Maprofesa, madaktari watawala baraza la JPM

Muktasari:

Baraza hilo, ambalo uteuzi wake umekamilika juzi baada ya kujaza mapengo yaliyokuwapo, lina maprofesa watatu, madaktari wa falsafa wanane na madaktari wawili wa tiba pamoja na wahandisi watano.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amekamilisha uteuzi wa Baraza la Mawaziri ambalo asilimia 53 ya wajumbe wote ni wasomi na wataalamu wa nyanja mbalimbali za kitaaluma.

Baraza hilo, ambalo uteuzi wake umekamilika juzi baada ya kujaza mapengo yaliyokuwapo, lina maprofesa watatu, madaktari wa falsafa wanane na madaktari wawili wa tiba pamoja na wahandisi watano.

Kundi hili pekee lina jumla ya watu 18 ambayo ni sawa na asilimia 53 ya baraza zima lenye mawaziri 34.

Katika baraza hilo yumo Profesa Sospeter Muhongo anayesimamia Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Jumanne Maghembe (Maliasili na Utalii) na Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano).

Licha ya kuunganishwa na wizara nyingine mbili ambazo ni uchukuzi na mawasiliano, Dk Magufuli amemkabidhi Profesa Mbarawa mikoba ya ujenzi, kazi aliyoifanya kabla hajanyakua kiti hicho cha juu katika uongozi wa Taifa.

Katika mgawanyo wa majukumu mapya, zipo baadhi ya wizara ambazo Rais amewaweka wabobezi hao kwa pamoja. Mathalan, Wizara ya Nishati na Madini itasimamiwa na Profesa Muhongo atakayesaidiwa na Dk Medard Kalemani.

Rais pia amewakabidhi madaktari wawili kuiongoza Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.

Hao ni Dk Augustine Mahiga atakayesaidiwa na Dk Suzan Kolimba.

Ipo pia Wizara ya Fedha na Mipango ambayo itaongozwa na Dk Philip Mpango huku naibu wake akiwa Dk Ashantu Kijaji.

Profesa Mbarawa atasaidiwa katika Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Mhandisi Edwin Ngonyani wakati Profesa Maghembe atasaidiwa na Mhandisi Ramo Makani Maliasili na Utalii huku Dk Joyce Ndalichako akishirikiana na Mhandisi Stella Manyanya kuiongoza Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.

Wizara ya Maji na Umwagiliaji inaongozwa na wahandisi watupu, Gerson Lwenge na naibu wake, Isack Kamwelwe.

Mwanasheria, Dk Harrison Mwakyembe ataongoza peke yake Wizara ya Katiba na Sheria kama ilivyo kwa Dk Hussein Mwinyi ambaye ni tabibu katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto itakuwa chini ya mwanasheria Ummy Mwalimu akisadiwa na Dk Hamis Kigwangalla ambaye ni tabibu.

Mawaziri wengine isipokuwa wachache, wana elimu za juu. Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba anaendelea na masomo yake ya Shahada ya Uzamivu katika Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mawaziri wengine wenye shahada za uzamili ni George Simbachawene (Utawala), January Makamba (Diplomasia na Usuluhishi wa Migogoro), Nape Nnauye (Utawala), Angelina Mabula (Uhasibu), Charles Mwijage (Masoko) na Angela Kairuki (Stashahada ya Uzamili ya Sheria) na William Lukuvi.

Matarajio ya wananchi kwa wasomi hao.

Wananchi wa kada mbalimbali wamekuwa na maoni tofauti juu ya matarajio yao kwenye baraza hilo lililosheheni wasomi.

Mhadhiri mwandamizi wa UDSM, Dk Omari Mbura alisema elimu ni moja ya vigezo vya uteuzi ambavyo vimezingatiwa na mkuu wa nchi kuchagua wasaidizi wake.

“Uwezo na uzoefu wa mtu binafsi katika utawala wa umma ni kitu muhimu kinachoongezeka kwenye elimu ya darasani.

Naona ujasiriamali miongoni mwao. Wengi ni watu wa uamuzi binafsi, hiki ni kigezo kikubwa kwa mtumishi wa ngazi ya waziri. Ni imani yangu kuwa kwa miaka mitano ijayo wataweza kukata kiu ya wananchi kwa utumishi uliotukuka,” alisema Dk Mbura.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kampala, Goodluck Mwashilindi alihadharisha kuwa watu wenye elimu kubwa wanaweza kuleta janga endapo wataamua kufanya hujuma kwa mfumo uliopo.

“Maarifa mengi waliyonayo ni rahisi sana kung’amua upungufu wa kimfumo. Kama watasema waibe basi itakuwa ni kwa matumizi ya akili nyingi ambayo inaweza ikachukua muda mrefu kugundulika. Lakini wakiwa wazalendo na wakaamua kuwahudumia wananchi, Taifa litaneemeka,” alisema Mwashilindi.

Mwanasheria na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili UDSM, Racheal Jonas alisema: “Natarajia mabadiliko. Uteuzi umebeba watu wanaoweza kukabiliana na changamoto zilizopo.”

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue alisema kuwa mawaziri wote na naibu waziri walioteuliwa wataapishwa Jumatatu saa tatu asubuhi, Ikulu.