Mambo 10 yanayomtofautisha Magufuli na watangulizi wake

Mambo 10 yanayomtofautisha Magufuli na watangulizi wake

Muktasari:

  • Bidii ya kufuatilia mambo na uwezo wa kujua vitu vingi ni miongoni mwa sifa nyingi za Rais John Magufuli, zinazomtofautisha na wengine.

Bidii ya kufuatilia mambo na uwezo wa kujua vitu vingi ni miongoni mwa sifa nyingi za Rais John Magufuli, zinazomtofautisha na wengine.

Rais Magufuli, ambaye kifo chake kilitangazwa Machi 17, mwaka huu, hivyo nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa makamu wake, Samia Suluhu Hassan, kipindi cha uongozi wake aliongoza kwa kuwasahihisha watendaji wa Serikali.

Kwa mujibu wa tathmini ya uongozi wa Rais Magufuli uliodumu kwa miaka mitano na siku 132, ni dhahiri watendaji wa Serikali na hata makandarasi walipata wakati mgumu kufanya kazi na Serikali chini ya Magufuli kuliko kipindi chochote kile kilichotangulia.

Mwaka jana, Rais Samia wakati huo akiwa Makamu wa Rais, alisema ni vigumu mno kumdanganya Magufuli. “Ukiona Magufuli anakuuliza kitu, ujue anazo taarifa zote. Ni mfuatiliaji sana,” alisema Samia alipokuwa kwenye mahojiano na chombo kimoja cha habari.

Amos Makalla ni mweka hazina wa zamani wa CCM, alipata kuwa Naibu Waziri wa Maji, pia Habari, Utamaduni na Michezo, kisha akahudumia mikoa ya Kilimanjaro, Mbeya na Katavi kwa nafasi ya Ukuu wa Mkoa.

Makalla amesema alifanya kazi na Rais Jakaya Kikwete na Magufuli kwa nyakati tofauti.

Alisema Rais Magufuli alikuwa na taarifa nyingi za Serikali, kiasi alipotembelea miradi ilibidi wakandarasi na watendaji wa Serikali wanaohusika na usimamizi wajipange kwelikweli.

“Magufuli akikuuliza kitu, ukitoa jibu la uongo utakwenda na maji, maana alikuwa na majibu yote,” alisema Makalla na kuongoza: “Alikuwa mfuatiliaji na alikuwa na uwezo mkubwa wa kutunza majibu kichwani.”

Hoja hiyo ya Makalla unaweza kuijaza zaidi kutokana na wasifu wa kitaaluma wa Magufuli kuwa ni msomi wa sayansi na hisabati, hivyo haikuwa rahisi kudanganywa mambo ya hesabu na vipimo.

Ushahidi wa hilo, mojawapo ni Julai mwaka jana, alipokuwa anazindua nyumba za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Magufuli alikataa vipimo vya mkandarasi wa nyumba hizo na akasema; “hapa tumeliwa.”

Upande mwingine, Makalla anamuelezea Magufuli kama kiongozi wa matokeo. Alisema kipindi akifanya kazi chini yake, aligundua kuwa unaweza kufanya mengi lakini kama kuna matokeo aliyataka lakini hukutimiza, huwezi kupona.

“Nilifanya kazi na Rais Magufuli nikiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na baadaye Katavi. Nilipokuwa Katavi, alinipigia simu, akaniambia nilifanya vizuri katika kusikiliza kero za wananchi, alinipongeza kwa kutatua kero za watu.

“Alinipongeza kwa ufuatiliaji wa miradi na kuwezesha Katavi kupiga hatua kimaendeleo na mkoa kuzalisha chakula kwa wingi. Hata hivyo, aliniambia sikufanya vizuri katika ugawaji wa vitambulisho vya wamachinga. Akaniondoa. Ni kwa sababu alitaka matokeo,” alisema Makalla.

Kwa kauli hiyo, ni sahihi kuwa jambo la pili ambalo Rais Magufuli alijitofautisha na watangulizi wake ni namna alivyoshughulikia suala la wamachinga, kwa kurasimisha uwepo wao, pia alivyotaka matokeo haraka bila kupindapinda.

Kuhusu wamachinga, Rais Kikwete katika muhula wake wa kwanza aliwajengea Machinga Complex, Karume, Ilala, Dar es Salaam ili kuwapa eneo rasmi la kufanyia kazi zao, wakati kipindi cha marais wengine, hakuna alama yoyote waliyoiacha ya wamachinga.

