Mambo ya kuzingatia kwenye uhusiano

Utakubaliana na mimi kwamba wengi wetu tunapitia changamoto nyingi sana katika ndoa au mahusiano yetu. Wengine hawapendi hali wanazozipitia lakini hawajui kwa nini wanapitia hali hizo, wakati wako ambao wanajua shida ilipo ila hawajui namna ya kuchomoka hapo, na hii inaongeza msongo wa mawazo kwao.

Ukweli ni kwamba yapo mambo muhimu ya kuzingatia ambayo walioko kwenye uhusiano wengi hawayajui na wengine wanayajua baadhi, lakini hawayatendei kazi na hivyo misuguano na kutofautiana kunazidi.

Hapa nakuletea mambo hayo, nikijaribu kuyaelezea kwa kifupi ili kukusaidia kuyaelewa na ikibidi kuyaweka kwenye utendaji. Ni kiu yangu na maombi yangu kwamba kila anayesoma makala hii aweze kuyaboresha na kuyafurahia mahusiano yake.
 

Jambo la 1

Sababu moja kubwa inayochangia watu wengi kushindwa kuyaona mabadiliko wanayoyatamani kutoka kwa wapenzi wao ni kwamba wanaanza vibaya safari ya kuonyesha uhitaji au kiu yao kwa wapenzi wao. Kama ilivyo katika safari yoyote, ukianza vibaya kuna uwezekano wa kuendelea na kumaliza vibaya.

Najua una kiu kwamba mpenzi wako abadilike, kuna vitu vingi unatamani kuviona vikifanywa tofauti na vile anavyovifanya sasa, ukweli ni kwamba kama ukikosea namna ya kuanza mchakato wa kuyatafuta mabadiliko hayo basi utaharibu kila kitu.

Wataalamu wa uhusiano wanashauri kwamba kabla hujaelezea yale unayotaka mpenzi wako abadilike au yale usiyoyapenda kwake, ni vema ukajiangalia upande wako kwanza na kuona kama yapo ambayo mpenzi wako anayalalamikia kwako, yale asiyoyapenda kwako na ujitahidi kuyabadili hayo kwanza, hapo unakuwa umemuandaa vema kupokea wito wa yeye kubadilika katika yale unayotamani ayabadilishe.

Kwa kumsukuma na kumlazimisha abadilike wakati bado anaona yapo ambayo na yeye anataka ubadilike na haoni ukibadilika kunafanya ugumu sana wa yeye kubadilika. Amua kuanza vizuri, utaona matunda ya kiu yako.
 

Jambo la 2

Utakubaliana na mimi kwamba wengi wetu tumekuwa tukiishi kwenye mtazamo wa “nitabadilika kama yeye atabadilika”, “akiamua kubadilika kwenye hiki basi na mimi nitabadilika kwenye kile”.

Tuwe wakweli katika hili, ukweli ni kwamba dhana hii kwa muda mrefu haijafanikiwa hata kidogo. Mabadiliko na mashindano ya kulinganishana katika kubadilika mara nyingi hayafanyi kazi. Amua kubadilisha mtazamo kwa kutafuta kubadilika wewe kwanza.
 

Jambo la 3

Unaweza kufanikiwa kuyafunika maovu na machafu yako ambayo mpenzi wako hayafahamu, lakini ukweli ni kwamba hali hii wakati wote haitakupa uhuru wa ndani.

Mara nyingine unaweza kujihisi kushitakiwa au kuhukumiwa “guilty conscious” na hii sio hali njema pia, lakini kama utaamua kukiri makosa yako kwa uwazi mbele ya mpenzi wako itakuweka huru na kukufungua kutoka kifungo cha utumwa wa uovu na hilo litapanua uwezekano wa kuleta mabadiliko makubwa kwako na kwa mpenzi wako, mabadiliko ambayo mmekuwa mkiyatamani kuyaona yakitokea katika mahusiano yenu.


Jambo la 4

Najua kuwa wengi wetu ni watu wa imani kutokana na dini au dhehebu lako. Mara nyingi unapojikuta umefanya kosa au kumtendea madhambi mpenzi wako, unahisi vibaya na unakimbilia kuomba Mungu akusamehe.

Hili ni jambo jema, lakini kwenye uhusiano wa kweli, jambo hili linahitaji hatua moja zaidi. Siyo tu unamalizia kwa kumwambia Mungu akusamehe kwa kile ulichokifanya kinachoweza kuathiri uhusiano wenu lakini pia unakiri makosa na kuomba radhi kwa mpenzi wako ambaye jambo hilo lingeweza kumuathiri au labda limemuathiri tayari.

Ni vema kusahihisha mambo na Muumba wetu, lakini pia tunapokuwa kwenye uhusiano tunatakiwa kusahihisha kwa uwazi, kwa ukweli na kwa kumaanisha kwa wapenzi wetu pia.
 

Jambo la 5

Ni kweli kabisa mara nyingine makosa tuliyoyafanya kwa wapenzi wetu hayawezi kufutika hata tunapokiri kosa na kuomba msamaha. Hatukiri makosa yetu ya awali na kuomba radhi kwa nia ya kuyafuta kabisa makosa hayo, kufutika haiwezekani na mara nyingine hata athari za yale tuliyoyafanya zinaweza kuendelea kuwepo.

Ukweli ni kwamba kwa kukiri na kukubali kuwa tulihusika na makosa yale na kwamba ndani yako unajisikia kukosa na haufurahii kabisa ulichokifanya na unajutia jinsi ulivyomuumiza mwenzako, hii inakupa uhalali wa kuomba radhi na kusamehewa na pia inakuweka katika nafasi ya kuanza vema safari ya kutafuta mabadiliko unayoyatamani kwa mpenzi wako.
 

Jambo la 6

Kati ya lugha za mapenzi yenye kuleta ufanisi, lugha ambayo unaweza kuizungumza kwa mpenzi wako na kuyaona matunda yake kwa haraka ni pamoja na kuzungumza maneno ya kumtia moyo, maneno ya kumfariji, maneno ya kumpongeza.

Jiulize lini umemwambia amependeza? Lini umemwambia amefanya vizuri? Lini umemwambia kuwa unajisifu sana kwa kuwa naye? Lini umemwambia kuwa yeye ni wa muhimu sana kwenye maisha yako? Lini umemwambia machoni kwake unampenda?

Nimewahi kumuuliza mwanandoa mmoja aliyekuja ofisini kwangu swali hili, lini umemwambia mke wako unampenda? Akanijibu kuwa anadhani alivyomwambia siku wanaoana inatosha kuthibitisha penzi lake kwa mkewe, nikamwambia hiyo haitoshi kabisa.

Hii ni sawa na wewe ukiwa kazini halafu ukifanya kitu vizuri na kutazamia bosi wako atakwambia “hongera umefanya vema”, tofauti na matarajio yako bosi anakwambia kuwa siku ile ulipofanya vizuri (labda mwaka juzi) nilikupongeza na hiyo inatosha kabisa kufidia mazuri yote utakayoyafanya, ukweli ni kwamba hilo litakufedhehesha sana.

Vivyo hivyo kwa mpenzi wako. Fahamu kwamba lugha ya kutia moyo, kusifia na kupongeza huiinua nafsi ya mpenzi wako, huhuisha vilivyokufa ndani yake wakati lugha za malalamiko, lawama, kejeli au matusi hukatisha tamaa na kuua kabisa vilivyoko moyoni mwake.

Itaendelea