Ummy aingilia madai watoto njiti kutolewa macho

Dar es Salaam. Watoto pacha waliozaliwa kabla ya wakati (njiti) wamedaiwa kung’olewa macho, kukatwa ulimi na kuchunwa ngozi kwenye paji la uso katika Kituo cha Afya Kaliua.

Watoto hao waliozaliwa kutokana na mimba ya miezi saba, wanadaiwa kufanyiwa ukatili huo Mei 9, 2023.

Kufuatia tukio hilo lililosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema jana kuwa hatua zimeanza kuchukuliwa.

“Tumelifuatilia suala hili, kuna ukweli. Uongozi wa Wilaya ya Kaliua umeshaanza kuchukua hatua. Baadhi ya watumishi wa afya waliomhudumia mama huyu wameshasimamishwa kazi.

“Nakemea vikali kitendo hiki. Ninamuagiza Mganga Mkuu wa Tabora kusimamia vyema weledi, maadili na miiko ya watumishi wa afya,” alisema Waziri ummy.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya mtandaoni, baba wa pacha hao, Kisaka Mtoisenga, mkazi wa Ushikola, Kaliua, Tabora alisema Mei 9, 2023 saa 4 usiku mke wake alijifungua salama watoto pacha katika Kituo cha Afya Kaliua wakati huo ujauzito ukiwa na umri wa miezi saba.

Alisema kwa kuwa Kituo cha Afya Kaliua hakina uwezo wa kuhudumia watoto njiti, waliwapa rufaa kwenda hospitali teule ya wilaya yenye mashine za kuhudumia watoto njiti na kwa kuwa kituo hakina gari la wagonjwa, waliambiwa wakatafute usafiri.

“Nikamuacha mke wangu na watoto wakiwa wazima wa afya, nikaenda kutafuta usafiri. Muda huo haikuwa rahisi kupata gari, nikapata bajaji. Tulipofika wahudumu wakasema tusubiri wawaandae watoto. Tukasubiri hadi saa tano dereva akaanza kulalamika,” alisimulia.

Alisema wahudumu wakasema waendelee kusubiri na ilipofika saa sita, dereva akataka kuondoka na alipowauliza kwa mara nyingine walimweleza kuwa wanamalizia kuwaandaa watoto.

Mtoisenga alisema alimwambia dereva angemuongezea malipo, hivyo asubiri kidogo na baadaye wahudumu wakatoka na kuwaambia bahati mbaya watoto wamefariki, hivyo wakawaahidi kuwapatia miili yao kesho yake asubuhi.

“Asubuhi wakatupatia maiti zikiwa ndani ya maboksi tukiwa kwenye chumba maalumu cha upasuaji, ambacho kina giza. Wakatusisitiza tukazike siku hiyohiyo kwa haraka kwa sababu watoto njiti hawafanyiwi msiba.

“Tulipofika nje kabla ya kupanda gari tukafungua maboksi. Tukakuta watoto wameng'olewa macho, wamekatwa ulimi na wamechunwa ngozi kwenye paji la uso. Tukahamaki. Tukarudi kuuliza nini kimetokea, hawakutupa majibu ya kuridhisha,” alisema Mtoisenga.

Alisema baada ya hapo walikwenda Kituo cha Polisi, lakini nako wakaambiwa wakazike tu maana wao hawashughuliki na ushirikina. Na walipojaribu kwenda kwa mkuu wa wilaya, alipoona maiti akasema huo ni ushirikina.

“Akatushauri tukazike tu maana hata tukienda mahakamani hatuwezi kushinda. Nikamuuliza kwa nini ushirikina ufanyike hospitalini? Nikakataa kuzika.

“Nikataka uchunguzi ufanyike. Mkuu wa Wilaya akaagiza maiti zipelekwe hospitali ya Urambo. Hadi leo zipo huko sijui nini kinaendelea.

“Watoto wangu wametendewa unyama kwenye kituo cha afya, halafu nanyimwa haki kwa kisingizio cha ushirikina? Naumia sana,” alisema Mtoisenga.

Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Rashid Chuachua hakupatikana alipotafutwa kupitia simu yake kiganjani jana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo alisema, “tukio hili ninalifahamu. Hatua tuliyoichukua ni kufungua jalada la uchunguzi ambao unaendelea kwa sasa.

Aliitaja namba ya jalada hilo kuwa ni KAU/PE/18/2023.