MAONI: Wanafunzi vyuoni msijasahau

Muktasari:

Zama zimebadilika, kiasi kwamba leo ni kawaida kwa mhitimu wa chuo kikuu kukaa nyumbani kwa miaka kadhaa akisubiria ajira.

Zama zimebadilika, kiasi kwamba leo ni kawaida kwa mhitimu wa chuo kikuu kukaa nyumbani kwa miaka kadhaa akisubiria ajira.

Hali haikuwa hivyo zamani. Kabla hata ya mtu kuhitimu, alishakuwa na uhakika wapi anakwenda kufanya kazi. Ajira zilikuwa ni za uhakika na za kuchagua, tofauti na sasa; ajira zimekuwa suala la bahati.

Mabadiliko hayo ni ya kawaida sio Tanzania pekee, ndivyo ilivyo karibu duniani kote.

Kila kona duniani kilio ni ukosefu wa watu kupata ajira hasa zile zinazojulikana kama ajira rasmi.

Tukiachana na teknolojia kuchukua nafasi za ajira zetu, lakini pia idadi ya wasomi inazidi kuongezeka.

Zamani ungekuta mtaa mzima mwana chuo ni mmoja, lakini leo mtaa mmoja una wahitimu zaidi ya 20. Na idadi inaongezeka kila uchwao.

Nimekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili. Miaka yangu kama mwanafunzi kuna jambo muhimu nilijifunza.

Pengine kwa wewe uliyehitimu tayari linaweza lisikusaidie tena, lakini kwa aliye mwanafunzi lina msaada tosha kwake kama ataamua kulitilia maanani.

Kumaliza chuo sio tukio la dharura. Ni wazi kuwa ukienda chuo leo, baada ya miaka kadhaa utarudi tena mtaani kuendelea na maisha. Swali la kujiuliza ukishamaliza chuo; utaishije huko mtaani?

Maisha ya mtaani yanapaswa kuan za sasa ukiwa bado chuoni. Ishi kama utahitimu chuo, vyuoni kuna makundi yanayonufaika na mikopo ya Serikali. Inawezekana ukawa ni mkopo wa asilimia 100 au pungufu lakini bado utaulipa tu.

Sasa unautumiaje mkopo huo kumudu maisha yako ya chuo na kubaki na ziada kwa ajili ya kuendeshea maisha baada ya kuhitimu?

Kuishi maisha chini ya kipato chako ni mbinu bora zaidi katika kuijali kesho yako.

Kuna wanavyuo maisha yao vyuoni ni kama tayari wamehitimu na wana kazi zao, au wanaishi kama ule mkopo ni bure na wana uhakika kuwa siku wanamaliza tu, ajira wataipata.

Ukiangalia utaona kuanzia utaratibu wa chakula chao, mapambo ya vyumba vyao na uvaaji wao, ni gharama kubwa sana kulinganisha na mkopo wanaopewa, na muda mwingine hujikuta wakiwa kwenye madeni mengi kabla ya kupokea mkopo mwingine. Kwa mtindo huu wapo wanaokosa hata nauli ya kurudia makwao.

Baada ya kuhitimu, kuna maisha kabla ya kupata ajira. Maisha hayo yanahusu kula, kuvaa, sehemu ya kulala na hata nauli za kupeleka barua za maombi katika ofisi au gharama za kutumia mtandao kusaka ajira au kutuma maombi ya kazi.

Maisha yote hayo yanahitaji pesa, sasa ikiwa una mkopo chuoni, achana na imani kuwa pesa haitoshi. Wewe simamia na kufanya mambo chini ya pesa unayopewa.

Unaweza kutunza hata 50,000 kwa kila ingizo la mkopo unalopewa. Kwa miaka utakayokuwa umekaa chuoni, kiasi utakachokuwa umekusanya kitakusukuma kutafuta ajira na kumudu maisha kwa jumla.

Jiulize ikiwa utamaliza chuo na ukapata kazi sawa na ingizo la mkopo kwa mwezi maisha yatakushinda?

Kuna wafanyakazi wanalipwa sawa na wanacholipwa wanafunzi, lakini maisha yanaendelea na ziada wanabaki nayo, kwa nini wewe ushindwe?

Chunguza maisha yako kama kwa siku unaishi kwa gharama ya zaidi ya 8,500 zinazotolewa kwa siku. Jibane uishi hata kwa 5, 000, ili ubaki na 3500, itakusaidia huko baadaye.

Kuna fursa kubwa ambayo kwa sasa ndio ina nafasi kubwa katika kusaidia watu kupata ajira nayo hiyo ni kujitolea. Hivi wahitimu wanaojitolea kufanya kazi katika ofisi, wengi wao ndio huingizwa kwenye mfumo wa ajira iwe taasisi binafsi au za kiserikali.

Maana halisi ya kujitolea ni kufanya kazi bila malipo ya kifedha, sasa utaweza kweli kujitolea ikiwa huna kiasi fyulani cha fedha cha kukusaidia?

Kwa namna yoyote ile ukiweza jitahidi utoke chuo ukiwa na pesa ya kukufanya uishi mtaani kwa miezi sita, ili hata ukipata sehemu ya kujitolea, uwe na uwezo wa kumudu huku ukiomba ndani ya miezi sita wawe wameshakufikiria kuanza kukulipa.

Maisha ya chuo yanapita, maisha halisi yako mtaani, tunajiandaaje?

Saul Kalivubha ni mtaalamu wa tiba, mshauri na mwalimu. 0652 134707