Mamlaka Mkoa wa Pwani zatakiwa kuboresha barabara

Muktasari:

  • Mamlaka za Mkoa wa Pwani zimetakiwa kuwa na mipango ya muda mfupi ya ujenzi na ukarabati wa barabara zake kwa manufaa ya wananchi na mamlaka hizo husika.

  

Pwani. Mamlaka za Mkoa wa Pwani zimetakiwa kuwa na mipango ya muda mfupi ya ujenzi na ukarabati wa barabara zake kwa manufaa ya wananchi na mamlaka hizo husika.

Akichangia hoja kwenye kikao cha Bodi ya Barabara ya mkoa huo leo Novemba 25, Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka amesema kumekuwa na msongamano mkubwa wa magari kwenye barabara kuu ya Dar salaam- Morogoro unaochangiwa na ubovu wa barabara ya zamani ya Picha ya Ndege -Visiga hadi Mlandizi.

"Nashukuru Serikali mradi mkubwa wa njia nane umekuja mpaka Kibaha lakini kimsingi ukiuangalia magari yote yakifika yanasongamana hapa.

“Kwa hiyo pamoja na mikakati ya Serikali ya kuendeleza njia nane kuanzia Kibaha mpaka Chalinze, tunayo pia barabara ya zamani ambapo ukiingia Picha ya Ndege inakwenda hadi Visiga na kuendelea hadi Mlandizi Kibaha vijijini tuifanyie kazi ipunguze adha hii," amesema Koka.

Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Mafia, Juma Ally amesema ratiba ya sasa hivi ya usafiri wa majini kwa kutumia boti ya MV Kilindoni kutoka Nyamisati hadi Mafia si rafiki, kwani hakuna ratiba maalumu ya muda wala siku, bali hutegemea kupwa na kujaa.

Ally ameshauri kivuko cha Kilindoni kiendelee kuwepo, "ila wakati huu Serikiali inapopanga kututengenezea chombo kingine, itutengenezee chombo ambacho kitasafiri kulingana na ratiba mfano kila saa tatu asubuhi chombo kitakua kinatoka Mafia kuelekea Nyamisati na kila saa tisa jion kinatoka huko kurudi ama vyovyote vile ratiba itakavyopangwa.

"Leo mmoja ataambiwa atoke saa nane usiku, kesho mwingine ataambiwa saba, saa 11 ama saa sita usiku muda ambao ni changamoto sana hivyo ili kuepusha adha hiyo kuwepo na vyombo vingine kama vya Baharesa ambavyo vimedizainiwa kufanya kazi muda wowote," amesema Ally.

Awali akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema bajeti ya matengenezo ya barabara za Wakala wa Barabara za Miji na Vijijini (Tarura) mkoani hapa, imeongezeka Sh12. 2 bilioni mwaka 2020/2021 hadi Sh43.1 bilioni mwaka 2021/22 sawa na ingezeko la  asilimia 35 na kwamba hadi sasa fedha zilizopokelewa ni Sh4.7 bilioni.

Kwa upande wa Wakala wa Taifa wa Barabara (Tanroads), amesema imeongezewa fedha kutoka Sh35.9 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh44 bilioni mwaka 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 16  na kwamba hadi sasa fedha zilizopokelewa na Sh5.5 bilioni.

Naye meneja wa Tanroads mkoa huo, Baraka Mwambage, amebainisha kuwa matengenezo ya barabara kwa kazi za 2021/22 hadi kufikia Septemba mwaka huu hakuna fedha zilizotumika kulipa kazi za matengenezo kwa kuwa mikataba ya katengenezo kwa barabara kuu na za mikoa iko kwenye hatua za manunuzi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Tarura mkoa huo, Leopold Runji amesema bado wanaiomba Seriakali kuu kuongeza bajeti na kuendelea kuziomba mamalaka za Serikali za mitaa kuchangia matengenezo ya barabara kwa vyanzo vyao vya mapato ya ndani.