Mambo ya kufanya kabla na baada ya kupata chanjo ya corona

Mambo ya kufanya kabla na baada ya kupata chanjo ya corona

Muktasari:

  • Wakati dunia imekuwa ikihangaika kutafuta namna ya kuwanusuru watu dhidi ya janga la virusi vya corona lililoibuka mwishoni mwa mwaka 2019, ikiwemo kuwapatia chanjo, mawazo ya wengine yamekuwa juu ya usalama wa chanjo zenyewe.

Wakati dunia imekuwa ikihangaika kutafuta namna ya kuwanusuru watu dhidi ya janga la virusi vya corona lililoibuka mwishoni mwa mwaka 2019, ikiwemo kuwapatia chanjo, mawazo ya wengine yamekuwa juu ya usalama wa chanjo zenyewe.

Chanjo hizo ambazo zimetengenezwa katika mataifa mbalimbali duniani na kupewa majina tofauti, tayari zimegunduliwa na hivi sasa zinatumika kuwakinga watu na athari za ya virusi hivyo.

Tanzania licha ya awali kusita kuingiza chanjo hizo, kwa sasa ni miongoni mwa nchi ambazo tayari zimeingiza chanjo ya corona kwa ajili ya kuanza kuwachanja watu wake, hasa kwa makundi yaliyopewa kipaumbele.

Hiyo ni baada ya kupokea awamu ya kwanza ya msaada wa dozi 1,058,400 za chanjo dhidi ya virusi vya corona kupitia mpango wa Covax facility kutoka Marekani na nyingine zikiwa zimepokewa upande wa Zanzibar.


Chanjo yenyewe

Chanjo iliyoingia nchini aina ya Johnson& Johnson imetengenezwa na Janssen Vaccines, Leiden, Netherlands, Belgian parent company Janssen Pharmaceuticals, subsidiary of American company Johnson & Johnson na huchomwa mara moja kwa mhusika.

Rais Samia Suluhu Hassan ameshazindua utoaji wa chanjo hiyo nchini Julai 28 ambapo pia alichanjwa yeye pamoja na viongozi wengine.

Kabla na baada ya kuwasili kwa chanjo hiyo nchini, watu wamekuwa na hisia tofauti, huku baadhi wakieleza kutokuwa tayari kuchanja kutokana na kile wanachodai kuwa “hata ukichanjwa unapata maambukizi.”

Ukweli ni kuwa mtu aliyepata chanjo na ambaye hajapata; pale wanapopata maambukizi ya ugonjwa huo, hali huwa tofauti, kwa kuwa aliyechanjwa haugui sana.


Kabla ya kuchanjwa

Kulingana na utaratibu uliweka hapa nchini, kabla ya mtu hajapatiwa chanjo atatakiwa kujaza fomu maalumu ya kukubali kupata chanjo hiyo na baada ya hapo huchanjwa.

Pia mhusika hutakiwa kuwa na kitambulisho kimojawapo kati ya kile ya taifa, cha mpiga kura au leseni ya udereva kwa kuwa waliochanjwa wanaingizwa kwenye kanzidata.

Mkurugenzi wa kuratibu na kukuza utafiti kutoka Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu, (NIMR) Dk Paul Kazyoba alisema kabla ya chanjo, ni muhimu mwili ukawa na sawa na wenye nguvu za kutosha. “Muda huo unaingiza kitu kipya mwilini, unaposhtuka na kuanza kupata uchovu na maudhi pale ndiyo unazalisha seli kinga kuuandaa mwili, ili adui akijaribu kuingia akutane na kinga muda huo. Mhusika akiona maudhi yanazidi amtafute daktari ingawa wanaopata hali hiyo ni wachache,” alisema


Baada ya kuchanjwa

Baada ya kuchanjwa mhusika hupewa kadi inayoonyesha kuwa umeshapatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Baada ya mtu kupata chanjo miongoni mwa mambo ya kuzingatia yanayosisitizwa ni kutopata kilevi cha aina yoyote kwa saa 72 sawa na siku tatu.

Hiyo inatokana na kwamba pombe na dawa ya chanjo vyote vinakwenda kwenye ini, hivyo upo uwezekano wa ini kuongezewa mzigo na kulichosha.

Kwa mujibu wa Dk Isack Maro, “Chanjo inapoingia mwilini inatakiwa ifanye kazi na ini lina kazi ya kuipokea na kuichuja endapo kutakuwa na madhara.
“Sasa kama dawa itaingia kwenye ini na pombe nayo ikaingia, kuna uwezekano wa ini kuchoka na hata sumu nyingine zikapita bila kuchujwa,” alisema.

Pia mtu anayetumia dawa kali zinazosababisha damu iwe nyepesi, naye anashauriwa asitishe kwa siku mbili au tatu baada ya kuchanja.

Naye Dk Paul Kazyoba alsema baada ya kuchanjamtu hatakiwi kutumia kilevi chochote, kwani kitaingilia mfumo wa uzalishaji wa kinga za mwili ambao unafanywa na chanjo kwa saa za mwanzo.

Dk Kazyoba alisema chanjo inapochomwa mwilini, ikiingia inaenda kuzisisimua seli za kinga ‘antibodies’ na zinazalishwa na zikishajaa mwilini zinakuwa askari wa kupambana na kirusi kitakachoingia.

