Mamia wawazika ndugu waliouawa, wapinga madai ya mgogoro wa fedha
Muktasari:
- Mamia walihudhuria mazishi ya Hamza na Ally Omary waliouawa Mwananyamala, ndugu na marafiki wamekanusha madai kuwa chanzo ni pesa zilizokuwa zinatumwa na mtuhumiwa wa mauaji kutoka Afrika Kusini, wakisema mtuhumiwa alikuwa na msongo wa mawazo.
Dar es Salaam. Mamia ya waombolezaji wamejitokeza eneo la Mwananyamala Kisiwani, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam kushiriki mazishi ya ndugu wawili wanaodaiwa kuuawa kikatili na mtoto wao Hosamu Hamza, maarufu Maopena.
Ndugu hao ambao ni Ally Omary, maarufu Bob na Hamza Omary, maarufu King wanadaiwa kuuwawa na Hamza kwa kitu chenye ncha kali usiku wa kuamkia Julai 17, 2026 kisha kuwafukia mbele ya nyumba yao.
Miili hiyo imezikwa leo Jumapili, Julai 19, 2026, makaburi ya Ndugumbi yaliyopo Magomeni, jijini Dar es Salaam.
Julai 18, 2026, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ilitoa taarifa ya kushikiliwa kwa Maopena akituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.
Polisi ilieleza mtuhumiwa alikamatwa Julai 17 saa 9 alasiri katika eneo la Makongo akiwa na kisu kilichokuwa na madoa ya damu huku mavazi aliyokuwa amevaa pia yakiwa na alama za damu.
Baada ya tukio hilo, kumekuwa na minong'ono kuwa chanzo cha mauaji hayo ni nyumba ambayo Hosamu alikuwa anamtumia baba yake pesa alipokuwa Afrika Kusini alikopelekwa na mjomba wake.
Majeneza ya Ally Omary maarufu Bob na Hamza Omary yakitolewa katika msikiti wa Kidile uliopo Mwananyamala Kisiwani , Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam kuelekea makabur ya Ndugumbi yaliyopo Magomeni kwa ajili ya mazishi
Hata hivyo, tetesi hizo zimekanushwa na ndugu pamoja na marafiki wa Hamza kutokana na mazingira aliyokuwa akiishi tangu mwanawe akiwa nje ya nchi hadi aliporudishwa nchini Julai 2025.
Akizungumza na Mwananchi Julai 19, 2026 Haji Mpangachuma, rafiki wa marehemu Hamza baba mzazi wa Hosam, amesema tangu amemfahamu marehemu hajawahi kumuona amebadilika hivyo tetesi za kijana huyo kutuma pesa hazina ukweli.
Amesema Hamza alikuwa akifanya kazi ya kukusanya na kuchambua makopo ya plastiki akishirikiana na mtu mwingine aliyemtaja kwa jina la Kibugu hivyo angekuwa anatumiwa pesa asingeishi maisha hayo.
"Tatizo la vijana wetu wakishakwenda Afrika Kusini wakirudi wakiona wamepotea kimaisha wanatengeneza chuki kwa wazazi, muda mrefu King anauza makopo ya plastiki na rafiki yake na mara kadhaa amekuwa akihangaishana na mtoto wake akikamatwa anakwenda kumtoa," amedai Mpangachuma.
Dada wa marehemu hao, Husna Omary amesema habari zinazosambazwa mtandaoni za chanzo cha mauaji hayo ni utumaji wa pesa si za kweli kwa kuwa wao wanajua ukweli wa maisha ya kaka yao.
"Watu wameamua kuzusha huko kwamba Hosamu alikuwa anamtumia pesa baba yake ajenge nyumba si za kweli, kaka yetu hakuwahi kula pesa ya mtoto wake hata alipoongea naye na kumuomba pesa alimjibu vibaya na mwisho wa siku aliamua kuachana naye hadi aliporudishwa nchini," amesema Husna.
Amesema mara kadhaa Hosamu amekuwa akimtishia baba yake hata kufikia hatua ya kusema anamfuatilia maisha yake jambo ambalo halipendi.
Mohamed Kombo, rafiki wa mtuhumiwa amesema kilichotokea ni msongo wa mawazo ya rafiki yao baada ya kutoka Afrika Kusini na kuona maisha yake hayabadiliki akaamua kutoa uhai wa wazazi wake na sio utumaji wa pesa.
"Tunashinda naye maskani dogo kila akikaa analalamika haelewi maisha yake yanavyokwenda si mara moja amekuwa akisema ipo siku atatoa uhai wa mtu lakini hatukujua ni nani, mara kadhaa amepelekwa polisi na baba yake ndiye anayemtoa kwa dhamani wakati mwingine anakuja mama yake kumtoa hapo ni akili ilishachoka kuwaza," amesema Kombo.
Sheikh Salim Muhidin wa Mwananyamala, amesema wazazi wasikubali kuendeshwa na mihemko ya watoto kwa kutaka maisha ya nje bila kujua uhalisia wa sehemu wanakokwenda.
"Wazazi kwa kiasi kikubwa tumeanza kujisahau kwenye malezi ndiyo maana tunaona kumekuwa na matukio ya mauaji ya watoto kwa wazazi kwa kiasi kikubwa kwa sababu hakuna maadili na woga na hivyo kila jambo linalofanyika tunaona la kawaida katika jamii," amesema Sheikh Muhidin.
Amesema sasa ni wa kati wa kumrudia Mungu na kuomba toba kwa wazazi wote ili kulinda kuzazi kijacho wasije kuona kuuana ni jambo la kawaida kwa binadamu na mbele ya Mungu.