Prime
Mapya DC aliyetenguliwa na Rais Samia
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini (DC), Komanya Kitwala.
Muktasari:
- Mahakama ya Rufani imethibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba hata Rais anawajibika kutoa sababu anapomstaafisha mtumishi wa umma kwa msingi wa “masilahi ya umma.”
Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani Tanzania imepigilia msumari wa mwisho katika hukumu ya Mahakama Kuu iliyoweka msimamo wa kisheria kuhusu mamlaka ya Rais kumstaafisha mtumishi wa umma kwa kigezo cha “masilahi ya umma” bila kutoa sababu.
Katika hukumu hiyo, Mahakama ya Rufani, ikiwa ndiyo chombo cha juu cha utoaji haki nchini na uamuzi wake kuwa wa mwisho, imethibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba hata Rais anawajibika kutoa sababu anapomstaafisha mtumishi wa umma kwa msingi wa “masilahi ya umma”.
Mahakama hiyo imetoa msisitizo huo katika huku ya rufaa iliyowasilishwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), dhidi ya aliyekuwa Ofisa wa Sheria wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Awali, Mahakama Kuu ilitengua uamuzi wa Rais wa kumstaafisha mtumishi huyo kwa masilahi ya umma bila kueleza sababu mahsusi, ikisema kuwa dhana ya “masilahi ya umma” ni pana na hivyo inahitaji kufafanuliwa kwa kina ili kuepusha matumizi holela.
Mbali na hilo, Mahakama Kuu ilielekeza Katibu Mkuu Utumishi kumrejesha Kitwala katika nafasi yake ya awali ndani ya PSSSF, alikokuwa akifanya kazi kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora, nafasi ambayo baadaye aliondolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na hatimaye kustaafishwa utumishi wa umma.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Utumishi pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hawakuridhishwa na uamuzi huo, hivyo wakakata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu.
Katika uamuzi uliotolewa Mei 5, 2026, jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani – Dk Gerald Ndika, Zainab Muruke na Agnes Mgeyekwa, limesisitiza kuwa wajibu wa kutoa sababu ni sehemu ya msingi katika maamuzi yote yanayoathiri haki za mtu binafsi.
Mahakama hiyo imebainisha kuwa kigezo cha “masilahi ya umma” pekee hakitoshi kisheria bila kuambatana na maelezo yanayoeleza sababu za uamuzi husika.
Sababu za rufaa
Warufani ambao waliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Deodatus Nyoni, Edwin Webiro na Erigh Rumisha waliwasilisha sababu nne za rufaa.
Katika sababu ya kwanza ya rufaa, mawakili hao walijenga hoja kuwa, Mahakama Kuu ilikosea kisheria kwa kushikilia kwamba Rais ana wajibu wa kutoa sababu za kumuondoa mtumishi wa umma kwenye utumishi kwa masilahi ya umma.
Katika sababu ya pili walieleza kuwa Mahakama Kuu ilikosea kisheria na ukweli kwa kutoa ahueni ambayo haikubaliki chini ya mapitio ya mahakama.
Sababu ya tatu ni kwamba, Mahakama Kuu ilikosea kisheria na ukweli kwa kutoa nafuu ambayo haikutafutwa na mwombaji katika wito wa chemba.
Kwamba, Mahakama Kuu ilikosea kisheria kwa kushindwa kuchukua na kuzingatia mawasilisho ya wakili wa warufani juu ya tofauti kati ya kuondolewa kwenye utumishi wa umma (removal) na kufukuzwa kazi kwa makosa ya nidhamu.
Akikazia sababu hizo, Wakili Nyoni alisema Ibara ya 36 (1) na (2) na Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298 na Kanuni za Utumishi wa Umma hazipendekezi kwamba Rais atoe sababu wakati akitumia mamlaka hayo.
Hivyo, ni hoja yake kwamba Mahakama Kuu ilikosea kwa kusema kuwa haikuwa sahihi kumwondoa mtumishi huyo bila kueleza sababu zozote na kuwa pale mtumishi wa umma anapoarifiwa kuondolewa kazini kwa masilahi ya umma, kwamba hilo neno ‘masilahi ya umma’ linatosha kuwa ndiyo sababu.
Hata hivyo, Wakili wa Kitwala; Jeremiah Mtobesya alipinga hoja hizo akisema Kitwala hakuwa ameondolewa katika utumishi wa umma alipochukuliwa PSSSF, bali aliazimwa (kwenda kuwa DC); na kwamba mawakili wanachanganya nadharia mbili, kuondolewa na kufukuzwa.
Mtobesya alieleza kuwa amri ya mapitio ya mahakama inapokubaliwa na kubatilisha uamuzi wa Rais uliopingwa, kilichobaki ni kurejesha suala hilo katika misingi yake halali ya kuangalia upya maombi ya mombaji ambayo ni kurejeshwa kazini PSSSF.
Hukumu ya Majaji
Katika hukumu yao, Mahakama ya Rufani imesema kuwa imeshawishika na hoja za Wakili Mtobesya kwamba wajibu wa kutoa sababu si suala la uzuri wa utaratibu, bali ni muhimu katika kanuni za haki, uwazi na uwajibikaji.
“Kama ilivyoelezwa ipasavyo katika kesi ya James Gwagilo dhidi ya AG, matumizi ya madaraka ya umma lazima yaambatane na sababu, hasa pale ambapo uamuzi husika unaathiri vibaya haki au matarajio halali ya mtumishi wa umma,” walisema.
