Mamia wamlilia Teddy Mapunda

Mamia wamlilia Teddy Mapunda

Muktasari:

  • Aligusa maisha ya wengi. Ndivyo unavyoweza kusema kuhusu kifo cha mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni ya Montage, Teddy Mapunda kutokana na watu wa kada mbalimbali kumlilia wakieleza jinsi alivyogusa maisha yao.


Dar es Salaam. Aligusa maisha ya wengi. Ndivyo unavyoweza kusema kuhusu kifo cha mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni ya Montage, Teddy Mapunda kutokana na watu wa kada mbalimbali kumlilia wakieleza jinsi alivyogusa maisha yao.

Teddy alifariki dunia jana usiku Jumanne Mei 4, 2021 baada ya kujisikia vibaya akiwa na rafiki zake katika hoteli ya Serena mkoani Dar es Salaam. Kwa mujibu wa rafiki zake wa karibu, alikimbizwa katika hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya matibabu lakini baadaye ilielezwa kuwa amefariki dunia.

Mkurugenzi wa TVE na redio EFM, Francis Ciza maarufu Majizzo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram amesema kifo cha Teddy ni msiba mkubwa kwake.

“Jambo moja limenitafakarisha sana, tangu nifunge ndoa ‘DP’ yangu ya WhatsApp ilikuwa ni picha yangu ya harusi. Ni juzi tu nikaamua kuibadilisha (wenye namba yangu wanajua) nikamuweka dada yangu Teddy.”

“Juzi Jumatatu Teddy aliniuliza kwa nini nimemuweka, yaani nimeondoa picha ya mke wangu nikamuweka yeye. Akauliza “au nakufa..., tukacheka kwa utani. Leo naambiwa ameondoka, kwa ufupi nimepoteza dada, rafiki na mshirika mwingine wa kweli katika kazi, Pumzika kwa amani dada yangu hadi tutakapoonana tena,” amesema Majizzo.

Haji Manara ambaye ni msemaji wa klabu ya Simba amesema familia yake imempoteza dada mkubwa.

“Ni mwanachama mwenzetu kwenye kamati mbalimbali za timu za Taifa na binafsi nina ukaribu naye sana wa kikazi kwa miaka mingi kidogo, naungana na wote kuitakia familia yake pole na subira nyingi kwao huku tukimuombea dada yetu pumziko jema, Bwana alitoa na Bwana alitwaa, jina lake lihimidiwe,” amesema Manara.