Maporomoka ya matope Mbeya yasababisha shule tano kufungwa

New Content Item (1)

Baadhi ya waathirika wa mafuriko katika kata ya Itezi jijini Mbeya wakiwa katika kambi maalumu katika  Shule ya Msingi Tanbukareli walipowekwa kwa muda, baada ya kutokea maporomoko ya matope yaliyoharibu miundombinu ikiwamo nyumba za baadhi yao. Picha na Sadam Sadick

Muktasari:

  • Kufuatia maporomoko ya tope katika Mlima Kawetele jijini Mbeya, imesababisha shule tano kufungwa kwa muda.

Mbeya. Takribani wanafunzi 3,000 watakosa  masomo baada ya shule tano kufungwa kwa muda, baada ya kutokea kwa maporomoko ya tope kutoka mlima Kawetele katika Kata ya Itezi jijini Mbeya jana.

Shule zilizofungwa ni Tambukareli ambayo kwa sasa inatumika kuweka kambi maalumu ya waathirika, huku Shule ya Mary's, Mafanikio na Itezi Sekondari zikifungwa kwa tahadhari na Generation ambayo imefunikwa na matope.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Aprili 15, 2024 kwa niaba ya Ofisa Elimu wa Jiji la Mbeya, Anderson Mwalongo,  Ofisa Elimu, Vifaa na Takwimu jijini humo, Ally Abdallah amesema shule hizi zimefungwa kwa takribani siku saba.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Amesema kwa sasa wataalamu wa miamba wanaendelea na uchunguzi, wakimaliza na kutoa ripoti, ndipo watajua hatma ya shule hizo.

"Shule ya Generation ilifunikwa na tope hiyo itasimama kwanza na shule za msingi Mary's,  Mafanikio na Itezi  zinafungwa kwa muda kwa tahadhari na Tambukareli inatumika kuwasitiri waathirika,” amesema Abdallah.

Baadhi ya waathirika waliozungumza na Mwananchi Digital wamesema kwa sasa hawajui hatma ya maisha yao, huku wakilalamikia kutoridhishwa na huduma katika kambi hiyo maalumu.

Inocent Eliya aliyepoteza nyumba na mali zote katika mafuriko hayo amesema hajui hatma yake.

"Tunaomba Serikali itusaidie hata mavazi, chakula na mahitaji hatujui hatma yetu kwa sasa, tumepoteza kila kitu hata hapa kambini huduma haziridhishi hatuna hata dawa,” amesema Eliya.

Naye Fortune John amesema bado hawaelewi pa kuanzia; "Hata kama imetokea kwa dharura, lakini sisi ni Watanzania hakuna aliyeomba au kutaka hili litokee, Serikali itusaidie tupate makazi na chakula, mpaka muda huu hatujala kitu chochote,” amelalamika John.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata hiyo, Sambwee Shitambala amesema bado haijajulikana hatma ya waathirika hao kwa sababu ni mapema kulizungumzia hilo kwa leo.

Amesema ndiyo kwanza Serikali imeanza kufanya tathmini, akawaomba wawe wavumilivu hali itakaa sawa.

Hata hivyo, amewaomba wadau na wananchi wengine kujitokeza kwa wingi kuwasaidia waathirika hao wapate huduma za msingi.

"Hapa ni shuleni ina maana vyoo vinatumika vya wanafunzi, maji yanahitajika mengi, dawa na chakula, mablanketi, tunashukuru kamati ya maafa inaendelea kutoa baadhi ya huduma kwa sasa,” amesema Shitambala.

Amesema licha ya kutokuwapo majeruhi wala vifo, lakini wamewaleta wataalamu wa saikolojia ili kuwaandaa vyema waathirika waliopoteza nyumba na mali zao.

Akizungumzia hali hiyo akiwa eneo iliko kambi ya waathirika hao, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Elizabeth Nyema amesema anasubiri ripoti ya maafisa ustawi wa jamii juu ya za waathirika.