“Tuko sawa na Mheshimiwa Nyoni (wakili wa Serikali) kwa kiasi, kwamba masharti yaliyotajwa ibara ya 36 ya Katiba, Sheria na Kanuni za utumishi wa umma, hakika yanampa Rais mamlaka ya kuondoa mtumishi wa umma kwa masilahi ya umma,” wamesema.
Hata hivyo, walisema mamlaka hayo hayaondoi wajibu wa kutoa sababu za kufanya hivyo. Lakini ukitazama barua aliyotumiwa Kitwala, imeeleza tu kuwa amestaafishwa kwa manufaa ya umma bila kufafanua, hiyo haikidhi kiwango kinachohitajika kisheria.
“Kwa maoni yetu, mtoa maamuzi (Rais) alikuwa chini ya wajibu wa kutoa sababu, si kama suala la fomu, lakini kama kipengele muhimu cha hatua halali na ya haki ya kiutawala,” wamesisitiza majaji hao.
“Sharti la kutoa sababu limejikita sana katika kanuni za kikatiba. Inamwezesha mhusika kuelewa msingi wa uamuzi, kuwezesha utekelezaji wa haki ya kuupinga, na hutumika kama kinga dhidi ya uzembe na matumizi mabaya ya madaraka”.
“Kwa hivyo, tunakubaliana na Jaji wa mahakama Kuu (Mkwizu) kwamba wajibu wa kutoa sababu ni kipengele cha lazima cha uamuzi wowote wa haki unaoathiri haki za mtu binafsi. “Masilahi ya umma” haiwezi kutosha kama sababu katika sheria.”
"Kwa hiyo, hatuwezi kukubaliana na hoja ya Wakili Nyoni kwamba Rais hana wajibu wa kutoa sababu,” walisisitiza na kuongeza kuwa:-
“Katika muktadha huo, Ibara ya 33 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inayohakikisha haki ya utawala bora, haiwezi kusomwa kwa ufinyu; badala yake, lazima ipewe tafsiri ya kimakusudi inayokuza uwazi, uwajibikaji na haki katika utendaji wa mamlaka ya utendaji.
“Kwa hivyo, tumeridhika kwamba Mahakama Kuu haiwezi kulaumiwa kwa kushikilia kuwa uamuzi huo uliopingwa uliharibiwa na kushindwa kutoa sababu. Hoja hizi (za warufani) hazina mashiko na zimetupiliwa mbali," wamesema.
Hata hivyo katika sababu ya pili na tatu ya rufaa, majaji hao wamekubaliana na hoja ya Wakili Webiro kwamba masharti ya utoaji wa amri za mapitio ya mahakama kama zilivyotatuliwa, hazikufikiwa katika hali ya kesi hii.
“Kwa maoni yetu, mara Mahakama Kuu ilipotoa amri hiyo ya certiorari (amri ya mahakama ya juu inayotolewa kuipitia upya na hatimaye kufuta au kubatilisha uamuzi wa chombo cha chini), haikupaswa kwenda mbali zaidi.
Kwa kuendelea kutoa amri ya mandamus (amri ya mahakama inayokitaka au kukiamuru chombo cha umma, afisa wa serikali au taasisi ya umma kutekeleza wajibu wake wa kisheria ambao imeshindwa au imekataa kuutekeleza), Jaji msomi alianguka katika makosa,” wamesema majaji hao.
“Kwa hivyo, agizo hilo haliwezi kusimama badala yake tunaelekeza kwamba utaratibu ufaao uchukuliwe kwa mamlaka husika kuamua, kwa mujibu wa sheria, kuhusu hali ya ajira ya mwombaji,” wamesisitiza majaji hao.
“Kwa hatua ya mwisho, kwa njia hii tunabatilisha, kwa sehemu, hukumu ya Mahakama Kuu pamoja na maagizo yote yanayotokana na hayo. Kwa hivyo, rufaa inafanikiwa kwa sehemu kwa kiwango kilichoonyeshwa,” wameeleza.
Kitwala alikuwa mtumishi wa umma akiwa Ofisa Sheria wa PSSSF kati ya Julai 30, 2010 hadi Julai 30, 2018 alipoteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mkuu wa Wilaya ya Tabora.
Hata hivyo, alihudumu katika wadhifa huo U-DC hadi Novemba 18, 2021 alipotenguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na baada ya kutenguliwa, aliandika barua kwa Katibu Mkuu Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili arejeshwe PSSSF.
Badala ya kurejeshwa katika nafasi yake ya awali PSSSF alikoazimwa na kupelekwa kuwa DC Tabora Mjini, Agosti 15,2022 alipokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu utumishi akimjulisha kuwa Rais amemstaafisha kwa masilahi ya umma.
Kitwala alifungua shauri la mapitio ya kimahakama kupinga uamuzi huo wa Rais wa kustaafishwa bila kuelezwa sababu.
Pia aliomba mahakama itoe amri ya kumshurutisha Katibu Mkuu Utumishi kumrejesha katika ajira aliyokuwa nayo kabla ya kuteuliwa kuwa DC na alipwe malimbikizo yake yote ya mishahara kuanzia Juni 28, 2021 hadi tarehe yake kurejeshwa.
Mahakama Kuu katika uamuzi uliotolewa Februari 8, 2024 na Jaji Elizabeth Mkwizu ilikubaliana na hoja za Kitwala ikatengua uamuzi huo wa Rais.
Jaji Mkwizu alisema kumstaafisha mtumishi utumishi wa umma kwa maelezo ya masilahi ya umma bila kueleza sababu ni kinyume na matakwa ya utawala bora na kuamuru arejeshwe kazini.
Wadaiwa hawakuridhika na uamuzi huo, wakakata rufaa hii.