Mambo 10 kuhusu mfumuko wa bei

Muktasari:

  • Uchambuzi wa Mwananchi chini ya mafunzo ya mwelekeo wa uchumi wa Taifa na hali ya mfumuko wa bei chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), unaonyesha maeneo 10 yanayoweza kukusaidia kutambua au kufanya uamuzi katika shughuli zako kiuchumi.

Dar es Salaam. Huenda umekuwa ukiumiza kichwa ni namna gani mfumuko wa bei unavyohusisha thamani ya shilingi yako na mabadiliko ya bei ya bidhaa na huduma mbalimbali nchini.
Uchambuzi wa Mwananchi chini ya mafunzo ya mwelekeo wa uchumi wa Taifa na hali ya mfumuko wa bei chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) yaliyotolewa wiki iliyopita, unaonyesha maeneo 10 ya msingi yanayoweza kukusaidia kutambua au kufanya uamuzi katika shughuli zako kiuchumi.
Kwanza kabisa, mfumuko wa bei ni ongezeko la jumla la bei za bidhaa na huduma kwa kipindi fulani ili kuonyesha ni kwa kiwango gani bei zimebadilika kipindi kimoja ukilinganisha na kingine kwa ukokotozi wa kila mwezi hadi mwaka. Huzingatia tabia ya vipindi vinavyofanana. Mfano Julai 2021- Julai 2022.
Pili, NBS hukusanya taarifa ya bei ya bidhaa 383 katika mikoa yote nchini kwa kutumia utafiti wa kisayansi wa kitakwimu katika sampuli ya kaya husika zinazotoa taarifa ya manunuzi kila mwezi. Bidhaa 132 ni vyakula na vinywaji baridi na bidhaa 251 bidhaa zisizokuwa za vyakula.
Tatu, ukokotozi wa bei hizo hufanyika kwa kuangalia wastani wa bei ya bidhaa moja moja na kwa ujumla katika bidhaa hizo 383 chini ya makundi 13 yanayopimwa kwa makadirio ya asilimia.
Nne, mfumuko wa bei unatakiwa kuwa chini ya asilimia kumi kwa kadiri ya malengo ya kisera ya mfumuko wa bei ya nchi lakini lengo la kisera ni kuwa na mfumuko wa bei usiozidi asilimia tano.
Tano, bei za bidhaa zinaweza kupanda lakini kasi ya upandaji wa bidhaa hizo ukaonekana kupungua. Bei zitashuka tu endapo mfumuko wa bei utaonekana kuwa hasi.
Sita, sio kila mfumuko wa bei ni hatari katika uchumi wa Taifa, kiwango kisizidi cha asilimia tano kwa kuwa unasaidia pia kuchochea uwekezaji wenye faida katika uzalishaji wa bidhaa. Mfumuko wa bei ukishuka ni kicheko kwa mnunuzi lakini inadhoofisha ukuaji wa faida kwenye uzalishaji.
Saba, mwenendo wa bidhaa za vyakula na vinywaji ndio kundi linaloathiri kwa kiwango kikubwa ongezeko la jumla la bei za bidhaa na huduma kwa kipindi fulani.
Nane, msingi wa ukokotozi wa bei hizo unatokana na utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi (HBS) na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa anasema wanatarajia kufanya marejeo ya mfumo wa ukokotozi wa fahilisi za bei za bidhaa na huduma mbalimbali mwaka 2024 ili kuakisi hali halisi.
Naye Kaimu Meneja wa takwimu za ajira na bei wa NBS, James Mbongo anasema;
“Tunafanya baada ya kukamilisha utafiti wa HBS Mwaka 2023/24 ndio tutaanza kufanya marejeo hayo, ni muhimu kwani kuna mabadiliko mengi sana hapa kati yametokea kiteknolojia na maisha.”
Tisa, athari katika huduma za umeme, maji, miundombinu, uchukuzi na usafirishaji huathiri uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma pamoja na kiwango kikubwa cha fedha katika mzunguko husababisha mfumuko wa bei kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma.
Kumi, kila ukokotozi wa taarifa za bei huzingatia hali ya masoko tofauti, maeneo tofauti na vipato tofauti vya sampuli inayohojiwa katika kaya zilizotambuliwa.