Upande wa kutaka matokeo ya haraka mfano upo kwa Mbunge wa Same Mashariki, Anne Malecela, aliyeondolewa kwenye nafasi ya ukuu wa mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha takriban mwezi mmoja tangu alipoteuliwa. Magufuli alimwondoa Kilango kwa kosa la kusema mkoani kwake hakukuwa na watumishi hewa.

Machi 15, 2016, Magufuli alipowaapisha wakuu wa mikoa, aliwaagiza waende kumaliza watumishi hewa kwenye mikoa yao.

Aprili 11, 2016, yaani siku 27 tangu Kilango alipoapishwa, alitenguliwa. Rais Magufuli alisema yeye alikuwa na taarifa za kutosha za uwepo watumishi hewa. Kutenguliwa kwa Kilango ni majibu mawili kwa mpigo, kwanza ni kutaka matokeo ya haraka, pili alikuwa na taarifa za kutosha hivyo, sio rahisi kumdanganya.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai amesema kwa upande wake, jambo chanya la pekee analoweza kumtofautisha Rais Magufuli na waliomtangulia ni alivyowafanya watu wachape kazi hasa watumishi wa umma.

“Watu walikuwa wavivu. Magufuli amesababisha watu watambue kuwa kufanya kazi ndiyo silaha pekee ya maisha,” alisema Mungai.

Alisisitiza kuwa kipindi cha marais kabla ya Magufuli, hakukuwa na msisitizo wa watu kufanya kazi. Kitendo cha kufanikiwa kuihamishia Serikali Dodoma, kimempambanua kuwa alitenda na kufanikisha alichokusudia kuliko watangulizi wake.

Mpango wa kuihamishia Serikali ulidumu kwa miaka 40 bila kukamilika mpaka Magufuli alipoingia madarakani.

La Dodoma ni la nne. Tano ni alivyoteua mawaziri wake. Wakati marais waliomtangulia waliamini kuteua wanasiasa, Rais Magufuli aliwapa nafasi wataalamu kuongoza wizara.

Profesa Joyce Ndalichako, Dk Phillip Mpango, Dorothy Gwajima, Geoffrey Mwambe na wengine, ni mfano wa wataalamu waliopewa nafasi. Jambo la sita ni namna alivyoweka nguvu katika makusanyo ya madeni ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Wakati awali ilionekana mnufaika wa mkopo wa elimu ya juu ni hiari yake kulipa, lakini Magufuli aligeuza kibao na kuwa deni ambalo lazima lilipwe.

Saba, ni mtazamo wake kuhusu nje. Tofauti na marais wengine, Magufuli alivuta pumzi ya mwisho bila kuvuka Bara la Afrika, wakati nane ni vile alivyoamini katika sheria kali na hatua kali katika kukabiliana na wawekezaji na wafanyabiashara, tofauti na wenzake ambao walifanya maridhiano.

Uamuzi wa Mungu kumchukua Rais Magufuli akiwa ameshaongoza nchi kwa miaka mitano na siku 132, unaweka alama ya kuwa Rais wa kwanza tangu mfumo wa vyama vingi uanze, kuongoza na kuondoka bila kufanya maridhiano na wanasiasa wa vyama vya upinzani.

Kuhusu maridhiano, unaweza kuongeza kuwa chini ya uongozi wa Rais Magufuli, wanasiasa wengi zaidi wa upinzani walikamatwa, wakachukuliwa hatua mbalimbali, kama kifungo, kulipa faini na kadhalika. Hii ni tofauti kubwa na watangulizi wake.

Ununuzi wa ndege na ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (MW 2115) ni mambo yaliyoacha alama, jumlisha miradi mingi iliyotekelezwa maeneo mbalimbali nchini ambayo ni alama kubwa.

Lakini jambo la 10 la tofauti mno ni jinsi alivyofanya kazi na mawaziri wake.

Marais waliomtangulia, mtindo wao wa uongozi ulikuwa kutoa uhuru kwa mawaziri ili wajitanue watakavyo, lakini Rais Magufuli yeye aliwafuatilia mawaziri wake kwa ukaribu, kiasi kwamba ilikuwa rahisi kumuona yeye (Magufuli), aking’ara kuliko mawaziri wake.