“Kuufanya mwili uzalishe hizi seli kinga, inatakiwa usiingiliwe na kitu chochote cha tofauti kwenye damu kwa saa 72. Kilevi cha aina yoyote kwa maana ya pombe, bangi, shisha au dawa za kulevya lazima kitaingilia mfumo na hivyo kuifanya chanjo kutofanya kazi yake vizuri.

“Ndani ya saa 72 ni muda ambao kazi kubwa inafanyika, ndiyo maana maudhi madogo madogo mtu anayapata ndani ya muda huo, vilevi vitaathiri uzalishaji wa mwanzo wa seli za kinga, ambazo zitajitengeneza mwilini mwako kwa miezi kadhaa,” alisema Dk Kazyoba.

Kati ya mambo ya kuzingatia baada ya kuchoma chanjo, inatakiwa mtu aushughulishe mwili kwa kipindi cha saa 72 za awali kwani kwa kufanya hivyo seli za kinga huzalishwa kwa wingi na huwa na manufaa zaidi tofauti na kinyume chake.


Athari (maudhi) za chanjo

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, baada ya mtu kuchanjwa anaweza kupata athari (maudhi) ndogo kama kuhisi kichefuchefu, kichwa kuuma, kupata uchovu kidogo na homa kwa mbali.

Mtaalamu wa macrobaiolojia kutoka Chuo Kiku cha Afya Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk Mtebe Majigo alisema mtu anapopewa chanjo yoyote anaweza kupata maudhi madogo madogo kama homa, ingawa si wote.

“Wakati mwili unapozalisha vichocheo vyake ambavyo ndiyo vitakuwa kinga ya mwili, vichocheo vingine ndiyo vinasababisha homa kutokea. Vinavyotoka ndiyo vinapeleka taarifa kwenye ubongo na vinarudi kama homa, hii ni baada ya mwili kushtuka kutokana na kilichoingia, lakini hali hii inatofautiana kati ya mtu na mtu,” alisema Dk Majigo.

Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tigest Mengestu alipozungumza siku ya kupokea awamu ya kwanza ya chanjo zilizoletwa nchini, alisema kupata chanjo ni miongoni mwa njia za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, lakini haiondoi au kuweka ukomo wa matumizi ya njia nyingine za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

“Kunawa mikono, kuvaa barakoa, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kutumia vitakasa mikono ni vitu ambavyo vinapaswa kuendelea kufanyika katika jamii yetu hata baada ya kupata chanjo,” alisema. Hiyo ni kwa sababu chanjo ni kama moja ya njia inayoweza kutumika kupunguza maambukizi ya virusi hivyo, lakini haiweki ukomo wa njia nyingine zinazotumika.

Lakini kutokana na watu kuwa na wasiwasi juu ya ubora wa chanjo iliyoletwa nchini, Waziri wa Afya, Dk Gwajima alisema ujio wa chanjo umefuata taratibu zote ambazo Serikali imekuwa ikitumia kujiridhisha juu ya bidhaa zote za afya zinazoingizwa nchini.

“Chanjo hii ni salama, imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ambayo huthibitisha chanjo zote, kisha sisi pia Tanzania tukathibitisha kupitia vyombo vyetu vya ndani kwa utaratibu uleule wa kuthibitisha chanjo nyingine zote zinazotoka nje ya nchi.

“Kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa kupokea, kuhakiki, kutunza na kusambaza chanjo mbalimbali, chanjo hizi zitaanza kutolewa hivi karibuni baada ya taratibu zote kufanyika kama ambavyo zimekuwa zikufanyika kwa bidhaa nyingine zote za afya,” alisema Dk Gwajima.

Alisema chanjo hizo zitakuwa zikitolewa katika vituo vyote vya afya nchini na pia vitaanzishwa vituo maalumu kwa ajili ya kurahisisha ufikiwaji wa huduma.

Pia chanjo itatolewa kwa mujibu wa miongozo na kwa kuanzia Watazingatia makundi ya vipaumbele yaliyowekwa na Serikali. “Watumishi wa afya, watu wazima wanaoanzia miaka 50 na kuendelea na watu wenye magonjwa sugu katika mikoa mbalimbali kama vile Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, Kigoma, Singida, Dodoma, Iringa na Mtwara,” alisema Gwajima.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Yunus Mgaya alisema usalama wa chanjo dhidi ya Covid-19 ni asilimia 99.9 na akawataka wananchi kuondokana na hofu.

“WHO haipitishi dawa kirahisi, ina kamati zake na imethibitisha chanjo zote aina sita ni salama na hapa Tanzania pia chanjo hizo zinahakikiwa kitaifa na taasisi zinazoshughulika na masuala ya afya.

“Sina wasiwasi na hii chanjo, na ikianza kutolewa mimi nitakuwa kati ya watu watano wa mwanzo,” alisema mtaalamu huyo.

Akizungumzia suala la mtu anayechanjwa kutakiwa kujaza fomu, jambo ambalo baadhi ya watu wanadai ni Serikali kutaka kujitoa endapo anayechanjwa atapata athari, Profesa Mgaya alisema hilo halina ukweli, kwani ni kawaida katika masuala ya matibabu kwani hata hospitali mtu anapofanyiwa operesheni huwa anajaza fomu maalumu.

(Taarifa ya ngongeza na Elizaeth Edward na Herieth Makwetta)