Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mama yake Frateri anayedaiwa kujinyonga naye afariki dunia

Baadhi ya ndugu jamaa na marafiki wakienda kutoa pole nyumbani alikozaliwa marehemu Levina Hugo, katika Kijiji Cha Umbwe Onana. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Frateri huyo alizikwa Mei 25, 2024 baada ya kudaiwa kujinyonga kwa kutumia mshipi Mei 20, mwaka huu akiwa kwenye nyumba yao ya malezi ya Magamba iliyopo wilayani Lushoto, mkoani Tanga.

Moshi. Zikiwa zimepita siku 16 tangu Frateri wa Kanisa Katoliki, Rogassian Massawe (25) anayedaiwa kujinyonga hadi kufa azikwe nyumbani kwao, katika Kijiji cha Umbwe Onana, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, mama yake mzazi, Levina Hugo (58) naye amefariki dunia.

Frateri huyo alizikwa Mei 25, 2024 baada ya kudaiwa kujinyonga kwa kutumia mshipi Mei 20, mwaka huu akiwa kwenye nyumba yao ya malezi ya Magamba iliyopo wilayani Lushoto, mkoani Tanga.

Kabla ya kutekeleza hilo, Frateri Massawe inadaiwa kuwa aliacha ujumbe wa maandishi kwa mama yake mzazi uliosomeka; “mama usilie, nimeshindwa kufikia malengo, najua nimewakwaza wengi."

Siku ya maziko Mei 25, 2024 nyumbani kwao, ndugu wa familia hiyo, Padri Andrea Hugo, aliwaomba waombolezaji kuiombea familia hiyo kwa kuwa mama yake mzazi Frateri huyo aliugua ghafla na kulazwa Hospitali ya KCMC, hivyo hakuweza kushiriki maziko ya mwanaye kwa mshituko alioupata.

"Familia hii inaendelea kushukuru kwa namna ambavyo mmetukimbilia, tunaomba mtuombee, mumwombee na mama ambaye yupo hospitali amelazwa," alisema Padri Hugo na kuongeza;

"Leo asubuhi tulimpeleka tena hospitali baada ya kumpeleka jana, madaktari wamesema hawezi kurudi wala kuruhusiwa kutokana na hali yake kuwa mbaya, presha imepanda na sukari nayo ipo juu sana. Tumwombee na mtuombee kama familia."

Baada ya Padri Hugo kutoa taarifa hiyo, mamia ya waombolezaji waliokuwepo msibani walishikwa na huzuni zaidi huku baadhi yao wakishindwa kujizuia na kuangua vilio. Walikuwa wakikaa makundi kwa makundi, wakijadili utata wa kifo cha Frateri huyo na namna mama yake alivyoshindwa kushiriki maziko ya mwanaye.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Juni 10, 2024, nyumbani alikozaliwa mama huyo eneo la Umbwe Onana, wilayani Moshi, mdogo wa marehemu, Jerome Aloyce amesema wamepata pigo lingine kwenye familia.

Aloyce amesema wapo kwenye wakati mgumu sana kwa sababu wamepoteza watu wawili ndani ya muda mfupi.

"Dada yetu tangu apate taarifa za mwanaye kufariki kule Tanga, hajawahi kukaa sawa maana alibadilika ghafla na kwa kipindi chote alikuwa Hospitali ya KCMC. Alishindwa hata kumzika mwanaye kutokana na mshituko alioupata kufuatia kifo hicho. Kifo chake kimetuumiza sana kama familia, kupoteza watu wawili kwa wakati mmoja ni pigo kubwa," amesema Jerome.

Akizungumzia mipango ya maziko, Aloyce amesema yatafanyika Jumamosi, Juni 15, 2024 katika Kijiji cha Umbwe Onana.

Maria Thadey, mmoja wa ndugu wa familia hiyo ambaye pia ni shangazi wa marehemu, amesema taarifa za msiba wa mama huyo zimemshtua kila mtu kwenye familia na kijiji kwa ujumla.

"Huyu ndugu yetu alipopata taarifa za msiba wa mtoto wake aliumia, alilia sana tunahisi huenda hali hii ndiyo imechangia kifo chake,” amesema Maria.

Amesema; "Mazishi ya mtoto wake yalikuwa ya uchungu sana, kulikuwa hakuna kuimba, kusali hata Rozari ya Huruma na leo hii mama naye kafariki. Hatuna la kusema, kazi ya Mungu haina makosa," amesema Maria.