Mama, watoto wawili wanusurika kifo kwa kushambuliwa na mbwa wanaowafuga

Picha ikionyesha mbwa aina ya Bull Dog

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwananchi Digital  kuhusu tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Januari 8, 2024, Baba wa familia hiyo, Nicholas Kunju amesema hali za majeruhi hao inaendelea vema baada ya kutibiwa katika Hospitali ya CF ya jijini Mwanza.

Mwanza. Mama na watoto wawili, wakazi wa eneo la Usagara Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, wamenusurika kifo baada ya kushambuliwa na mbwa wao waliokuwa wakiwafuga.

Akizungumza na Mwananchi Digital  kuhusu tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Januari 8, 2024, Baba wa familia hiyo, Nicholas Kunju amesema hali za majeruhi hao inaendelea vema baada ya kutibiwa katika Hospitali ya CF ya jijini Mwanza.

"Ni kweli tukio hilo limetokea na walioshambuliwa na mbwa hao aina ya Bull Dog ni mke na watoto wangu wawili. Mke wangu alishambuliwa akiwa katika jitihada za kuwasaidia watoto wetu wasishambuliwe na mbwa," amesema Kunju.

Amesema familia yake imewafuga na kuishi na mbwa hao wa kike na kiume kwa takribani miaka saba, na anajiuliza kilichotokea hadi mbwa wake dume kuchachamaa na kuwashambulia watoto.

"Mbwa wangu walikuwa aina ya Bull Dog na nimeishi nao takribani miaka saba. Yupo mtu anayewatunza. Watoto wangu walirejea likizo na tumeishi bila tatizo hadi usiku wa juzi tukio hilo lililotokea," amesema.

Amesema kwa kipindi chote cha likizo ya watoto, mbwa wake ambao hawakuwa na tatizo lolote la kiafya kutokana na tiba ikiwemo chanjo mbalimbali anazowapatia, hawakuonyesha dalili zozote za ukali wala hasira kiasi kwamba tukio la juzi bado limewaacha na maswali mengi.


Tukio lilivyotokea

"Mtoto wangu mmoja ambaye yuko kidato cha nne alitoka nje usiku kufanya shughuli zake, yule mbwa dume akamnyemelea na kumtishia, kabla ya kuanza kumshambulia,"  amesema Kunju.

Amesema kelele za kuomba msaada zilimfanya mke wake kutoka nje na kwa kushirikiana na mbwa jike akafanikiwa kumdhibiti mbwa dume na wote watatu kuingia ndani, huku mbwa wote wawili wakibaki nje wakiendelea kubweka.

"Vurugu zilizoambatana na kelele za mbwa kubweka ziliwashtua majirani ambao walipiga simu iliyowezesha askari Polisi kufika na kuwadhibiti mbwa wale kwa kuwapiga risasi, na majeruhi kuwahishwa hospitali kwa matibabu," amesema baba huyo wa familia.


Matibabu 

Amesema baada ya kufikishwa hospitalini, majeruhi walipewa huduma mbalimbali ikiwemo kuchomwa sindano ya kichaa cha mbwa katika Hospitali ya CF, kabla ya kupelekwa Hospiali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa uchunguzi na tiba zaidi.

Baadaye majeruhi hao waliruhusiwa  kurejea nyumbani na hali zao zinaendelea vizuri.

Meneja wa Hospitali ya CF ya jijini Mwanza, Noel Chacha amesema pamoja na huduma nyingine, majeruhi hao walitibiwa majeraha na kufanyiwa vipimo kadhaa, kubaini iwapo wamepata madhara mengine zaidi ya majeraha yaliyokuwa yanaonekana kwa macho.

"Baada ya wataalamu kujiridhisha na hali zao kiafya waliruhusiwa kurejea nyumbani usiku ule ule, kabla ya kurejea tena hospitali kulipokucha kwa huduma zaidi," amesema Chacha.


Wataalam wa mbwa

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Joseph Ndalu, mtaalamu wa mifugo amesema mbwa aina ya Bull Dog ni kundi na aina ngumu kufugika, kutokana na kuwa na tabia ya kubadilikabadilika.

"Ni jambo la kawaida kwa mbwa aina ya Bull Dog kushambulia siyo mgeni pekee, bali hata mmiliki au mtu anayemuhudumia pindi anapohisi mazingira au uwepo wa wageni asiowazoea. Ni muhimu mtu au watu wanaowafuga mbwa wa aina hiyo kupata mafunzo na elimu maalumu jinsi ya kuwafuga na kuishi nao," amesema Ndalu. 

Akizungumzia hali iliyojitokeza kwa familia ya Kunju, mtaalamu huyo amesema; "Yawezekana ujio wa watoto pale nyumbani ulionekana kama vile ni wageni iwapo mbwa wale walikuwa wanafungiwa bandani. Yawezekana watoto hawakuwa na ukaribu na mbwa wale tangu waliporejea likizo.


Charles Oging', mtaalamu wa mifugo amesema japo mbwa aina ya Bull Dog siyo wakali na wakorofi kulinganisha na aina nyingine ya Rottweiler, kuna mazingira manne yanayoweza kusababisha wabadilike tabia na hata kuwashambulia wamiliki, watu wanaowatunza na wageni bila kutarajiwa.

"Moja ya sababu zinazoweza kumfanya mbwa kumshambulia mtu yeyote ni ugeni. Lakini mbwa dume pia wanaweza kubadilika tabia na kumshambulia mtu yeyote anayemsogelea mbwa jike aliye kwenye heat (nyakati za kutunga mimba) kwa sababu ya tabia ya wivu," amesema Oging'.

Mtaalamu huyo amesema zaidi ya ugeni na wivu, maradhi ikiwemo kichaa cha mbwa pia kinaweza  kusababisha mbwa kumshambulia mmiliki, anayemtunza na wageni.