriki wakishangilia