VIDEO: Dada asimulia ndugu watano walivyofariki matope Hanang
Muktasari:
- Serikali na wananchi wameungana kwa pamoja kuwaombea wakazi wa Hanang’ mkoani Manyara kutokana na mafuriko ya matope yaliyosababisha vifo vya watu 47, wakiwemo wanafamilia watano.
Dar es Salaam. Maporomoko ya tope yaliyosababishwa na mvua katika Mlima Hanang mkoani Manyara yamesababisha vifo vya watu 49 huku familia ya Magret Daraja ikieleza tope hilo lilivyokatisha uhai wa wanandugu watano.
Akizungumza na Mwananchi, kwa njia ya simu leo Desemba 4,2023, dada wa familia Magreth Daraja amesema ndugu zake watano wamefariki dunia kutokana na maporomoko ya tope Hanang.
“Hapa naelekea Singida kwa ajili ya taratibu za mazishi, ndugu zangu watano wamefariki, mjukuu mmoja, dada kaka wawili na mama, mama alisombwa na tope hadi kwenye mto na akapoteza maisha lakini ndugu zangu wengine wamefukiwa wakiwa ndani,”amesema.
Magreth amesema pia wamepoteza nyumba yao iliyobomoka, mifugo imepoteza maisha, trekta kusombwa na tope.
Mbali na vifo hivyo, tayari watu 93 wameripotiwa kujeruhiwa na tayari Rais Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole na kuelekeza mamlaka zinazohusika kukabiliana na maafa katika katika eneo hilo na tayari vimeanza kazi.
Maporomoko hayo yalisababishwa na mvua iliyoonyesha usiku wa kuamkia jana Jumapili Desemba 3,2023 ambapo sehemu ya Mlima Hanang ilimomonyoka.
Tayari shughuli nyingi za kijamii mkoani Manyara zimesimama na Serikali imeelekeza nguvu eneo la tukio kutoa msaada kwa wananchi na kuopoa miili iliyofukiwa na tope.
Akizungumzia tukio hilo, Mjiolojia wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk Emanuel Kazimoto amesema eneo la Hanang lipo ndani ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki.
“Bonde la ufa la Afrika Mashariki ni ufa mkubwa unaotokea kwenye Bara la Afrika unaoambatana na milipuko ya Volcano na michakato mbalimbali ya kijiolojia, milipuko ya Volcano ndiyo inatengeneza milima ya Volcano kama ilivyo Manyara na maeneo mengine ya bonde la ufa,”amesema.
Amesema milipuko hiyo inapotokea na kutengenezeka kwa milima kutokana na volcano kuna michakato mingine inaendelea ikiwemo kutokea kwa majanga kama ilivyotokea Mlima Hanang.
Kwa upande wake Deus Rashidi mkazi wa Wilaya ya Simajiro, amesema ameshafika eneo la tukio kwa ajili ya kufuatilia taratibu za mazishi ya ndugu zao.
Amesema ndugu hao watano waliofariki miili yao imepatikana yote.
Mtalamu wa Jiolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Emmanuel Kazimoto amesema tukio la Hanang si la kwanza kutokea akitolea mfano tukio lililowahi kutokea na Mlima Meru kuporomoka.
“Yalitokea maporomoko makubwa yaliyotambulika duniani ambapo tani bilioni 55 za mawe ziliporomoka,”amesema.
Ili kujikinga na majanga hayo, Dk Kazimoto amesema Mikoa ya Arusha na Manyara inapaswa kutambua mazingira waliyopo na mambo yanayoweza kutokea .
Amesisitiza kuwa ni muhimu wananchi wanaoishi kwenye mikoa hiyo wakapewa elimu zaidi na kuchukua tahadhari.
“Mfano kufuatilia taarifa za kijiolojia sio tu milima kuporomoka bali kuna milipuko pia inayoweza kutokea, kwahiyo ni muhimu kufuatilia hiyo milima na hatari inayoweza kutokea ili kujiandaa,”amesema.