Mapya biashara ya mkojo wa wajawazito

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya wamesema hakuna ukweli kuwa mkojo wa wajawazito unaweza kutumika kutengeneza tiba ya magonjwa ya binadamu kama inavyodai Kampuni ya Polai (Tz) CO LTD inayokusanya mikojo hiyo.

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wamesema hakuna ukweli  kuwa mkojo wa wajawazito unaweza kutumika kutengeneza tiba ya magonjwa ya binadamu kama inavyodai Kampuni ya  Polai (Tz) CO LTD inayokusanya  mikojo hiyo.

David Myemba, Mfamasia na Mkufunzi wa Shule ya Famasia kutoka Chuo Kikuu Muhimbili (Muhas) alisema anachofahamu ni kuwa mikojo ya wajawazito hutumika kuonesha mimba, maendeleo ya mtoto tumboni, ukuaji wake pamoja na uzito atakaozaliwa nao.

Jana gazeti hili liliripoti habari ya uchunguzi wa siku 14 uliobaini  kuwa ukusanyaji wa mikojo hiyo unafanyika kwa usiri mkubwa mkoani hapa, kwa wajawazito ambao hufuatwa majumbani na kushawishiwa kukubali.

Mikojo hiyo hukusanywa na huwekwa kwenye vikopo kisha kupelekwa kwenye nyumba iliyopo Mtaa wa Mferejini Kata ya Manzese, kabla ya kupelekwa kwa raia wa kigeni anayetajwa kuwa mmiliki wa kampuni hiyo Kampuni hiyo imeeleza kuwa ndani ya mikojo hiyo kuna homoni aina ya Human Chorionic Gonadotropin (HCG), Human Menopausal Gonadotrophins (HMG) na urokinase ambazo ndizo hutumika kutengeneza dawa hizo.

Mikojo hiyo hukusanywa na huwekwa kwenye vikopo kisha  kampuni hiyo iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam huichukua kwa maelezo kuwa wanaitumia kutengeneza dawa.

Katika maelezo yake Myemba alisema pia mikojo ya wajawazito hutumika kuonesha kama mtu ana maambukizi ya U.T.I, magonjwa mengine ya kuambukiza na kuonesha mzunguko wa hedhi hususani ovulation stage.

“Kiukweli kuhusu mkojo wa mama mjamzito kutumika kutengeneza dawa hapo sifahamu,” alisema Dk. Myemba

Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake Hospitali ya Mwananyamala, Daniel Mkungu alisema homoni zilizotajwa na kampuni hiyo ni kweli zinapatikana kwenye mkojo au damu lakini hafahamu kama zinaweza kutengeneza dawa hizo za binadamu.

“Kama wanakusanya mikojo kwenye visado wanapaswa kuulizwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kama kisheria jambo hilo ni sahihi,” alisema Dk. Mkungu.

Mratibu wa shughuli ya ukusanyaji wa mikojo hiyo mtaa wa Mferejini Amri Kizyala alikaririwa akisema kuwa wajawazito hao uwapatiwa vikopo vidogo vya kuweka mikojo hiyo na uwataka kuileta kila siku asubuhi ili kuweza kukusanywa kwa pamoja na kupelekwa mahali husika.

Hata hivyo Kiazyala alisema kila mwisho wa mwezi wajawazito hao upatiwa zawadi za vyakula ambazo ni sukari, mchele, unga, sabuni kama motisha kwao kuendelea kutoa mikojo.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake Hospitali ya Rufaa ya KCMC Mwanza, Benjamin Shayo alisema anafahamu kuwa zipo homoni kama hizo katika mikojo ya wajawazito, ila hatambui ni kwa namna gani zinatengenezwa kama dawa kwa ajili ya tiba.

Alisema hajawahi kusoma au kufuatilia ni kwa namna gani homoni hizo zinatengenezwa ili zije kutumika kama dawa tiba ya magonjwa ya binadamu.

“Mimi binafsi sijawahi kusoma wala kufatilia wanatengeneza vipi na wanazipataje hizo homoni, hivyo itoshe kukwambia kuwa sifahamu kama homoni hizo zinaweza kutengeneza dawa kwa ajili ya tiba za kiharusi,” alisema