Manusura wa ajali Morogoro wasimulia kilichotokea

Muktasari:

  •  Wakati majeruhi wa basi la abiria la Ahmeed wakisimulia namna ajali ilivyotokea idadi ya vifo kutokana na ajali hiyo imeongezeka na kufikia 23 huku majeruhi 26 wakiendelea kupatiwa matibabu hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.

  

Moro. Wakati majeruhi wa basi la abiria la Ahmeed wakisimulia namna ajali ilivyotokea idadi ya vifo kutokana na ajali hiyo imeongezeka na kufikia 23 huku majeruhi 26 wakiendelea kupatiwa matibabu hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.

Machi 18, 2022 saa 10:30 jioni katika eneo la Meela Kibaoni Wilaya ya Mvomero basi la abiria la Ahmeed lililokuwa likitokea jijini Mbeya kwenda Tanga  liligongana uso kwa uso na lori la IT likitokea Dar es salaam kwenda Congo na kusasabisha vifo na majeruhi.

Majeruhi aliyekuwa kwenye hilo, Halfan Mwinchuma amesema ikiwa imebakia takribani kilometa thelathini kufika Morogoro mjini kutokea Mbeya walikutana na lori la mizigo  na kugongana nalo uso kwa uso.

“Magari yote mawili yalikuwa kwa mwendo kasi, na lori lilionekana kuhama njia yake na kuingia kulia lilipotaka kurudi kwenye njia yake tayari basi aliamua kumkwepa na ndipo walipogongana,”.

Majeruhi huyo amesema tangu amefikishwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro huduma imetolewa vizuri, majeruhi wengine waliokuwa na hali mbaya zaidi wamehudumiwa kwa ukaribu na haraka.

“Mkono wangu una michubuko mingi lakini huduma naendelea kupata ingawa bado sijapata Xray nasubiri daktari atakaponieleza cha kufanya,”amesema majeruhi huyo.

Majeruhi mwingine Bertha Aganila Mwanafunzi wa chuo cha Utumishi Tanga alikuwa akitokea Mafinga amesema kuwa yeye alikuwa amelala na hakuelewa nini kilitokea alishtuka akiwa kwenye gari akikimbizwa hospitali damu zikimtoka puani na usoni.

Mwanahawa Mbarouk aliyekuwa akitokea Mafinga kuelekea Dar es Salaam ambaye alilazimika kuunganisha kutokana na kukosa gari la moja kwa moja ambapo angeshukia Morogoro,

Amesema alikaa siti za nyuma na ajali ilipotokea hakuwa akifahamu kwa sababu alikuwa ameinama na alipoteza fahamu kutokana na ajali na aliposhtuka watu wameshuka anachoshukuru ni kupata msaada wa kutoka kwenye ajali na kufikishwa hospitali.

Mmoja wa  mashuhuda aliyekuwepo eneo la tukio James Juma amesema tatizo la mwendo kasi lilikuwa kwa madereva wote wawili wa basi na lori ambapo ameeleza kuwa dereva wa lori alionekana kutokuwa makini.

“Huyu wa lori hakuwa makini kwanza pale palikuwa eneo la daraja hivyo alitakiwa kwenda mwendo wa kawaida, na hata tahadhari wakati akimkwepa mwendesha bodaboda hakuangalia kama kuna gari inakuja mbele yake,”.


Mkuu wa mkoa wa Morogoro akiwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Morogorol, Martine Shigela ametoa pole kwa ndugu waliopoteza maisha na majeruhi waliolazwa wanaendelea na matibabu huku akiwashukuru wauguzi na madaktari kwa kazi wanayoifanya ya kuhakikisha wanaokoa maisha ya majeruhi hao.