Mapya yaibuka mwanafunzi aliyepotea, mwili kukutwa kwenye shimo la choo

Muktasari:

  • Polisi laeleza uchunguzi wa awali unaonyesha aliuawa, msako waendelea kuwanasa waliohusika.

Kibaha. Wakati familia ya mwanafunzi Angel John aliyekutwa amekufa ndani ya shimo la choo Kibaha, mkoani Pwani, ikiendelea na taratibu za mazishi, Polisi limesema kuna uwezekano mkubwa kuwa aliuawa.

Kutokana na hilo, Polisi limesema linawasaka waliohusika wa mauaji ya mtoto huyo mwenye miaka minane.

Angel aliyekuwa akisoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Carisa mjini Kibaha alipotea Mei 6, 2024 alipomfuata dada yake aliyekuwa ameenda kusuka jirani na makazi yao.

Mwili wake ulipatikana Mei 7, 2024 ndani ya shimo la choo akiwa amefariki dunia.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Mei 9, 2024 imesema Jeshi hilo linaendelea na msako kumpata mtu au watu waliohusika na mauaji hayo, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Amesema kuna uwezekano mkubwa kuwa mwanafunzi huyo aliuawa kisha kutumbukizwa kwenye shimo hilo la choo.

"Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kiuchunguzi umebaini mtoto huyo aliuawa na kisha kutumbukizwa kwenye shimo hilo, tofauti na taarifa iliyotolewa awali," inaeleza taarifa hiyo.”

"Hivyo, Jeshi la Polisi limeshaanza msako kuwatafuta watu au mtu aliyehusika na tukio hilo," amesema.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 9, 2024 Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwendapole, Muhidini Muhidini amesema usiku wa Mei 8, kuna watu walifika mtaani hapo wakijitambulisha ni askari Polisi.

Amesema waliambatana naye hadi kwenye nyumba ya mkazi mmoja wa mtaa huo anayedaiwa awali alieleza amepata maono kuwa mtoto huyo yuko kwenye shimo la choo.

"Nasikia huyo mtu wakati mtoto anatafutwa yeye alisema amepata ufahamu kupitia maono kuwa mwanafunzi huyo yupo kwenye shimo la choo na baadaye kweli alikutwa huko," amedai.

Amesema walipowasili kwenye makazi ya mtu huyo anayeishi jirani na familia ya marehemu hawakumkuta ikaelezwa amesafiri.

Hata hivyo, Kamanda Lutumo alipopigiwa simu kuzungumzia suala hilo, hakukubali au kukataa, bali amesema si kila hatua za uchunguzi lazima zianikwe.

Akizungumza na Mwananchi Digital Mei 7, 2024 baba mzazi wa mwanafunzi huyo, Mseveni John alisema alipata taarifa za mwanaye kupotea aliporejea nyumbani akitoka kazini saa 11.00 jioni.

"Niliporudi kutoka kazini niliambiwa mwanangu amepotea tukaenda polisi kutoa taarifa, lakini wakatuambia hawawezi kupokea taarifa ya tukio ambalo halijamaliza saa 24, hivyo tulirudi tukaendelee kumtafuta," alisema.

Mseveni ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Tumbi alisema walimtafuta usiku mzima wakipita mitaa kadhaa hakupatikana.

Alisema asubuhi ya Mei 7, 2024 mwili wake ulikutwa ndani ya shimo la choo ambacho hakijaanza kutumika.

Mseveni alisema eneo ulipokutwa mwili walipita hapo usiku zaidi ya mara mbili lakini hawakuona chochote.

"Ni jambo la kushangaza, hapo kwenye shimo tulipita mara mbili usiku hatukuona chochote wala dalili yoyote, lakini asubuhi tukaona mwili ndani ya shimo, hili linaleta maswali mengi kwetu," alisema.