Maofisa wawili Uhamiaji wauawa kwa mishale Mbogwe

Muktasari:

  • Maofisa wa Idara ya Uhamiaji wawili wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wameuawa kwa kupigwa mishale ya sumu inayodaiwa kurushwa na wananchi wa kijiji cha Mtakuja Kata ya Lulembela Wilaya ya Mbogwe.

Mbogwe. Maofisa wa Idara ya Uhamiaji wawili wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wameuawa kwa kupigwa mishale na wananchi wa kijiji cha Mtakuja Kata ya Lulembela Wilaya ya Mbogwe.

Maofisa hao waliofahamika kwa jina moja; Salum na Mtobi wameuawa usiku wa kuamkia leo Jumatano Oktoba 26.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Geita, Emmanuel Lukumay amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ingawa hakutaja sababu za mauaji hayo huku akiahidi kutoa taarifa zaidi baada ya kufika eneo la tukio.

“Nimepata taarifa hizo na hivi sasa niko njiani naenda eneo la tukio. Hadi sasa bado hatujajua sababu za mauaji hayo. Nitatoa taarifa zaidi baada ya kufika huko,” amesema Lukumay


Tukio lilivyotokea


Habari zilizopatikana kutoka kijiji cha Mtakujaa zinasema kuwa maofisa hao waliuawa usiku wa kuamkia leo baada ya kufika kijijini hapo kwa lengo la kuwakamata watu wanaodaiwa kuwa ni wahamiaji haramu ambao walikuwa nyumbani kwa mkazi wa kijiji hicho.

Diwani wa kata ya Lulembela, Deus Lyankando ameiambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa maofisa hao walishambuliwa na wananchi baada ya kuhisiwa kuwa ni majambazi kutokana na kitendo chao cha kuvamia na kuvunja mlango wa nyumba ya mzee Masara Lubadili usiku bila kuambatana na kiongozi yeyote wa kijiji wala kata.

“Baada ya mlango kuvunjwa, waliokuwepo nyumbani kwa mzee Masara Lubadili walihisi wamevamiwa na majambazi na hivyo kupiga yowe kuomba msaada ndipo wananchi walipojitokeza na kuwashambulia maofisa hao,” amesema Diwani Lyankando na kuongeza

 “Niko safari, lakini hizo ndizo taarifa nilizopata kutoka kwa viongozi wenzangu wa kijiji na kata”.

Mkuu wa Uhamiaji Wilaya ya Bukombe, Evarist Roman ambaye tayari yuko eneo la tukio hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo akisema yeye siyo msemaji huku akishauri atafutwe Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Geita, Emmanuel Lukumay ambaye alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kuahidi kutoa taarifa zaidi baadaye.

Wilaya ya Mbogwe inahudumiwa na maofisa Uhamiaji kutoka Wilaya ya Bukombe.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba ambaye pia ndiye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe hakupatikana kuzungumzia tukio hilo baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa.