Mapya yaibuka ripoti watoto njiti kutolewa viungo

Tabora. Mkuu wa Mkoa Tabora (RC), Balozi Batilda Burian amesema uchunguzi wa awali wa vifo vya mapacha waliozaliwa kabla ya wakati katika Kituo cha Afya Kaliua mkoani Tabora umebaini watoto hao walihifadhiwa chumba cha wauguzi na sio wodi ya wazazi.

Pia, Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa huo amesema, idadi ya watumishi waliosimamishwa kutokana na sakata hilo wamefikia wanne na watafikishwa mahakamani wakati wowote kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mkuu huyo wa mkoa amesema hayo kipindi ambacho familia ya mapacha hao ikiongozwa na baba wa watoto hao, Kisaka Raphael kugoma kuchukua miili kwenda kuizika akitaka watuhumiwa wakamatwe kwanza.

Mei 9 mwaka huu katika kituo cha afya Kaliua, Musaneza Benson (25) alijifungua pacha waliodaiwa kufariki muda mfupi baadaye na siku iliyofuata maiti moja ilikutwa imenyofolewa baadhi ya viungo vya mwili kama kung’olewa macho, kukatwa ulimi na kuchunwa ngozi kwenye paji la uso.

Kutokana na hatua hiyo na mijadala kushika kasi mitandaoni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alijitokeza na kusema hatua zimeanza kuchukuliwa hatua ikiwemo kusimamishwa kazi.

Licha ya Serikali kutangaza hatua hiyo na uchunguzi, baba watoto hao, Raphael pamoja na Kiongozi wa familia hiyo ambaye ni babu wa watoto hao, Alex Paul Nyika wameweka msimamo wa kutochukua miili kwenda kuizika hadi hatua zichukuliwe na waone kwa macho zimechukuliwa.

Miili ya watoto hao bado imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Urambo ambako pia kulifanyika uchunguzi wa miili yao.

Jana, RC Burian akizungumza na gazeti hili kuhusu suala hilo alisema watumishi waliosimamishwa wamefikia wanne baada ya kuagiza wengine wawili nao kuunganishwa na wenzao

"Nimemuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kaliua kuwasimamisha kazi watumishi wengine wawili," alisema RC huyo

Mkuu huyo wa mkoa alisema uchunguzi umeonesha miili ya watoto hao ilihifadhiwa katika chumba cha wauguzi na sio katika wodi ya wazazi kama ilivyoelezwa awali kwa maana wahusika walidanganya.

"…kwanza tulipata taarifa za awali kwamba wauguzi wetu wale wawili waliosimamishwa walitoa taarifa watoto wale walikuwa katika wodi ya wazazi wote lakini baada ya kufikishwa polisi na upelelezi kuendelea ikabainika watoto wale walikuwa chumba cha wauguzi," alisema

Aliwataja watumishi hao waliosimamishwa na watafikishwa mahakamani wakati wowote ni Theresia Kakiziba, Asha Majid, Pauk James na Benson Maikase.

Baada ya kauli hiyo, gazeti hili lilizungumza na Babu wa watoto hao ambaye pia ni msemaji wa familia, Alex Paul Nyika alieleza kushukuru uamuzi wa mkuu wa mkoa akisema anadhani sasa wamebaini ukweli.

Alisema kwa sasa wanasubiri watumishi hao kufikishwa mahakamani na leo au kesho nao sasa wamepanga kuwazika watoto hao.

Hata hivyo, alitoa angalizo kama watumishi hao hawatafikishwa mahakamani, wao wataendelea na msimamo wao wa kutoichukua miili na kuizika.

"Tunapongeza namna Mkuu wa Mkoa alivyobaini ukweli na kufahamu upotoshaji waliopewa awali hivyo tutazika Alhamisi kama wahusika wakifikishwa kweli mahakamani," alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi alisema uchunguzi wa shauri hilo umekamilika na jalada la shauri hilo linatarajia kufikishwa kwa mwanasheria mkuu wa Serikali leo,

Alisema katika uchunguzi wao, Jeshi la polisi limewahoji watu wengi ambao walitoa ushirikiano mkubwa.

"Kwa upande wetu sisi kama Jeshi la Polisi, tayari tumekamilisha uchunguzi wetu ambao ulihusisha idadi kubwa ya watu," alisema

Kwa mujibu wa kaimu kamanda huyo, ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali ndio itaamua lini shauri hilo litafikishwa mahakamani.

Wiki iliyopita, gazeti hili lilizungumza na Mkurugenzi Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dk Ahmed Makuwani ambaye alitaja hatua zinazopaswa kuchukuliwa na wataalamu wa afya mara baada ya mtoto/watoto kuzaliwa kabla ya wakati yaani njiti.

Dk Makuwani alifafanua kile ambacho kilitakiwa kufanyika mara baada ya watoto hao kuzaliwa.

Alisema rufaa kwa mama aliyejifungua watoto au mtoto chini ya umri wa mimba inategemea hali ya mama na hali ya mtoto na ngazi ya kituo cha huduma alichopo kama ni zahanati, kituo cha afya na hospitali.

Dk Makuwani alisema endapo mama amejifungua katika kituo ambapo hakuna huduma za watoto njiti, mama atapewa rufaa kwenda kwenye kituo chenye huduma za watoto wachanga wagonjwa na njiti (NCU).

"Kabla ya rufaa mtoto hupatiwa huduma za kabla ya rufaa ili kuimarisha afya yake kabla ya kumsafirisha.

"Muongozo unaelekeza mtoto njiti ambaye ana uzito wa gramu 1800 kwenda juu ambao hawana changamoto nyingine wanaweza kuhudumiwa katika vituo vya afya vyenye huduma za Mama Kangaroo," alisema Dk Makuwani.