Vifo vyafikia 49 Hanang, wanajeshi 350 kushiriki uokoaji

Hali ilivyo kwenye mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang' Mkoani Manyara baada ya kutokea mafuriko.

Muktasari:

  • Wakati vifo vilivyosababishwa na maporomoko ya matope vikiongezeka na kufikia 49 wilayani Hanang’, askari 350 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wamewasili kwa ajili ya kusaidia shughuli za uokoaji.

Hanang'. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema wanajeshi 350 kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wamewasili mkoani humo kwa ajili ya kuongeza nguvu ya uokoaji huku vifo vikiongezeka na kufikia 49.

Sendiga ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 4, 2023 wakati akizungumzia kuongezeka kwa vifo hivyo ambavyo hadi jana Desemba 3, 2023 vilikuwa 47 na majeruhi 85.

Amesema  askari na maofisa wa JWTZ ambao ni wataalamu wa uokoaji wameshafika Hanang' na watashiriki shughuli za uokoaji wa watu waliokumbwa na maafa hayo.

Hata hivyo, amesema vituo vitatu vimeshatengwa na Serikali kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa maporomoko hayo.

Ametaja maeneo hayo ni Shule ya Sekondari Ganana, Shule ya Msingi Katesh na Shule ya Msingi Dumananga, ambapo watapata huduma zote za kibinadamu kwa ajili ya kujikimu kimaisha.

"Serikali imetenga maeneo hayo kwa ajili ya malazi, chakula, maji na ulinzi wa kutosha hivyo wale waliopo kwenye maeneo hatarishi ya Gendabi waondoke huko," amesema Sendiga.

Stephen Samoo, mkazi wa Gendabi amempongeza Sendiga na Mkuu wa Wilaya ya Hanang', Janeth Mayanja kwa namna walivyolibeba na kukabiliana na janga hilo.

"Viongozi wetu hao hawakukaa ofisini muda wote walikuwa kwenye eneo la tukio ili kuhakikisha waliokumbwa na janga hilo wanasaidiwa kwa namna moja au nyingine," amesema Samoo.

Mkazi wa Katesh, Sophia John amesema hali ya jana Desemba 3, ilikuwa mbaya kwa wananchi wa Hanang' kwani tukio hilo halijawahi kutokea tangu azaliwe mwaka 1970.

"Watoto walijaa hofu na masikitiko kwani ni jambo ambalo halitaweza kusahaulika kwa miaka ya hivi karibuni kwa wananchi wote wanaoishi kwenye Wilaya ya Hanang'," amesema.

Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji wilayani Hanang', Omary Memba amesema wameendelea kufuatilia maeneo mbalimbali ili kubaini miili ya watu waliopoteza maisha au kujeruhiwa kwenye tukio hilo.

"Pia tunawashukuru viongozi na wananchi wa Hanang' ambao kwa namna moja au nyingine wameshiriki kutusaidia katika kuokoa maisha ya wote waliokumbwa na janga hili kubwa," amesema Memba.

Maporomoko ya matope yaliyoikumba Wilaya ya Hanang’ yalisababishwa na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia Jumapili Desemba 3, 2023 ambapo sehemu ya Mlima Hanang' ulimomonyoka.